Home Kitaifa Miaka 20 ya Mtibwa Sugar katika VPL, mataji mawili na ‘ukubwa wao’...

Miaka 20 ya Mtibwa Sugar katika VPL, mataji mawili na ‘ukubwa wao’ baada ya Yanga na Simba

5809
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

MIAKA 29 tangu kuanzishwa kwake, klabu bingwa mara mbili ya zamani ya Tanzania Bara, Mtibwa Sugar FC ipo katika msimu wake wa 20 wa ligi kuu Bara.

“Niliingia katika timu ya Mtibwa wakati ambao kiwanda cha Mtibwa Sugar kilipobinafsishwa mwishoni mwa mwaka 1998 ndiyo tukaanza usajili kwa msimu wa 1999. Ifahamike timu ilianza kucheza ligi kuu ikiwa chini ya mwekezaji mpya mwaka 1999 na ikafanikiwa kushinda ubingwa wake wa kwanza msimu wa pili ikicheza ligi kuu na ndiyo timu ya kwanza kutoka nje ya Yanga na Simba kutetea ubingwa. Tulifanya hivyo msimu wa mwaka 2000.” anasema, Jamal Bayser kiongozi wa muda mrefu wa klabu hiyo wakati nilipofanya naye mahojiano marefu kuhusu misimu 20 ya klabu ya Mtibwa Sugar FC katika tangu ilipopanda ligi kuu.

Miaka 9 katika madaraja ya chini

Mtibwa Sugar ilianza kuonyesha matamanio ya dhati ya kucheza ligi kuu miaka mitano tu baada ya kuanzishwa kwake mwaka 1988.

Hilo lilipelekea kuanza kuwasaini wachezaji wakali. Salhina Mjengwa mmoja wa wafungaji bora wa muda wote klabuni hapo, John Thomas Masaki ambaye alikuwa mfungaji mkali kutokea Singida, Said Msham aliyesajiliwa kutoka Majimaji, Christopher Michael aliyetokea Tiger ya Tunduma, Loui John, Kassim Mwabuda ambao walisajiliwa kutokea Coastal ya Tanga wote hawa walisajiliwa mwaka 1995 wakati ambao klabu iliamua kwa dhati kuitoa timu hiyo katika ligi daraja la tatu hadi ligi kuu.

Usajili ‘bab-kubwa’ waipa taji la kwanza

Abubakary Mkangwa alikuwa mchezaji-mfungaji aliyekuwa akichipukia vizuri , Moja Liseki, Yusuph Macho, golikipa Steven Nemes, Zubeiry Katwila wote hawa walikuwa mastaa waliosajiliwa kutoka Yanga na Simba na kocha John Simkoko kwa msaada wa mratibu wa timu hiyo Jamal Bayser mwaka 1998.

Mlinzi wa kushoto Kassim Issa naye alisajiliwa mwaka huo na kuungana na kina Mjengwa, Masamaki, Geofrey Magori, Mayanga, Meck Mexime na wengineo.

Siku ya mwisho wa msimu wa 1999 katika mchezo wa kukumbukwa sana katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa mara ya kwanza Mtibwa Sugar FC ikatawazwa kuwa mabingwa wa ligi kuu baada ya kuifunga Yanga 2-1 katika mchezo wa kusisimua ambao hadi kufikia dakika ya 86 ilionekana wazi Yanga wanakwenda kushinda ubingwa wa nne mfululizo kwani walikuwa mbele kwa goli 1-0 na matokeo hayo ama sare yalikuwa yakiwapa taji lingine baada ya kutwaa mfululizo misimu ya 1996, 1997 na 1998.

“Hii timu imetoka mbali sana” anasema,  Mkangwa nilipofanya naye mahojiano akiwa nchini Italia ambako anaendeleza harakati zake za kutafuta kipato. “ Sitasita kuwataja baadhi ya watu walisaidia timu hii kufika hapa ilipo sasa.”

“Naweza kumtaja mtu mmoja kwanza, Mayanga kocha wa sasa wa timu ya Taifa. Mayanga ametoka nayo sana timu hii, nakumbuka toka  ligi daraja la tatu. Marehemu Said Mhando pia ni kati ya watu walisaidia sana kuifikisha Mtibwa hapa ilipo sasa. Wakati tunatwaa ubingwa wa kwanza mwaka 1999 Mayanga alikuwa mchezaji, lakini mara nyingi alikuwa akimsaidia kocha Simkoko.” Anaongeza kusema mshambulizi  huyo wa zamani wa Taifa Stars.

“Licha ya kwamba kuna nyakati nyingi nzuri ninazikumbuka kama vile kuishi kifamilia, kwa kweli siwezi kusahau mechi yetu dhidi ya Yanga ambayo Kassim Issa anafunga magoli mawili ya haraka haraka dakika za mwisho na kuipa timu ubingwa wa kwanza. Yanga walikuwa wakihitaji sare ili kushinda ubingwa na walikuwa tayari wanaongoza mchezo hadi kufikia dakika tatu kabla ya kumalizika, lakini mambo yalikuja kugeuka dakika za majeruhi . sitasahau ubingwa ule. Tulikuwa na kikosi kikali sana wakati ule” Anasema Mkangwa mfungaji bora wa ligi kuu bara mwaka 2004.

Timu ya kwanza kutoka nje ya Yanga na Simba kutetea ubingwa wa ligi kuu bara

Mara baada ya kikosi cha Simkoko kushinda ubingwa wa kwanza wa ligi kuu mwaka 1999 ikiwa ni miaka miwili tangu wapande ligi kuu mwaka 1997, timu hiyo iliendeleza makali yake na kufanikiwa kumaliza juu ya Yanga na Simba na kutwaa ubingwa wa ligi kuu mwaka 2000.

“Usajili mzuri tuliofanya kipindi hicho na maandalizi mazuri kabla ya kuanza kwa msimu ndiyo sababu kubwa iliyotupa ubingwa wa kwanza na wa pili mfululizo ikiwa ni muda mfupi  tu baada ya kupanda daraja. Unajua sisi timu yetu hukaa kambini msimu mzima na siyo kwa ajili ya maandalizi ya mechi Fulani tu. Nakumbuka Prisons ndiyo timu iliyokuwa ikitupa sana tabu kwa sababu nao walikuwa ‘fit’ kama sisi, lakini Yanga na Simba hazikuwa zikitusumbua.” Anasema Bayser

Mecky Maxime mchezaji ‘alisi’ wa Mtibwa

Mara baada ya kustaafu soka msimu wa 2010/11, mlinzi bora zaidi wa muda wote wa klabu ya Mtibwa Sugar, Mecky Mexime alipewa kazi ya kumsaidia Mkenya Tom Olaba katika benchi la ufundi.  Mexime ni alama hasa ya Mtibwa na kijana ambaye alijitolea kwa nguvu na akili zake zote kwa miaka 18 mfululizo tangu alipoingia akiwa kinda mwaka 1993.

Amechezea Mtibwa katika kila hatua wakati ikiwa katika madaraja ya chini, ameshinda mataji yote ambayo klabu imewahi kushinda (ligi kuu mara mbili, Tusker Cup mara moja, Mapinduzi Cup mara moja, Ngao ya Jamii mara moja, kombe la FA mara moja)

Licha ya uwepo wa watu muhimu kama Bayser, Mayanga, Mjengwa, ila Mexime ni mtu ambaye anatazamwa kama jasiri aliyependa sana kuifanyia kazi jamii yake. Yanga na Simba zote ziliwahi kumfuata ili zimsaidi mlinzi huyo bora zaidi wa kulia kuwahi kutokea Afrika Mashariki kwa wakati wake. Aliipenda Mtibwa na klabu inamuheshimu hadi sasa.

Ameshaonyesha mwanga kuwa anaweza kufuata nyayo za Simkoko na Mayanga siku moja akiwa kocha wa klabu hiyo. Misimu yake mitatu kama kocha mkuu aliweza kuonyesha namna gani alivyo na uwezo wa kuwakusanya vijana wa mji mmoja wenye vipaji na kuwatengeneza kuwa wachezaji wakali.

Sasa yupo katika msimu wake wa tano kama kocha katika ligi kuu Bara na msimu huu ni wa pili kwake klabuni Kagera Sugar ambako aliwasogeza hadi nafasi ya tatu msimu uliopita huku yeye akishinda tuzo ya kocha bora wa msimu.

Wafungaji bora wanne VPL

Masamaki, Mhando, Mkangwa, na Abdalla Juma wote hawa wamewahi kushinda tuzo ya ufungaji bora wa ligi kuu bara wakiwa wachezaji wa Mtibwa Sugar lakini isisahaulike kuwa Monja, Omary Matutta hadi sasa  kizazi cha Hussein Javu klabu hiyo imekuwa ikitoa washambuliaji-wafungaji wakali nchini.

Hadi tuzo ya kipa bora wa msimu

Mtibwa imeshatoa wachezaji wawili ambao wamefanikiwa kushinda tuzo ya golikipa bora wa msimu. Shaaban Kado msimu wa 2008/09 na Hussein Shariff msimu wa 2013/14. Ukiachana na washindi hao wawili wa tuzo binafsi katika kipindi cha miaka yao 20 ya ushiriki wa VPL klabu hiyo imekuwa ikiwainua walinda mlango wengi bora na sasa wanaimairisha kiwango cha kijana Benedict Tinoco.

Iliwahi kuingia mitini caf na ndiyo mwanzo wa kupotea kwao

Ikicheza kwa mara ya kwanza michuano ya Caf mwaka 2004 Mtibwa Sugar ilifanya ‘kituko’ cha aina yake baada ya kutopeleka timu jijini Cape Town kwa ajili ya mchezo wa marejeano dhidi ya Santos FC. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika hapa nyumbani Mtibwa ilichapwa 3-0 na hivyo walihitaji ushindi unaoanzia magoli manne ugenini.

Kitendo hicho kiliwafanya wafungiwe na Caf miaka isiyopungua mitatu kucheza michuano yoyote ya Shirikisho hilo la soka Afrika. Inawezekana jambo hilo ndilo lilichangia kwa kiasi kikubwa kupoteza dira ya ushindani kwa Mtibwa kwani walianza kusajili wachezaji wa kawaida kwa kisingizio kuwa hata wakifanya vizuri  katika ligi hawatakuwa na mahala pa kwenda kushindana kimataifa.

Kwa nini Simba na Yanga hawachezi Manungu, kwanini wamekimbia Jamhuri vs timu ndogo?

“Nakumbu Yanga na Simba zimeshawahi kuja kuja Manungu na hapakuwahi kutokea tatito lolote lile. Udogo wa uwanja wetu si tatizo. Ifahamike kuwa kutokucheza Mangungu kwa Yanga na Simba hivi sasa kulitokana na maamuzi yetu sababu tuliona Jamhuri tutapata mapato zaidi.” Anasema mratibu wa timu hiyo Jamal Bayser

“ Kuna wakati tulihamishia Jamhuri michezo yetu yote ya nyumbani lakini gharama na ubovu wa uwanja huo zilichangia kuachana nao na kuendelea kutumia uwanja wa Manungu isipokuwa kwa mechi dhidi ya timu hizo zenye ushawishi mkubwa pia.”

Miaka 13  mfululizo ya kudorora kwao, Mtibwa inaweza kuibuka mwaka 2017 VPL

Tangu mwaka 2003 waliposhindwa kuifungwa Twiga katika siku ya mwisho ya msimu ili kutwaa ubingwa wao wa tatu, Mtibwa haijajaribu tena kuwa tishio dhidi ya Simba na Yanga huku Azam FC ambao inacheza msimu wake wa tisa ikiwa na taji moja ikimaliza ndani ya nafasi mbili za juu mara nne mfululizo tangu msimu wa 2011/12 walipofanya hivyo kwa mara ya kwanza.

Licha ya kwamba wakati ule ikishinda mataji mawili mfululizo ya VPL, Prisons, Majimaji FC pia zikiwa na nguvu lakini sasa kitendo cha timu hiyo kushindwa kuweka mkazo katika nia ya ubingwa kimewaacha wakiangaika katika nafasi za katikati ya msimamo tangu mwaka 2005.

“Tunaweza kuamka tena na kushinda ubingwa msimu huu. Hakuna kisichowezekana” anaongeza kusema Bayser ambaye tupo katika klabu hiyo kwa miaka 18 mfululizo na kuipa mafanikio makubwa.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here