Home Kitaifa Mkongwe aliyeanza kucheza ligi kuu Tanzania bara kabla golikipa wa Yanga hajazaliwa,...

Mkongwe aliyeanza kucheza ligi kuu Tanzania bara kabla golikipa wa Yanga hajazaliwa, leo wanacheza pamoja

10583
0
SHARE

Ni Star asiyetajwa kwenye vyombo vya habari, inawezekana kutokana na maisha anayoishi nje ya uwanja lakini pia hatajwi sana hata kwa kile anachokifanya akiwa kazini. Ukijua historia yake japo kidogo tu huenda ukastushwa na kutamani kumfuatilia, huyu ni kiungo wa Kagera Sugar George Kavila.

Jamaa ameanza kucheza ligi kuu Tanzania bara wakati golikipa wa Yanga Ramadhani Kabwili bado hajazaliwa (achana na mwaka ambao Kavila alianza kucheza soka), kwa mujibu wa takwimu, Kabwili anatimiza miaka 18 mwaka huu (amezaliwa mwaka 1999) wakati huo tayari Kavila akiwa na mwaka mmoja tangu aanze kucheza ligi kuu.

Kabwili ni mfano tu lakini wapo wachezaji wengi ambao wanacheza ligi kuu wakiwa umri sawa na Kabwili hususan vijana wa Serengeti Boys kama Shaaban Ada wa Lipuli, Dickson Job wa Mtibwa na wengine ambao sasa hivi wanacheza na Kavila lakini yeye wakati anaanza kucheza ligi kuu wao walikuwa bado hawajazaliwa.

Mkongwe wa ligi kuu Tanzania bara na nahodha wa Kagera Sugar ameanza kucheza ligi mwaka 1998 akiitumikia Coastal Union ya Tanga ambayo ndio timu yake ya kwanza kumtambulisha kwenye soka kwa ngazi ya juu nchini.

Vilabu alivyocheza

Amecheza vilabu vitano tofauti vya ligi kuu hadi sasa (Coastal Union ya Tanga, Twiga ya Dar, Polisi Moro ya Morogoro, Villa Squad ya Dar na Kagera Sugar ya mkoani Kagera ambako amedumu hadi leo).

Kavila alijiunga na Kagera Sugar mwaka 2009 (miaka nane iliyopita) na ameweza kudumu kudumu kwenye kikosi cha kwanza kwenye timu hiyo chini ya makocha tofauti ambao wamewahi kumfundisha. Mayanja, Mayanga, Kibadeni, Mbwana Makata, Mecky Maxime ni makocha ambao wamemuamini Kavila na kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Kagera Sugar.

Taifa Stars

Katika miaka yake yote aliyocheza soka nchini, hajabahatika kuitwa kwenye timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, aliwahi kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 chini ya makocha marehemu Matokeo na Ernest Mokake lakini hakuwa sehemu ya kikosi kilichosafiri kwenda Burundi.

Siri ya kudumu kwenye soka kwa muda mrefu

Ni mwaka wa 19 sasa anaendelea kucheza ligi kuu achana na madaraja ya chini ambako alianza kucheza soka la ushindani, si kitu cha kuchukulia poa kabisa. Mtu yeyote lazima angeshawishika kumuuliza Kavila amewezaje kumudu kucheza kwa muda wote huo bila kushuka kiwango.

“Katika maisha lazima ujue kitu gani kinatakiwa katika kazi yako, ukishajua huwezi kupata tabu. Miiko ya mpira inajulikana lakini kikubwa ni kupumzika tu”, ndio lilikuwa jibu la George Kavila kuhusu kudumu kwenye soka la ushindani kwa muda mrefu.

Dar ni changamoto kwa wachezaji

Kavila anasema hakuna sehemu ngumu kucheza soka kama Dar kutokana na changamoto za vishawishi vya starehe: “Ujue Dar ni pagumu kucheza mpira kama utaingiza mpira na mambo mengine.”

Mastaa wa zamani aliowahi kucheza nao timu moja

Lunyamila, Mmachinga, Malima ni baadhi ya ma-star waliotamba Simba na Yanga ambao alicheza nao Twiga timu ambayo ilikuwa inasimamiwa na Idd Azzan.

Ameshafikiria kustaafu?

Ameshawahi kufikiria kustaafu soka lakini waajiri wake (Kagera Sugar) kwa kuwa bado wanamuunga mkono kwa kumpa nafasi ya kuendelea kucheza, anapata nguvu ya kuendelea kukomaa na kupambana na vijana.

“Huwa nafikiria kustaafu, lakini waajiri wangu bado wananipa nafasi ya kucheza. Nawaheshimu, wananiheshimu na wanaheshimu na kuthamini kile ambacho nakifanya katika timu, hiyo inanipa nguvu ya kufanya vizuri kila msimu.”

Wachezaji wanaomvutia

Kwa upande wa Bongo, Kavila anamkubali sana Mbaraka Yusuph mshambuliaji wa Azam ambaye msimu uliopita walicheza pamoja katika kikosi cha Kagera Sugar na kufanikiwa kumaliza katika nafasi ya tatu  kwenye msimamo wa ligi huku kijana huyo (Mbaraka Yusuph) akishinda tuzo ya mchezaji chipukizi kwa msimu huo.

Viungo wa Barcelona Andres Iniesta na Sergio Buqsuet ndio wanaomvutia kwa upande wa wachezaji wa kimataifa.

Kavila humwambii kitu kuhusu Man United

“Mimi ni shabiki wa kutupwa wa Manchester United kaka, msimu huu hatuna presha tumeanza kwa kasi ya 4G.”

Kavila ni darasa tosha kwa vijana

Kuna wachezaji wengi wamekuja kwenye ligi wamemkuta Kavila na kupotea wakimuacha yeye anaendelea kupeta tu, ipo haja ya vijana kukaa na Kavila kuchukua ‘uchawi wake’ na kujivika mabeni mwao lakini kama watakuwa wanakutana nae na kuishia kumpiga ngumi uwanjani, rekodi anayoiweka wataishia kuisoma tu.

Nasubiri kwa hamu kuona George Kavila anatimiza miaka 20 tangu aanze kucheza ligi kuu, hii itakuwa ni msimu ujao 2018/2019, tuombe uzima kushuhudia shujaa huyu wa kikosi cha Kagera Sugar akiweka historia na rekodi ya aina yake kwenye ligi yetu.

Kwa namna yoyo ile ile tunapaswa kujivunia kuwa na Kavila kwenye ligi yetu, kinachosikitisha na kuumiza ni kwamba, soka letu na ligi yetu si watunzaji wa kumbukumbu, leo hii hatujui Kavila amecheza mechi ngapi za ligi kuu.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here