Home Kitaifa “Tunacheza katika muonekano wa kisu, Bodi ya ligi iwalinde wachezaji wasiolipwa mishahara...

“Tunacheza katika muonekano wa kisu, Bodi ya ligi iwalinde wachezaji wasiolipwa mishahara VPL”-Amri Said

4796
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

LIPULI FC ilifanikiwa kupata ushindi wa pili msimu huu katika ligi kuu ya Tanzania baada ya kuifunga 1-0 Majimaji FC siku ya Jumamosi iliyopita katika uwanja wa nyumbani (Samora Stadium.) Ushindi huo umeipeleka timu hiyo hadi nafasi 8 wakiwa wamefunga kila kitu na Ndanda FC.

Timu hizo mbili zimekusanya pointi 9 kila moja huku kila timu ikiwa imefunga magoli manne na kufungwa manne. Kama ilivyo kwa Ndanda FC, timu ya Lipuli nayo imepoteza game mbili, sare tatu na kushinda michezo miwili katika michezo 7 iliyopita.

Jumapili hii nilifanya mahojiano marefu na kocha mkuu wa kikosi hicho, Amri Said ‘Stam’ ambaye ni mshindi wa mataji ya ligi ya kuu Tanzania mwaka 1998 akiwa na Majimaji FC, VPL 2001, 2003 na 2004 akiwa Simba SC.

Amri ameichukua timu hiyo baada ya kurejea ligi kuu na amezungumzia mambo mbalimbali yanayoendelea kikosini mwake na katika ligi kiujumla. Hii ni sehemu ya mahojiano hayo

www.shaffihdauda.co.tz: Habari yako mwalimu?

Amri Said: Namshukuru Mungu niko salama. Sijui hali yako?

www.shaffihdauda.co.tz: Nashukuru pia mambo yanakwenda. Nafuatilia sana timu yako, napendezwa na mwendo wenu katika michezo hii saba iliyopita.

Amri Said: Asante sana.

www.shaffihdauda.co.tz: Unaizungumziaje ligi baada ya game saba za mwanzo?

Amri Said: Ligi ni ngumu na bado tuna changamoto kadhaa, unajua timu yetu ilichelewa kufanya usajili jambo ambalo lilipelekea tuchelewe pia katika maandalizi ya msimu. Kwa ufupi hatukuwa na maandalizi ya kutosha kabla ya ligi kuanza.

Unajua hivi sasa ukitazama katika ligi yetu kuna makocha kadhaa raia wa Burundi. Wingi wao unatokana na kufanya vizuri na kutimiza malengo yao katika timu wanazozifundisha. Sasa ni kupambana nao ili kudhihirisha uwezo wetu sisi kama makocha wazawa. Tunapaswa kutimiza malengo yetu na klabu.

www.shaffihdauda.co.tz: Ni kupambana nao tu Mwalimu.

Amri Said: Ndio tunachofanya hapa Lipuli FC nikiwa na wenzangu wakiongozwa na Selemani Matola. Kama unavyojua niliichukua timu hii wakati ambao muda umeshakwenda na ligi ilikuwa karibu kuanza, hivyo muda wetu mwingi kama benchi la ufundi tumekuwa tukiutumia kuimarisha kikosi chetu.

www.shaffihdauda.co.tz: Unafanya nini ili kwenda sawa na hali hiyo maana tayari mko katika mapambano

Amri Said: Nimekaa na wenzangu na kuzungumzia hali hiyo. Tunajipanga kikamilifu kukabiliana na hali hiyo ili tufanye vizuri.

www.shaffihdauda.co.tz: Nimetazama ligi hadi sasa. Timu nyingi zimekuwa na changamoto ya ufungaji hata timu yako pia. Unachukuliaje hali hiyo?

Amri Said: Nafikiri hilo ni tatizo kubwa hata upande wetu, bado timu yetu haina mtu maalum wa kufunga magoli. Tegemeo letu kubwa ilikuwa ni yule kijana Madebe lakini bahati mbaya bado hajaruhisiwa kutoka ofisini na waajiri wake.

www.shaffihdauda.co.tz: Machaku alifunga goli 13 katika game 14 kwanini? Inakuwaje anakosa nafasi sasa?

Amri Said: Machaku si mchezaji mbaya kiufungaji ila tumemuongezea majukumu, sasa hivi tumekuwa tukimtumia kama kiungo mshambuliaji.

www.shaffihdauda.co.tz: Anayaweza majukumu hayo? Kama anaweza kufunga na timu haifungi kwanini usimrudishe nafasi ya kati?

Amri Said: Tunafanya hivyo ili timu isifungwe magoli mara nyingi na ukitazama hadi sasa tumefanikiwa kwa maana licha ya kuwa tunafanya maandalizi tukiwa katika ligi ila hatujaruhusu magoli mengi.

www.shaffihdauda.co.tz: Game ijayo mnacheza na nani? Wapi

Amri Said: Mechi inayofuata tunacheza na Mbao FC katika uwanja wetu wa nyumbani.

www.shaffihdauda.co.tz: Kweli ligi inaanza kuwa ngumu zaidi. Mbao FC wametoka kucheza mechi 6 mfululizo pasipo ushindi kati ya hizo nne mfululizo wametoa sare nyumbani, unadhani itakuwa mechi ya aina gani upande wenu?

Amri Said: Ni kweli ligi ngumu na tunakwenda kucheza mchezo mwingine mgumu wikend ijayo. Kwetu sisi kila mchezo ni mgumu hivyo tumejiandaa kukabiliana na hali hiyo kadri itakavyowezekana.

Tunafahamu Mbao ni timu nzuri, lakini tunajipanga kuhakikisha tunachukua pointi zote tatu katika uwanja wa nyumbani.

www.shaffihdauda.co.tz: Uwanja wa nyumbani ni nyenzo muhimu katika ligi. Unadhani timu yako inapata sapoti ya kutosha katika uwanja wa Samora?

Amri Said: Hakika, tena napenda kuwashukuru watu wa hapa (Iringa). Kumalizika kwa tatizo lililokuwa nje ya uwanja baada ya uongozi wa juu wa Mkoa, wilaya na Wazee wa Iringa, sasa Lipuli FC ni timu moja na hata kiwango cha juu cha mashabiki waliofurika katika mchezo wetu wa Jumamosi walikuja pale kuisapoti timu yao. Kwa kweli nawapongeza sana wakuu wa wilaya zote na mkuu wa Mkoa, wazee wa Iringa na mashabiki kiujumla.

www.shaffihdauda.co.tz: Baada ya game 7 za mwanzo msimu huu, unazungumziaje uchezeshaji wa waamuzi hasa kwa game mlizocheza ugenini?

Amri Said: Siwezi kuwalaumu waamuzi kwa sababu wengine huchezesha mechi pasipo kuwa na uzoefu hivyo matokeo yanapokuwa sare katika mchezo mwamuzi wa aina hii hujiona amechezesha vizuri. Wengine hujisifia kuwa wamemudu pambano lakini wakati mwingine ukweli mpira huchezwa katikati ya uwanja zaidi na kupelekea kukosekana kwa mashambulizi mengi golini.

Ukitazama hata katika michezo mingi iliyomalizika kwa sare utaona mpira ulichezwa zaidi katikati ya uwanja. Mechi isipokuwa na mashambulizi mengi si rahisi kupima uwezo halisi wa mwamuzi.

www.shaffihdauda.co.tz: Kuna chochote hupendezwi nacho katika ligi?

Amri Said: Mabadiliko ya waamuzi pasipo taarifa na mwamuzi mmoja kurudia rudia kuchezesha timu moja zaidi ya mara mbili wakati ligi ipo mzunguko wa saba tu. Kingine ni mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba.

www.shaffihdauda.co.tz: Mmeshakutana na mabadiliko ya ghafla ya waamuzi? Ilikuwa wapi?

Amri Said: Ndiyo, kama kocha niliona hili wakati timu yangu ilipocheza na Majimaji jana (Jumamosi iliyopita) lakini sijalalamika.

www.shaffihdauda.co.tz: Umevutiwa na lolote hadi sasa katika ligi?

Amri Said: Ndiyo, kuna mambo yamenivutia hasa kuona baadhi ya viwanja vikiboreshwa kwa kiwango kizuri katika eneo la kuchezea. Pitch ni sehemu muhimu sana kwa wachezaji, kwani ikiwa nzuri humfanya mchezaji kuwa tayari kucheza na kupokea maagizo ya walimu wake.

www.shaffihdauda.co.tz: Timu yako imeonekana kucheza vizuri katika kujilinda. Kuwa beki wakati wa uchezaji wako ndio kunapelekea hali hiyo?

Amri Said: Kwa kiasi fulani inanisaidia kwa sababu mara nyingi nimefanya mazoezi jinsi ya kulinda wakati nikiwa mchezaji. Tunalinda kama kilivyokaa kisu-mbele mtu mmoja, golikipa na wachezaji wengine wanajaa katikati ya uwanja.

www.shaffihdauda.co.tz: Neno lako kwa bodi ya ligi

Amri Said: Wajipange kwa ajili ya kuongeza wadhamini, na waweke mikataba na wanasheria watakaosimamia haki za wachezaji wanaocheza ligi na haki zao. Ni aibu kuona mchezaji wa ligi kuu ya Tanzania bara akicheza na kumaliza ligi nzima pasipo kulipwa mshahara huku timu ikisafiri bila posho.

www.shaffihdauda.co.tz: Asante sana mwalimu na nakutakia kila la heri katika kazi yako.

Amri Said: Asante sana, karibu tena wakati mweingine.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here