Home Kitaifa Jicho la 3: Baada ya mataji matatu mfululizo, manne katika misimu mitano...

Jicho la 3: Baada ya mataji matatu mfululizo, manne katika misimu mitano VPL, Yanga inaanguka tena?

11773
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

BAADA ya ‘anguko’ kubwa la kwanza kubwa ndani ya uwanja katika karne ya 21, mabingwa wa kihistoria wa Tanzania Bara, timu ya kandanda ya Yanga ilifanya ‘uamuzi bora’ zaidi katikati ya mwaka 2012. Chini ya mwenyekiti wakili, Chunga mabingwa hao mara 27 wa ligi kuu walipitia kipindi kigumu kiuchumi msimu wa 2011/12 kiasi cha kupelekea klabu hiyo kumaliza nafasi ya tatu katika ligi kuu.

Tangu kuanza kwa karne mpya (mwaka 2000) Yanga haikuwa imemaliza nje ya ‘Top 2’ Katika ligi kuu huku ikitwaa mataji sita kabla ya kuanguka nafasi ya tatu wakicheza ligi kama mabingwa watetezi. Wakati ule timu
ilipokuwa ikianguka chini ya Nchunga, niliandika makala kadhaa za kuwataka wanachama wa klabu hiyo kupiga kura ya kutokuwa na imani na utawala wa Nchunga ili kuinusuru timu yao.

Niliambiwa na wachezaji kadhaa waandamizi kuwa Nchunga hakuwa amewalipa mishahara kwa miezi zaidi ya mitatu huku akishindwa pia
kuwalipa posho isiyopungua Tsh. 70, 000 katika michezo 17 mfululizo.

Kuna mengi yalichangia kipigo cha ‘fedheha’ walichokipata Yanga Mei 7, 2012 kutoka kwa mahasimu wao Simba SC.

Yanga ilikuwa katika kipindi kigumu kiuchumi na kuelekea mchezo ule, Nchunga kama mwenyewekiti wa klabu alihakikisha wachezaji wanapata kiasi cha Tsh. 500, 000, halafu walikuwa wakienda kucheza na kikosi hatari cha Simba ambacho kiliwaumiza ‘waarabu’ wa Entente Setif, Al Ahly Shandy huku wakipiga zaidi ya pasi 27 mfululizo.

Simba iliyoipiga Yanga 5-0, Mei 2012 ilikuwa kali sana lakini ukata ulichangia kwa kiasi kikubwa kutengeneza historia mbaya kwa wachezaji bora kuwahi kutokea klabuni Yanga kama, Shadrack Nsajigwa, Athumani Idd
‘Chuji’, Nurdin Bakary, Yaw Berko na golikipa mwenzake Said Mohamed ‘Dunda’, Nadir Haroub na wengineo ambao waliingia kucheza mechi wakiwa hawana pesa, hamasa, huku klabuni tayari kukiwepo kwa mpasuko mkubwa
kati ya ‘Wazee wa klabu’ na mwenyekiti wao Nchunga.

Baada ya mataji matatu mfululizo, manne katika misimu mitano, Yanga inaanguka tena?

Kama funzo la anguko la klabu chini ya utawala wa Nchunga, Mei, 2012 halitatazamwa kwa ‘jicho la tatu’ na ‘watu hasa wa Yanga yenyewe’ klabu inaenda kuanguka. Na bahati mbaya wanaenda kuangushwa na mtu ambaye alikerwa na utawala wa Nchunga huku yeye akiwa makamu mwenyekiti wakati huo, Clement Sanga ambaye sasa anakaimu nafasi ya mwenyekiti aliyejiuzulu Yusuph Manji.

Wakati ule Nchunga alipoficha madhaifu makubwa ya klabu kwa rekodi nzuri ya timu vs Simba, niliandika makala ambayo iliniletea vitisho kadhaa kwa kuandika kwangu namna maisha ya ndani ya wachezaji yalivyo klabuni hapo na nilisema pia kama sababu ya yeye (Nchunga) kuendelea kuifunga Simba basi anaenda kuitia ‘aibu’ kubwa klabu yake mbele ya Simba.

Hadi sasa naamini ‘mashabiki wachache damu’ wa klabu waliobaki uwanjani baadaya marehemu, Patrick Mafisango kufunga goli la tano kwa mkwaju wa penati huku zikiwa zimesailia dakika zaidi ya kumi kabla ya kumalizika kwa mchezo ndiyo walioinusuru ‘aibu kubwa’ zaidi kwa klabu yao.

Hadi wanafungwa goli la tano, ndani ya uwanja lugha za wachezaji wa Yanga zilikuwa zikitoa ishara ya kuhitaji  magoli zaidi katika lango lao.

Waliamini wapo sambamba na kundi kubwa la wanachama na mashabiki wa klabu wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa klabu, Mzee Akilimali (ambaye aliwaongoza wazee wenzake kuvua kofia mbele ya wanahabari kama ishara ya kuonyesha hawako pamoja na timu yao kuelekea mchezo huo vs Simba).

Kwa nini nasema, mashabiki hasa wa Yanga waliokoa jahazi siku ile? Nakumbuka wale waliokuwa majukwaa ya juu walishuka haraka baada ya timu yao kuruhusu goli la tano na kusogea katika jukwaa la chini kabisa. Hawakuwa wengi sana sababu wenzao wengi waliamua kuondoka uwanjani. Uchache wao na sauti zao za uchungu ziliwafikia wachezaji.

Kikubwa waliwaomba wachezaji wao kuhakikisha kwa namna yoyote wanacheza kwa kujituma kuhakikisha Simba hawafungi goli la 6 na kufikia rekodi ya mwaka 1977, ama kupata goli nyingine mbili kutengeneza rekodi mpya ya Dar es Salaam-Pacha.

Licha ya kuzungumza kwa kuomba, wakasisitiza kwa kupaza sauti kwa wachezaji wao wakiwaambia, ‘Simba wakipata goli la Sita hamtatoka salama humu uwanjani’ huku wakisisitiza kwa kuwaambia wachezaji kuwa wasitegemee ulinzi wa askari kwani ni wachache sana kwao.’

Baada ya mkwara huo, wachezaji walicheza kwa nguvu kubwa na ungeamini walikuwa wakicheza kwa kuhitaji goli moja tu ili wawe mabingwa.

Sasa ni timu Yanga

Sanga alikuwa msaidizi wa Nchunga  ambaye aliingia madarakani Juni, 2010 akichukua nafasi ya Imani Madega. Nakumbuka baada ya mchezo ule huku Nchunga akisisitiza kutoachia madaraka. Sikuwa upande hivyo kwa maana sikutaka kuona Yanga ikiangukia mbali zaidi ikiwa kuna watu wanaweza kuisaidia kunyanyuka na kuwasaidia vijana wa kitanzania kutengeneza maisha yao.

Hivyo niliendelea kuwachochea wanachama kutumia njia hata ya maandamano hadi Nchunga atakaposalimu amri na kuachia madaraka. Baadae akakubali kushindwa hasa baada ya kina Sanga na wajumbe wa kamati ya
utendaji kuamua kujiuzulu.

Mara baada ya Manji kutangaza kujiuzulu katika nafasi hiyo mapema mwaka huu, niliandika kuwa Yanga inapaswa kuingia katika uchaguzu mdogo wa kuziba nafasi yake kabla ya kufikia Julai mwaka huu.

Inawezekana Manji alitoa sababu  za kiafya kuwa zimechangia kujiuzulu katika nafasi ambayo ameitumia kwa miaka isiyopungua mitano –Julai 2012 hadi Mei, 2017.

Manji aliondoka wakati mwafaka, lakini tamaa ya madaraka tatizo 

Hakuna asiyefahamu ni watu wangapi ambao wametengeneza maisha yao na historia nzuri ya klabu katika utawala Manji. Tangu wakati anachukua fomu ya kuogombe nafasi ya uenyekiti Juni, 2012 nilikuwa upande wa Manji na niliamini wazi Yanga inaweza kufanikiwa katika baadhi ya sehemu ikiwa chini ya Manji.

Na kuondoka kwake kulikuja wakati mwafaka, licha ya kusumbuliwa na mambo binafsi tangu mwanzoni mwa mwaka huu, Manji alisubiri hadi pale msimu ulipomalizika ndiyo akatangaza kukaa kando na wale wafuatiliaji
wa mambo wanafahamu kuanza Mei hadi sasa Manji amepitia vipindi gani na je, angekuwa na uwezo wa kuendelea kuisimamisha Yanga kama vile ilivyokuwa?

Kujiuzulu kwake mapema ilikuwa ni funzo zuri ambalo alilipata kutoka kwa Nchunga ambaye alimuachia nafasi licha ya kuwa ni baada ya
kupigiwa sana kelele ila ilikuwa ni wakati ambao timu inapaswa kufanya usajili.

Manji alitaka Yanga isajili kwa namna watakavyoweza kuwahudumia wachezaji hao, lakini kwa jicho langu la tatu naona Sanga na utawala wake wanaamini Manji atarudi katika nafasi yake ama ataendelea kutoa msaada pale atakapoombwa. Kumbe sivyo, hata kiubinadamu lugha ya mwili  ya Manji inahitaji kupumzika baada ya misukosuko mingi ndiyo maana alitaka alijiuzulu wakati ambao aliamini klabu inaweza kujaza nafasi yake.

Hakuna kimfurahishacho mtu kama cheo, hasa pale mtu anapokuwa katika cheo cha juu zaidi katika taasisi, ila cheo ni dhamana tu. Dhamana ambayo unaweza kuitumikia kwa uaminifu, huku ukileta  matokeo ‘chanya’ kwa taasisi na katika maisha yako binafsi.

Sanga tayari anaonekana ni mtu anayependa cheo kikubwa, hivyo ni wachezaji wake kufuata taratibu ili kukipata cheo hicho. Na cheo anachotaka yeye pale Yanga ni cha kuchaguliwa, aipeleke klabu katika uchaguzi haraka ili kuleta matokeo chanya klabuni na si kwa mtu binafsi pekee. Awe mwadilifu kama ilivyokuwa kwa Manji.

Sanga hakuchaguliwa kuwa mwenyekiti Yanga, ni yeye atakaeiangusha klabu

Kitendo cha makamu mwenyekiti wa klabu, Sanga ambaye anakaimu nafasi ya uenyekiti iliyoachwa na Manji kuendelea kuamini Manji atarudi au kuendelea kutoa pesa  nyingi klabuni ni sawa na kuiangushia mbali klabu hiyo wakati kuna watu ambao wanaweza kuinyanyua zaidi ikiwa klabu itakwenda katika uchaguzi mdogo. Ameshachelewa, lakini wanaweza kuwahi Novemba au Desemba  ijayo kwa uitisha mkutano wa dharura wa klabu kwa lengo la kumchagua mwenyekiti mpya.

Sanga ni kiongozi mzuri  ila hakuchaguliwa na wanachama kuwa mwenyekiti wa klabu na naamini kama angegombea nafasi hiyo wanachama wasingempigia kura nyingi za ushindi kama zile alizopata katika chaguzi 3 zilizopita alizosimama kama mgombea wa nafasi ya umakamu mwenyekiti. Ni lazima akubali klabu iende katika uchaguzi wa dharura ili kujaza nafasi iliyoachwa na Manji kabla ya Januari, 2018.

Kuna baadhi ya wanachama wa klabu wanaamini udhamini kutoka SportPesa unatosheleza kuendesha klabu kwa msimu mzima huku ukiwalipa wachezaji posho, bonasi, mishahara, benchi la ufundi na wafanyakazi wengine klabuni.

Niliposema Yanga inapaswa kufanya uchaguzi mdogo Juni iliyopita wapo ambao walinibeza, lakini naamini   ni wale waliokuwa na fikra kuwa Manji atarudi na wengine walioamini katika SportPesa pekee. Natazama zaidi ya hilo kwa kuamini ukiitishwa uchaguzi watajitokeza watu wenye kaliba ya Manji ama zaidi na hapo ndipo wanachama watakapoamua. Hivi sasa wachezaji wa Yanga wanadai malimbikizo  ya mishahara.

Ndiyo kuna wakati tunamlaumu kocha kutokana na kiwango kibovu cha timu lakini huku katika utawala pia mambo ni hovyo na msiendelee kuamini katika udhamini  mmoja na kukataa makampuni yanayokuja hata kwa milioni 100 kwa mwaka.

Matokeo yao katika michezo mitano ya mwanzo msimu huu yanachanganya sana watu wa Yanga, lakini naamini huu ni mwanzo tu wala si mwisho mbaya ikiwa Sanga na timu yake ya utawala itakubali kuishi bila fikra za Manji bila shaka kutokana na misukosuko aliyopitia kwa miezi nane iliyopita atakuwa ameshaanza kusahau kuhusu mafanikio aliyowapa Yanga kati ya Julai 2012 hadi Mei 2017 akiwa mwenyekiti mshindi.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here