Home Kitaifa Niyonzima yuleyule majukumu tofauti

Niyonzima yuleyule majukumu tofauti

13215
0
SHARE

Usajili wa Haruna Niyonzima kujiunga na Simba ulizungumzwa sana na kutawala mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari, lakini baada ya kutua Msimbazi kuna baadhi ya watu wanaamini kwamba nyota huyo ameporomoka kiwango kwa sababu tu amekuwa hazungumzwi na hafanyi yale ambayo aliyafanya wakati yupo Yanga.

Kinachowasumbua watu wengi ni kushindwa kutambua kuwa, vilabu hivi viwili vinatofautia falsafa za kiuchezaji, vinafundishwa na walimu tofauti, lakini pia wachezaji wanapewa majukumu tofauti kulingana na mahitaji ya kocha na timu kwa ujumla.

Siku moja Amri Kiemba aliwahi kuniambia, viongozi wa klabu yake (Simba) waliwahi kumlaumu wakisema, akiwa kwenye klabu hachezi kama ambavyo anacheza akiwa na timu ya taifa ‘Taifa Stars’ (wakimaanisha anafanya vizuri sana akiwa Stars kuliko anapokuwa Simba) jambo ambalo lilizua mjadala mzito kati yake na viongozi hao.

Alichowajibu Kiemba ni kwamba, timu hizo mbili zinafundishwa na makocha tofauti wenye falsafa tofauti, majuku anayopewa akiwa Stars ni tofauti na yale anayopewa akiwa Simba lakini pia akiwa Stars anakutana na wachezaji tofauti na wale anaocheza nao kwenye klabu.

Alichoniambia Kiemba ndio hiki ambacho nakiona kwa Niyonzima, watu wanamhukumu akiwa Simba kwa kutolea mifano namna alivyokuwa akicheza wakati yupo Yanga, siungi mkono kwamba Niyonzima uwezo wake umeshuka bali anatumika tofauti na alivyotumiwa akiwa Yanga na hili sio kosa ni jambo la kiufundi zaidi.

Namna ambavyo Yanga ilikuwa ikicheza ilikuwa inamfanya Niyonzima aweze kuwa na mpira kwa muda mwingi. Yanga ilitengenezwa kwa kumzunguka Niyonzima ndiyo maana kila lilipo tukio la mpira Niyonzima alikuwepo kwa sababu yeye alikuwa anaangalia zaidi eneo la mbele kwa ajili ya kusambaza mipira hivyo alikuwa huru zaidi.

Kuna kipindi alikuwa akichezshwa kama namba 10 lakini akiwa chini kidogo ‘shimoni’ kwa hiyo mipira yote ilikuwa inapita kwake kwenda kwa kina Msuva na washambuliaji wengine.

Kwa sasa yupo Simba amekutana na kocha mwenye falsafa tofauti, wakati mwingine inawezekana amepewa majukumu mengine na hapewi uhuru kama aliokuwanao wakati akiwa Yanga kutokana na sababu za kiufundi za kocha mpya aliyekutana nae.

Simba wana viungo wengi ambao wanaweza kuuchezea mpira tofauti na Yanga ambao kwa namna wanavyocheza, kuna wakati Yanga walikuwa wakicheza wakiwa na walinzi wa kati watatu (Twite, Cannavaro na Yondani) maana yake Niyonzima alikuwa na uhuru mkubwa wa kuichezesha timu tofauti na Simba ambayo inawachezeshaji wengi.

Kwa sasa unaweza ukaona ‘touches’ anazofanya Niyonzima akiwa Simba ni chache kulingana na staili ya uchezaji wa klabu hiyo kwa sababu timu nzima wanacheza pasi. Inawezekana kwa namna watu walivyomzoea Niyonzima huenda wakaona anacheza chini ya kiwango wakitaka kulinganisha na namna alivyokuwa anacheza wakati yupo Yanga. Ni kumuonea.

Kiuhalisia anaisaidia timu ndiyo maana inaongoza ligi na imekusanya pointi za kutosha na kufunga magoli ya kutosha, Niyonzima ni yuleyule majukumu tofauti.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here