Home Kitaifa Ndondo Cup Mwanza imeongeza soko la ‘Power Bank’

Ndondo Cup Mwanza imeongeza soko la ‘Power Bank’

2413
0
SHARE

Kauli ya mkuu wa mkoa wa Mwanza Mh. John Mongela pamoja na Kaimu meya wa jiji Biko Kotecha imetimia kuhusu fursa zinazoletwa na Ndondo Cup kwenye mkoa wao. Katika mchezo wa ufunguzi kulikuwa na wafanya biashara ndogondogo wengi, ShaffihDauda.co.tz ililiona hilo lakini tukadhani labda ni kwa sababu ya ufunguzi ndio maana kulikuwa na wajasiriamali wengi.

Kwenye mchezo kati ya Iseni vs Copco walikuwepo tena wajasiriamali wengi hapo ndipo ShaffihDauda.co.tz ikaamua kuzungumza na mwanamama mmoja ambaye alikuwa akiuza mihogo mibichi.

Mihogo mibichi ilijizolea umaarufu mkubwa kwenye michuano ya Ndondo Cup Dar hadi kufikia kupewa jina na Power Bank. Sasa Power Bank zinapatikana pia kwenye Ndondo Cup Mwanza na sio Dar pekee.

“Siku ya kwanza (siku ya ufunguzi) nilikuja na beseni moja nikauza na kumaliza mihogo yote, nilikutana na wenzangu wengine wawili na wao walikuwa na mabeseni yamejaa lakini wote tuliondoka tumemaliza mihogo yote,” anasema Mama Vero mkazi wa Igogo ambaye alikuwa anauza mihogo uwanja wa Nyamagana.

“Mihogo hii naitoa Buhongwa au Custom, kabla ya mashindano haya nilikuwa nalazimika kuzunguka maeneo mbalimbali ya mjini kutafuta wateja lakini kwa sasa nachukua beseni langu moja kwa moja nakuja uwanjani nauza namaliza narudi nyumbani. Kwa hiyo siku mbili hizi sijazunguka mjini zaidi ya kuja uwanjani.”

Wateja wengi wa mihogo mibichi ni wanaume japo wanawake pia wapo wanaokula, wanaume wanaamini mihogo inaongeza nguvu za kiume lakini mimi sijui kama kunaukweli au ni imani yao tu,” alijibu mama Vero nilipomuuliza kuhusu aina ya wateja wake wengi.

Siku ambayo timu ziligawiwa vifaa kwa ajili ya michuano ya Ndondo Cup, kaimu Meya wa jiji la Mwanza alisema michuano hiyo itakuwa fursa kwa wajasiriamali lakini pia mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela alirudia kusema mbali na maendeleo ya soka yatakayoletwa na Ndondo, lakini pia itakuwa ni fursa kwa wafanyabiashara ndogondogo.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here