Home Kitaifa Ibrahim MO au Domayo utakuwa usajili bab-kubwa Yanga si Mohamed Issa ‘Banka’

Ibrahim MO au Domayo utakuwa usajili bab-kubwa Yanga si Mohamed Issa ‘Banka’

23791
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

MABINGWA mara tatu mfululizo wa ligi kuu Tanzania Bara, timu ya Yanga inapaswa kurejea sokoni wakati huu wa usajili wa dirisha dogo na kusaini mchezaji mmoja wa kiwango cha juu ama wawili. Yanga inahitaji mfungaji mpya kuelekea michuano ya Caf mwezi Februari, 2018 na pengine kocha Mzambia George Lwandamina anaweza kusaini kiungo mmoja wa kati mwenye uzoefu kama atalazimika kufanya hivyo.

Kukosekana kwa washambuliaji wa kigeni Mrundi, Amis Tambwe ambaye hajacheza mchezo wowote msimu huu kutokana na majeraha ya goti, Mzimbabwe, Donald Ngoma ambaye alicheza michezo minne tu na kupata maumivu yanayosemekana kuwa ya nyama za  paja na namna wachezaji hao wanavyoendelea kupona napata wasiwasi mkubwa kama Yanga inaweza kufikia malengo bila nyongeza ya mfungaji.

Matheo Anthony ameshindwa kupenya katika kikosi, Emmanuel Martin si mfungaji na kuendelea kutegemea magoli ya Ibrahim Ajib na Obrey Chirwa pekee katika VPL na michuano ya Caf na ile ya FA ni jambo ambalo linaweza kuwayumbisha hasa nikichukulia mfano wa kile kilichowatokea msimu uliopita waliposhindwa kuiondoa timu ya kawaida Zanaco FC kutoka Zambia katika Caf Champions league.

Yanga ilishindwa kuwaondoa Wazambia na kufuzu kwa hatua ya makundi kwa sababu haikuwa na safu imara ya ushambuliaji kutokana na majeraha ambayo yalikuwa yakiwaandama Tambwe, Ngoma, Chirwa. Licha ya kufanikiwa kuhifadhi ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya tatu mfululizo Mei, 2017 lakini bado michezo yao saba ya mwisho katika ligi ilikuwa migumu na hilo lilichangiwa na idadi ya chini ya magoli waliyokuwa wakifunga.

Stamili Mbonde

Lwandamina anaweza kutazama mbali zaidi na kusaini mfungaji wa kutoka nje ya nchi, lakini anaweza kumtazama mshambulizi wa Mtibwa Sugar FC, Stamili Mbonde ambaye si tu anaweza kucheza vizuri mbele ya lango la timu pinzani, bali ana uwezo wa kudhibiti mpira, kutoa pasi  na kutengeneza nafasi za kufunga.

Mbonde amefunga magoli mawili tu msimu huu, lakini anacheza katika kikosi ambacho hakitengenezi nafasi  nyingi za kufunga. Msimu mmoja uliopita Yanga ilimsaini, Paul Nonga kutoka Mwadui FC kwa kuamini mshambuliaji huyo angeweza kuwa msaidizi mzuri wa kina Tambwe na Ngoma lakini hakufanya vizuri.

Mbonde si Nonga kwa sababu kwanza ni kijana anayeanza kukomaa katika soka wakati Nonga ni mchezaji aliyepanga kustaafu soka ndani ya misimu miwili ijayo. Wanaweza kuongeza mfungaji toka ng’ambo ya nchi kama atapatikana lakini ‘mtu huyu’ mwenye mwili mkubwa anaweza kufanya vizuri sasa na baadae.

Frank Domayo

Kumrudisha Frank Domayo katika kikosi cha Yanga wakati huu ni bora zaidi kuliko kumsaini Mohamed Issa ‘Banka’ kutoka Mtibwa Sugar. Domayo anaweza kukosa nafasi katika timu ya kwanza pale Azam FC lakini ni mchezaji ambaye anaweza kutumia uzoefu wake kutengeneza muunganiko mzuri sambamba na Mcongoman, Papy Tshishimbi na Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.

Sioni kitu kipya kutoka kwa Mohamed Issa ikiwa atasajiliwa kwa sababu Rafael Daud, Pius Buswita wamesajiliwa kwa ajili ya kuunganisha timu kutoka kati mwa uwanja hadi kwa washambuliaji. Hawajafanya vibaya hadi sasa na naona wakienda kujiamini zaidi na itakapotokea hivyo watakuwa
msaada mkubwa katika utengenezaji wa magoli.

Kama jaribio la kuwasaini Said Ndemla, Mohamed Ibrahim kutoka Simba litafanikiwa itakuwa jambo zuri sana kwa kocha Lwandamina lakini akishindwa kuwapata wachezesha timu hao anaweza kumtazama Domayo ambaye alifanya mambo makubwa wakati angali kinda katika timu hiyo. Sasa amepevuka, na Yanga inahitaji mchezaji bora mwenye uzoefu katika kiungo na si chipukizi.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here