Home Kitaifa Uhondo wa VPL Jumamosi hii

Uhondo wa VPL Jumamosi hii

3271
0
SHARE

Ligi kuu Tanzania bara itaendelea tena Jumamosi ya September 30, 2017 kwa mechi za mzunguko wa tano. Itachezwa michezo sita halafu Jumapili utachezwa mchezo mmoja kukamilisha weekend hii.

Kuna mechi tatu ambazo ni gumzo siku ya Jumamosi, zitaangaliwa na mashabiki wengi ukilinganisha na mechi zingine zitakazochezwa siku hiyo.

Yanga vs Mtibwa Sugar, Singida United vs Azam FC, Mbao vs Tanzania Prisons ni mechi ambazo zitafuatiliwa kwa karibu na mashabiki wengi.

Yanga vs Mtibwa Sugar

Yanga watakuwa wenyeji kwenye uwanja wa Uhuru Dar, watahitaji ushindi wa aina yoyote ili kufikisha pointi 11 zitakazo waweka katika nafasi nzuri wakati wakisikilizia matokeo ya timu nyingine zinazowania uongozi wa ligi kama Tanzania Prisons, Simba, Singida United na Azam.

Hadi sasa Yanga na Mtibwa bado hazijapoteza mechi zikiwa tayari zimecheza michezo minne. Yanga imeshinda mechi mbili na kutoka sare mara mbili, mtibwa imeshinda mechi tatu mfululizo na kutoka sare katika mchezo mmoja.

Mtibwa imecheza mechi mmoja tu ugenini na kuambulia sare ya kufungana goli 1-1 na Ruvu Shooting, mechi zote ilizoshinda ilicheza uwanja wa nyumbani. Yanga imeshinda michezo miwili, mmoja uganini na mwingine nyumbani, sare mbili kati ya hizo moja ni nyumbani na nyingine ugeni.

Yanga imefunga magoli manne na kuruhusu magoli mawili wakati Mtibwa wao wamefunga magoli matano na kufungwa magoli mawili. Kwa hiyo ni mechi ambayo inazikutanisha timu ambazo zinaweza kufunga lakini pia zinaruhusu kufungwa.

Mbao vs Tanzania Prisons

Watu wanataka kuona Mbao itafanya nini baada ya kuisimamisha Simba kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza. Vijana wa Mbao wanaingia uwanjani kutafuta ushindi wao wa kwanza kwenye uwanja wa nyumbani msimu huu katika mechi ya pili kwenye uwanja huo.

Mbao itacheza mechi ya pili CCM Kirumba msimu huu baada ya kucheza na Simba mchezo uliopita na kulazimisha sare ya kufungana 2-2 ikiwa ni mechi yao ya kwanza nyumbani msimu huu.

Prisons ambayo ipo kwenye mwendo mzuri tangu kuanza kwa ligi ikiwa haijapoteza mchezo katika mechi zake nne zilizopita. Imeshinda mara mbili na kutoka sare mara mbili, ina pointi nane sawa na Yanga na Simba.

Mbao wenyewe wameshinda mechi moja, wametoka sare kwenye mchezo mmoja na kupoteza miwili. Wapo katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama nne.

Singida United vs Azam FC

Hawa ni mafahari wawili watakaokuwa wakipambania pointi tatu kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Hadi sasa Azam bado haijafungwa goli katika mechi nne walizocheza ikiwa ni timu pekee ambayo haijaruhusu wavu wake kuguswa na mpira ni rekodi ambayo Azam wanajivunia safu yao ya ulinzi.

Singida United wao wanajivunia rekodi yao ya kushinda nyumbani, wamecheza mechi mbili na kushinda zote (Singida 2-1 Mbao, Singida 1-0 Kagera Sugar)

Singida imeshida michezo mitatu kati ya minne waliyocheza, wamepoteza mechi moja, wana pointi tisa wakiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa VPL wanapambana na Azam ambayo haijapoteza mechi wala kuruhusu bao.

Azam ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 10 sawa na Mtibwa huku timu hizo zikitofautishwa kwa wastani wa magoli.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here