Home Kitaifa Nicholas Gyan, yale maneno yao matamu, yana damu mikononi mwao!

Nicholas Gyan, yale maneno yao matamu, yana damu mikononi mwao!

6307
0
SHARE

Na Halidi Mtumbuka

Miaka ya 1744 hadi 1829 kulikua na mwanasayansi mmoja anaejulikana kwa jina la Jean-Baptiste Lamarck. Huyu bwana alikuja na sheria moja rahisi sana lakini ni ngumu mno kueleweka kwa urahisi kama ilivyo. Huyu bwana alikuja na dhana iliyokua ikielezea ni kwa jinsi gani kitu kikitumika ipasavyo kinakua na nguvu na kinaendelea kujikuza chenyewe. Yaani kitu kinachotumika huendelea kuishi milele. Upande wa pili wa dhana yake hiyo ilikua ikijaribu kuelezea juu ya kitu kisichotumika ipasavyo, au kinachotumika mara chache chache tu.

Lamarck alisema kuwa kitu kisichotumika kamwe hupotea. Yaani hufa. Mfano wake mzuri ulikua ni namna ambavyo Twiga huitumia shingo yake. Kwa mujibu wa dhana hio ya Lamarck, miaka mingi iliyopita, Twiga hakua na shingo ndefu kama ilivyo hivi sasa, isipokua mabadiliko ya maisha kwa maana majani ya chini yalipoanza kupungua ilimlazimu mnyama Twiga kuanza kutafuna majani ya juu ya miti, hivyo ndivyo ambavyo mnyama huyo alivyoanza taratiibu kuirefusha shingo yake bila mwernyewe kujijua na hatimae hii leo, Twiga ndie mnyama mwenye shingo ndefu zaidi.

Unapoitafakari kwa kina dhana ya bwana Lamarck kisha ukailinganisha mikono yako miwili, kati ya hiyo upi una nguvu kuliko mwingine? Kwanini? Kiasi fulani unaweza kumuelewa tu Lamarck, hofu yangu ni juu ya kipaji cha Nicholas Gyan! Hakitumiki hivi sasa, hivi hakiwezi kupotea kweli au kupoteza ubora wake ule uliomfanya kusajiliwa na Simba kutoka nchini Ghana? Gyan ni kilikua ni kipaji chenye hatari yake huko kwenye Ligi Kuu ya nchini Ghana mpaka Simba akafanikiwa kuweka windo lake na kufanikiwa kuinasa saini yake, hakuwa wa kipole pole Ghana.

Rekodi iliyowavutia Simba ni ile ya kufunga mabao yake 11 na kutoa pasi zake tatu za mabao msimu ule aliposajiliwa. Hii ilikua ni rekodi ambayo ingemfanya mtu yeyote yule kuvutiwa na uwezo wake huo ukizingatia kuwa Ghana ni taifa linalozalisha wachezaji wengi wanaokwenda kucheza soka barani Ulaya au hata waliozagaa duniani kote na barani Afrika. Simba haikuwa na mtu ambae alihitaji kwanza kujiridhisha endapo aina ya uchezaji wake ingetosha kumfanya aingie moja kwa moja kwenye kikosi chao hivyo rekodi tu zilitosha kabisa kuamini wamelamba dume.

Hili ni moja kati ya mambo yanayofanya wachezaji wengi wa kimataifa kusajiliwa tu mithili ya magari au nguo kutoka nje ya nchi. Kwenye mpira wa miguu huwa kunachezwa kamari kubwa mno kuliko hata kamari yenyewe. Huwa hakuna uhakika nyota anaesajiliwa ataingia moja kwa moja kikosini au atasubiri kwana. Hakuna ukweli wa wazi wa sababu zao za kushindwa kuingia moja kwa moja kikosini. Mwisho wa siku hata akiondoka huwa ni haki kuliko kusalia na kufanya vizuri. Akifanya vizuri huwa ni afueni lakini huwerzi kutamba mbele ya vyombo vya habari kuwa atafanya vizuri.

Gyan, matumbo yetu yanauma bwana. Chakula ulichoanza kukipika tangu utue Tanzania hakioneshi ishara yoyote ya kuiva wala kupakuliwa na hatimaye kiingie kwenye midomo yetu. Lini utaanza kutushibisha? Maisha ya kusubiri yana changamoto moja kubwa, endapo ukiamua kukisubiri kitu kwa hamu, ni sharti uuone muda hausongi mbele, ndio! Kila siku kesho, kesho, kesho itafika lini? Hiyo ahadi ya mama kuku na wanawe tumeshaichoka bwana, tunachokihitaji kwa sasa kutoka kwako ni kuanza kutuonesha thamani ya fedha zako za usajili kutoka Ghana.

Ulisajiliwa kwenye kikosi chenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 tangu dirisha lililopita ili uje kufunga mabao uje kuondoa ukame kwenye safu ya mbele ya Simba ambayo ilikumbwa na ukame mkubwa sana kipindi kile. Usitembelee nyota ya wachezaji wenzako wanaofunga mabao ili kutimiza adhma yako ya kuchukua fedha za Tanzania, hio si sawa kabisa Nicholas Gyan, maisha hayapo hivyo kabisa Gyan. Ni lazima utuoneshe thamani yako, ni lazima ucheze mpira kwenye Ligi ya Tanzania ili tupate walau cha kukijadili juu ya uwezo wako bwana.

Kuamua kukaa benchi kutatufanya tugawanyike pande mbili, kwanza huna uwezo wa kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Simba. Ndio, ni lazima tuwaze hivi kwa kuwa siku zote kocha humchunguza mchezaji wake kuanzia kwenye viwanja vya mazoezi na hapo ndipo huwa na uhakika kuwa unaweza kuingia kwenye kikosi chake au kinyume chake. Ukimya wako unatuacha na wasiwasi pia kama huenda ulisajiliwa kwa ajili ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika tu ambalo Simba itashiriki kuanzia mwakani, tuamini hivyo?

Lakini kama huku tu kwa kina Tanzania Prisons, Ruvu Shooting, Mbeya City au hata Kagera Sugar hupati nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza, utatushawishi vipi tukupe nafasi kwenye michezo mikubwa barani Afrika? Haiingii kwenye akili zetu bwana Nicholas Gyan, inasemekana kwamba kimya kingi kina mshindo, hatuna budi kuziandaa ngoma za masikio yetu kusubiri huo mshindo wako, ila kumbuka utapotuletea kishindo na si mshindo, wakati huohuo itabidi utangulie Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, hutakua na fursa ya kunyanyua mdomo wako na kuulizia mizigo yako, itakua tayari huko ikisubiri tu ujio wako muanze safari.

Hivi unafikiri yale maneno yao matamu wakati wakikukaribisha na wengine wakipokea mizigo yako pale Uwanja wa Ndege yalimaanisha hilo? Hawakua sahihi hata kidogo kama uliwaza hivyo! Usitegemee furaha wakati ambapo ukishindwa kutoa mchango tulioutegemea Nicholas Gyan, usitegemee kabisa. Yale maneno yao yalikua na ishara za damu kwenye mikono yao, yaani hawa ni watu ambao wanaweza kumuua nyani bila kumuangalia usoni ndio maana mikono yao ilitapaa damu nyingi. Muulize tu Danny Sserunkuma, Amissi Tambwe na Gilberb Kaze watakusimulia kila kitu. Tumechoka kusubiri, kinachofuata unakijua? Hata mimi sikifahamu, acha tusubiri!

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here