Home Kitaifa Tayari Azam imeonekana kuwa imara zaidi ya Yanga, Simba labda itokee

Tayari Azam imeonekana kuwa imara zaidi ya Yanga, Simba labda itokee

5668
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

KUCHEZA michezo 25 na kuruhusu magoli manne katika michuano ya ndani ya nchi kwa miezi karibia kumi sasa si jambo la ‘kubeza’. Michezo sita pasipo kuruhusu goli iliambatana na ubingwa wa Mapinduzi Cup, Januari mwaka huu, na kikosi hicho cha Azam FC kilicheza michezo 15 na kuruhusu magoli manne tu katika mzunguko wa pili msimu uliopita.

Kuondoka kwa wachezaji wanne wa kikosi cha kwanza katika ngome wakati wa usajili uliopita bado hakuonekani kuwayumbisha mabingwa hao mara moja wa Tanzania bara na wameanza msimu huu wakiwa imara zaidi baada ya kucheza michezo minne pasipo kuruhusu goli lolote hadi sasa.

Mara baada ya kuondolewa kwa Wahispaniola sita katika benchi la ufundi waliokuwa wakiongozwa na Zeben Hernandez, Azam FC imeonekana kucheza vizuri katika idara ya ulinzi chini ya Mromania, Aristica Cioaba ambaye anashirikiana na ‘wazalendo wa timu hiyo’ Idd Cheche na kocha wa magolikipa, Idd Abubakary.

Wametengeneza beki ya kimataifa

Tangu wakati wa maandalizi ya msimu Juni mwaka huu, Aristica amekuwa akitumia safu ileile ya ulinzi. Jambo ambalo limewafanya Aggrey Morris,  Mzimbabwe, Bruce Kangwa, waghana, Yakubu Mohamed na Daniel Amoah kucheza kwa maelewano makubwa na huwezi kuona mapengo yaliyoachwa na Shomari Kapombe aliyejiunga Simba SC, Gadiel Michael aliyejiunga Yanga, Erasto Nyoni na golikipa Aishi Manula ambao pia wamesajiliwa Simba msimu huu.

Golikipa, Mghana, Razak ameanza msimu huu kwa kuonyesha ‘mwanga’ kuwa huenda Azam FC ikawa mefanikiwa kupata kipa wa kwanza bora kutoka nje ya nchi. Mghana huyu U20 ameshacheza michezo minne pasipo kuruhusu goli huku kiwango chake katika michezo vs Simba na Lipuli FC kikiendelea kujenga ‘uaminifu’ kuwa kijana huyo anaweza kufanya zaidi ya kile ambacho kilikuwa kikifanywa na Manula katika misimu mitatu iliyopita.

Akiwa chini ya kocha Idd Abubakary ambaye amekuwa ‘mzalishaji’ wa makipa bora klabuni hapo tangu mwaka 2007, Razak anaweza kucheza vizuri mipira ya krosi, kona, pia amekuwa mtulivu na mchangamfu golini. Kitendo cha kuwa na golikpa mwenye kupaza sauti kwa walinzi wake na yeye mwenyewe akiwa ‘sharp’ ni sababu ya kwanza ya kutengeneza ukuta imara kwa timu.

Inawezekana bado hajakutana na washambuliaji wakali zaidi lakini kucheza dhidi ya Ndanda FC, Simba, Kagera Sugar FC, na Lipuli pasipo kurusu goli katika kikosi kinachojengwa upya ni dalili njema si tu kwa timu bali hata kwa mchezaji mwenyewe ambaye anaendelea kujiamini huku akizoea ligi ambayo hakuwahi kucheza.

Kabla ya kuanza kwa msimu huu niliitazama Azam FC kuanzia wakati wa maandalizi yake marefu, na niliandika humuhumu kuwa kikosi hicho kinaweza kupenya katikati ya vigogo Yanga na Simba na kushinda ubingwa msimu huu baada ya kuona namna kilivyobalansi-kiumri huku wachezaji yosso kama Yahya Zayd wakionesha uwezo mkubwa wa kuibeba timu hiyo.

Ukitazama katika ngome yao, Mzawa, Aggrey ndiye pekee anaonekana kuwa mkubwa kiumri.  Aggrey ambaye alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshinda taji la kwanza la VPL kwa klabu hiyo msimu wa 2013/14 kwa sasa ana umri wa miaka 33 huku akiwa klabuni hapo tangu mwaka 2009.

Mchezaji bora wa klabu mwezi Agosti, Yakubu yeye amezaliwa Juni 29, 1996, Kangwa amezaliwa mwaka 1988 huku Amoah akiwa kijana mdogo tu mwenye miaka 19. Hawa ni wachezaji wanne wa ulinzi na ukiongeza na golikipa Razak utaona ni kiasi gani Azam FC ilivyo na ‘damu changa’ katika ngome lakini tayari wameonyesha ukomavu.

Nidhamu

Wakati kizazi cha miaka ya 1980 kikichukuliwa kama cha mwisho chenye uwezo wa juu kimpira, vijana wa miaka ya kuanzia 1995 wamekuwa wakiamini kuwa soka linahitaji nidhamu, kujituma na kuwa tayari kufuata maelekezo ya makocha wao.

Azam FC huenda hawana kiungo mahiri kama Athuamani Idd ‘Chuji’ au Haruna Moshi ‘Boban’ ila nidhamu ya juu kutoka kwa nahodha Himid Mao Mkami, Frank Domayo, kiungo wa zamani wa Cotton Sporp ya  Camerron, Kingue imefanya timu hiyo kuwa na safu bora ya kiungo ambayo inaifanya timu icheze katika mwelekeo wa kitimu.

Azam FC wanashambulia kama timu na hata inapotokea mpira ukawa kwa timu pinzani bado hujihami katika mtindo wa kitimu. Hii inatokana na wachezaji wote katika timu kucheza huku wakiamini katika nidhamu ya kimchezo, nidhamu binafsi.

Kuwa na kipaji pekee katika soka la kisasa hakutoshi kumfanya mchezaji kuwa bora, kujituma na nidhamu ndiyo jambo linaloongoza kipaji cha muhusika na Azam FC wataendelea kubebwa na nidhamu yao ndani na nje ya mchezo. Walivumilia kila shambulizi la Lipuli FC na walicheza kwa tahadhari kubwa vs Simba wakati walipokutana na mashambulizi mengi katika michezo hiyo msimu huu.

Mbaraka Yusuph

Magoli yake mawili aliyofunga Mbaraka Yusuph yameipatia Azam FC alama sita. Hiki ndicho kinachotakiwa na watu wa Azam FC. Wanataka kuona washambuliaji wao vijana waliosajiliwa Wazir Junior, Salmin Hozza, Mbaraka Yusuph wakifunga magoli na kuisaidia timu kupata pointi 3.

Mbaraka aliingia uwanjani akitokea benchi katika mchezo walioshinda 1-0 ugenini dhidi ya Ndanda siku ya ufunguzi. Alichukua nafasi ya mfungaji wa goli pekee katika mchezo huo, Mghana, Yahaya Mohamed. Alianza katika mchezo dhidi ya Simba lakini mechi ilimalizika 0-0.

Kitendo cha kufunga mara mbili mfululizo  katika michezo Azam 1-0 Kagera, Azam 1-0 Lipuli ni dalili nyingine kuwa wakati safu ya ulinzi, na ile ya kiungo zikifanya kazi vizuri, kijana huyu anaweza kuwaongoza vyema wenzake katika ufungaji licha ya kwamba timu imefunga magoli matatu tu katika michezo minne. Ila faida yake ni kwamba magoli hayo matatu yamewapa alama kumi huku ulinzi ukiwa sababu ya mafanikio hayo hadi sasa.

Benchi la ufundi

Nadhani kwa sasa Azam FC ipo katika ‘umbo moja’, kiutawala hadi kimpira. Wote walikubali kuanza moja na njia pekee ya kufankiwa katika hilo ni kutengeneza uaminifu klabuni. Sizungumziii uaminifu wa kumsaliti mtu, bali ule wa kumtii mwenzako na kumkubali. Tayari Azam FC imeonekana kuwa imara zaidi ya Yanga, Simba labda itokee wakaharibu muunganiko wao.

Nikitazama ‘lugha’ ya miili ya makocha, Aristica, Cheche na Abubakary, wachezaji na utawala naona kabisa upendo wa dhati katika klabu hiyo. Wanapaswa kuendelea kuamini katika uaminifu wao, kujituma, na kuwa tayari kupitia vipindi vigumu wakiwa pamoja kwa maana wapo katika ligi na kuna wakati mambo huenda ‘mrama.’

Nidhamu kubwa iliyopo katika benchi la ufundi ni ishara nyingine njema kwa Azam FC ambayo imeanza msimu huu wakidhaniwa hawatafanya lolote baada ya kuwapoteza kina John Bocco, Hamis Mcha Hamis, Mudathir Yahya, Aishi, Kapombe, Erasto, Gadiel huku wakifanya usajili ulioitwa wa ‘bei chee’ sasa bei chee zinaunganishwa na Aristica, Chechen na Abubakary na huenda zikapanda thamani.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here