Home Kitaifa Singida Utd vs Yanga, vita ya Pluijm na Lwandamina kuthibitisha ubora wa...

Singida Utd vs Yanga, vita ya Pluijm na Lwandamina kuthibitisha ubora wa mbinu

2488
0
SHARE

Mechi ya Singida United vs Yanga inapambwa na makocha wa timu hizo Hans van der Pluijm kwa upande wa Singida United na George Lwandamina kwa upande wa kikosi cha Yanga. Kumbuka ujio wa Lwandamina ndio ulimng’oa Pluijm ndani ya Yanga licha ya kuipa timu hiyo mafanikio ya soka la ndani na kimataifa lakini bado alilazimika kumpisha mzambia Lwandamina aliyetokea Zesco United ya nchini kwao.

Mwezi November, 2016 Lwandamina alitambulishwa rasmi kuwa kocha mpya wa Yanga huku Pluijm akipewa kitengo cha ukurugenzi wa ufundi kwenye klabu hiyo baada ya kubadili maamuzi ya kujiuzulu nafasi ya ukocha ndani ya Yanga.

Miezi michache baadae Pluijm alichukuliwa na Singida United kuwa kocha mkuu baada ya klabu hiyo kupanda daraja kucheza VPL na kuachana na klabu ya Yanga ambayo ameipa heshima kubwa huku na yeye jina lake likinawiri kupitia klabu hiyo kongwe nchini.

Leo Jumamosi November 4, 2017 Singida United inakutana dhidi ya Yanga kwenye uwanja wa Namfua Singida katika mchezo wa VPL, kupitia mchezo huu Hans van Pluijm atakutana na Lwandamina ambaye alichukua nafasi yake Yanga, ni mechi ya mafahari wawili kuoneshana umwamba wa mbinu uwanjani.

Pluijm atakuwa akicheza kwa mara ya kwanza dhidi ya timu iliyomleta nchini, www.shaffihDauda.co.tz imeandaa takwimu za Singida United na Yanga msimu huu zikiwa chini ya makocha hao ambao kila mmoja atalazimika kudhihirisha ubora wake kwa mwingine.

Lwandamina (Yanga)

Ameiongoza Yanga katika mechi nane za msimu huu, amekusanya jumla ya alama 16 akiwa ameshinda mechi nne, sare nne huku timu yake ikiwa bado haijapoteza mchezo tangu kuanza kwa ligi. Yanga imefunga jumla ya magoli 11 kuhu ikiwa imeruhusu magoli manne na kufanya wastani wake wa magoli kuwa ni +7.

Katika mechi nane ambazo Yanga imecheza, michezo minne kati ya hiyo ilikuwa viwanja vya ugenini (nje ya Dar) huku mechi nne nyingine ikizicheza kwenye uwanja wa nyumbani (Uhuru, Dar).

Pointi nyingi ugenini

Yanga imekuwa hatari zaidi inapocheza ugenini kwa sababu katika mechi nne za ugenini imeshinda mechi tatu na kutoka sare mchezo mmoja na kuvuna jumla ya pointi 10 huku pointi nyingine sita ikizipata uwanja wa nyumbani

 • Njombe Mji 0-1 Yanga
 • Majimaji 1-1 Yanga
 • Kagera Sugar 1-2 Yanga
 • Stand United 0-4 Yanga

Magoli mengi ugenini

Magoli mengi ya Yanga yamefungwa ugenini, jumla ya magoli nane kati ya 11 yamefungwa kwenye viwanja vya ugenini, wamefanikiwa kufunga goli kwenye kila mechi waliyocheza ugenini hata ile ambayo wametoka sare.

Kutoruhusu magoli (cleen sheets)

Yanga haijaruhusu goli katika mechi nne kati ya nane ambazo imeshacheza hadi sasa, mechi mbili kati ya hizo ni ugenini (Njombe Mji 0-1 Yanga na Stand United 0-4 Yanga) pia imefanya hivyo katika mechi zake mbili za nyumbani (Yanga 1-0 Ndanda) na Yanga 0-0 Mtibwa Sugar).

Matokeo ya mechi tatu zilizopita

Katika mechi tatu zilizopita, Yanga imeshinda michezo miwili na kutoka sare mmoja, michezo ambayo Yanga imeshinda ni ya ugenini na nyumbani mmoja, wanaingia kwenye mchezo dhidi ya Singida wakiwa wanajiamini kutokana na mfululizo wa matokeo yaliyopita.

 • Kagera Sugar 1-2 Yanga
 • Stand United 0-4 Yanga
 • Yanga 1-1 Simba

Pluijm (Singida United)

Singida United chini ya Hans van der Pluijm imefanya vizuri hadi sasa ikiwa na alama 13 katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa VPL pointi tatu nyuma ya wapinzani wao wa leo Yanga walio nafasi ya pili kwenye msimamo. Katika mechi nane ambazo imecheza, imeshinda mechi tatu, imepoteza moja na kutoka sare katika mechi nne.

Singida ilikuwa ikiutumia uwanja wa Jamhuri Dodoma kama uwanja wa nyumbani kwa sababu uwanja wao wa Namfua ulikuwa unafanyiwa ukarabati mkubwa, kwa hiyo mechi zao za nyumbani nitakuwa nikimaanisha walizocheza uwanja wa wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Kikosi cha Hans kimecheza mechi tatu uwanja wa nyumbani, kimeshinda mechi mbili na kutoka sare mchezo mmoja, mechi nyingine tano kikicheza ugenini.

Singida wamepata pointi nyingi kwenye uwanja wa nyumbani

Wamekusanya pointi saba katika mechi tatu walizocheza nyumbani huku pointi sita wakizipata kwenye michezo ya ugenini. Singida imecheza michezo michache ikitumia uwanja wa nyumbani (mechi tatu) huku ikicheza mechi tano ugenini. Kwa kifupi matokeo mazuri wamepata nyumbani kwa sababu wameshinda mechi mbili na sare moja.

 • Singida United 2-1 Mbao
 • Singida United 1-0 Kagera Sugar
 • Singida United 1-1 Azam

Magoli ya Singida ni ‘pasu kwa pasu’

Katika magoli sita waliyofunga kwenye ligi hadi sasa, matatu wamefunga kwenye uwanja wa nyumbani na mengine matatu wakiwa ugenini. Singida imeruhusu magoli manne kwa hiyo inawastani wa magoli +2.

Kutoruhusu magoli (cleen sheets)

Singida imecheza mechi tano bila kuruhusu goli katika mechi nane, katika mechi zake za nyumbani haijaruhusu goli kwenye mchezo mmoja kati ya michezo mitatu (Singida 1-0 Kagera Sugar), mechi nyingine mbili wameruhusu magoli, imecheza mechi nne bila kufungwa goli ikiwa ugenini katika mechi tano kwa maana hiyo, Singida wanafungika zaidi nyumbani kuliko ugenini.

Matokeo ya mechi tatu zilizopita

Katika mechi nne zilizopita, Singida United haijashinda mechi hata moja, pia haijafanikiwa kufunga goli hata moja katika mechi zake tatu zilizopita wakati huohuo yenyewe haijaruhusu goli wala kupoteza, mechi zote imetoka suluhu (0-0).

 • Ruvu Shooting 0-0 Singida United
 • Ndanda 0-0 Singida United
 • Mtibwa Sugar 0-0 Singida United

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here