Home Kitaifa Mabao 75 ya mwanzo VPL balaa

Mabao 75 ya mwanzo VPL balaa

2232
0
SHARE

Na Arone Mpanduka (Tumaini Media)

IDADI ya mabao ya raundi tano za mwanzo za Ligi Kuu Tanzania Bara imepiku Ligi za misimu miwili iliyopita hadi kufikia sasa.

Kwa sasa Ligi Kuu imesimama kwa muda kupisha majukumu ya timu ya taifa, Taifa Stars katika kalenda inayotambuliwa na Shirikisho la soka duniani FIFA na baada ya hapo itaendelea tena kuanzia Oktoba 13 mwaka huu.

Ligi hiyo imesimama huku mechi zikiwa zimechezwa katika raundi tano tangu msimu mpya wa 2017/18 ulipoanza rasmi Agosti 26 mwaka huu.

Katika raundi hizo, jumla ya mabao 75 yamefungwa na kupiku idadi ya mabao ya msimu wa 2016/17 na 2015/16 yaliyofungwa ndani ya raundi tano za mwanzo.
Katika msimu uliopita wa 2016/17 jumla ya mabao 70 yalifungwa katika raundi tano za mwanzo wakati msimu wa 2015/16 jumla ya mabao 65 yalifungwa katika raundi hizo hizo.

Kwa msimu wa sasa, raundi ya kwanza ndiyo inaongoza kwa kuwa na mabao mengi ya kufungwa kuliko zingine nne(mabao 18) huku raundi ya pili ikiwa na mabao 13, ya tatu mabao 11, ya nne mabao 17 na ya tano mabao 16.
Kitakwimu, raundi ya kwanza ya msimu uliopita inaonekana kuwa ngumu zaidi ikilinganishwa na ya msimu wa sasa, kwani raundi hiyo ilivuna jumla ya mabao 9 pekee.

Mabao hayo 9 yalipatikana kupitia mechi 7 kati ya 9 zilizochezwa wakati huo ambapo Simba iliifunga Ndanda 3-1, Ruvu Shooting iliifunga Mtibwa 1-0, Tanzania Prisons iliifunga Majimaji 1-0 wakati Toto Africans iliilaza Mwadui 1-0 na Azam FC ilitoka sare ya 1-1 na African Lyon.

Raundi za pili za Ligi ya msimu huu na uliopita zinafanana katika uvunaji wa mabao ambapo zote zilivuna mabao 13.

Timu iliyovuna pointi nyingi ugenini 

Maafande wa Jeshi la Magereza, Tanzania Prisons wanaongoza kwa kuvuna pointi nyingi ugenini kuliko timu zingine katika raundi tano za mwanzo za msimu huu.
Prisons wamepata jumla ya pointi 7 ugenini kwa kuifunga 2-1 Njombe mji kwenye uwanja wa Sabasaba mjini Njombe na kisha kuifunga 3-1 Mwadui FC kwenye uwanja wa Mwadui Complex Shinyanga huku ikiambulia sare ya 1-1 na Mbao FC kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza. Kwa ujumla Prisons imeshinda mechi mbili ugenini na sare moja ugenini.

Timu iliyovuna pointi nyingi nyumbani

‘Wakata Miwa’ Mtibwa Sugar imetumia vema uwanja wake wa nyumbani hadi sasa baada ya kuzoa jumla ya pointi 9 na kumfanya aongoze Ligi kwa muda kabla ya Simba SC kumpiga kumbo kileleni.

Mtibwa iliifunga Stand United bao 1-0, Mwadui 1-0 na kisha ikaifunga Mbao FC mabao 2-1.

Kipa Azam awapiku wa Yanga na Simba 

Golikipa wa timu ya soka ya Azam FC Mghana Razak Abalora ameruhusu bao moja tu tangu Ligi ianze ikilinganishwa na Aishi Manula wa Simba na Rostand wa Yanga.
Razak ameruhusu bao moja pekee wakati Azam ikicheza na Singida United kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Golikipa wa Simba Aishi Manula ameruhusu mabao matatu hadi sasa huku Rostand akiwa ameruhusu mabao mawili pekee.

Manula aliruhusu mabao mawili kwenye mchezo dhidi ya Mbao FC ambao ulimalizika kwa sare ya 2-2 kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Pia aliruhusu bao moja katika mchezo dhidi ya Stand United kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga ambapo Simba ilishinda 2-1.

Rostand wa Yanga aliruhusu bao kwenye mchezo dhidi ya Lipuli FC ambao timu zilitoka sare ya 1-1 na kisha kuruhusu bao lingine kwenye mchezo dhidi ya Majimaji FC ambao timu zote zilitoka sare ya 1-1.

Timu ambayo haijapata bao ugenini 

Ni Kagera Sugar ya Mkoani Kagera ambayo imecheza mechi tatu ugenini na kufungwa 1-0 dhidi ya Azam kisha kufungwa 1-0 na Singida United kabla ya kutoka suluhu ya bila kufungana na Majimaji FC.

Ama kwa hakika, Kagera ambayo msimu uliopita ilimaliza Ligi ikiwa katika nafasi ya tatu, hivi sasa imeanza Ligi kwa kusuasua.

Timu za Singida United na Mbao FC

Singida United na Mbao FC kila moja imefunga jumla ya mabao 6 hadi sasa, idadi ambayo ni sawa na mabao ya mshambuliaji wa Simba SC Emmanuel Okwi ambaye hadi sasa anaongoza kwa ufungaji akiwa na idadi ya mabao 6.

Kichuya na Oktoba mosi

Oktoba mosi imekuwa na bahati kwa winga wa Simba SC Shiza Kichuya katika kipindi hiki cha miaka miwili.

Oktoba mosi mwaka huu kwenye mechi dhidi ya Stand United, Kichuya aliifungia timu yake bao la kwanza, mchezo ambao Simba iliibuka na ushindi wa 2-1. Lakini ikumbukwe Oktoba mosi mwaka jana, Kichuya alifunga bao dhidi ya Yanga, mchezo wa Ligi Kuu ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Kichuya alifunga bao kwa ustadi kupitia mpira wa kona ulioingia wenyewe wavuni bila kuunganishwa na mtu.

0786 160643

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here