Home Kitaifa Lwandamina amepiga pasi ya mwisho kwa Mahadhi, tuone pasi ‘rula’ na magoli...

Lwandamina amepiga pasi ya mwisho kwa Mahadhi, tuone pasi ‘rula’ na magoli ya ‘video’ Yanga

14320
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

KOCHA, George Lwandamina tayari ameonekana kuwaamini wachezaji kadhaa wapya, lakini imani yake ya muda mrefu kwa kiungo Juma Mahadhi inaweza kumletea matokeo mabaya kama mchezaji mwenyewe atashindwa kujiuliza kipi anachotafuta kocha wake katika mchezo wake.

Mahadhi alitarajiwa kuwa mchezaji  mwenye kipaji cha ‘ukweli’ nchini akitandaza pasi zake za kwenda mbele akitokea kati mwa uwanja. Msimu wa 2015/16 aliweza kusimama katika kiungo cha kati akiwa na timu ya Coastal Union ya Tanga na licha ya klabu yake kuonesha soka bovu hadi kufikia kuteremka daraja, lakini kiwango cha Mahadhi kilitambulika nchini kote.

Kocha mwenye ‘macho makali’ Hans van der Pluijm alifanikiwa kumsaini mchezaji huyo katikati ya mwaka 2016, na michezo yake ya kwanza akiichezea Yanga katika michuano ya Shirikisho Afrika kilimfanya wengi waamini kuwa kiungo huyo wa kati angekua haraka kimchezo akicheza katika kikosi chenye wachezaji ‘wenye njaa ya mafanikio.’

Miezi 15 sasa akiwa mchezaji wa Yanga, Mahadhi ameshindwa kufikia walau nusu ya kiwango kile alichokionesha akiwa Coastal. Chini ya Mholland, Hans alipewa nafasi mara kadhaa huku kiwango chake kibovu katika mchezo wa Caf Champions League,Machi mwaka huu dhidi ya Zanaco kutoka Zambia kilionesha ni kiasi gani kiungo huyo ameporomoka kiuchezaji.

Amepoteza kujiamini

Mahadhi amekuwa akipoteza mipira mingi katikati ya uwanja, amekuwa akipiga pasi nyingi mkaa na wakati mwingine kupeleka mpira kwa mchezaji wa timu pinzani. Kupaisha penalty muhimu katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC kumeendelea kumpotezea hali ya kujiamini mchezaji huyo japo kocha wake ameendelea kuvuta subira kwa kuamini  Mahadhi ana vitu ambavyo vinaweza kuipaisha sana Yanga.

Anapojiamini, Mahadhi anapelekea pasi ndefu au fupi pale anapotaka, huchezesha trimu huku akiwahamasisha wenzake, na hujenga utulivu pale anapopiga mikwaju yake ya mbali kuelekea golini mwa timu pinzani. Kuwa na kiungo mwenye uwezo wa kumiliki mpira, kukokota kwa kasi,mchangamfu na mwenye kupendelea kupiga pasi za kushambulia haraka ndicho anachokisaka Mzambia, Lwandamina kutoka kwa Mahadhi.

Ni ‘pasi’ ya mwisho Mahadhi amepigiwa, kabla ya ujio wa Buswita

Katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Lipuli FC, Lwandamina hakumteua Mahadhi hata katika wachezaji wa akiba. Nadhani alifanya hivyo baada ya Mahadhi kupoteza mkwaju wake wa penalty vs Simba siku tatu nyuma. Inawezekana tayari Lwandamina anatambua mchezaji wake amekosa kujiamini hivi sasa huku kitendo cha Mahadhi kuzungumza sana katika vyombo vya habari kuhusu mustakabali wake wakati wa usajili uliopita ukiondoa utayari wa kiungo huyo.

Lwandamina ameshapata safu ya mabeki wake wa kuanza mchezo ambayo inaundwa na golikipa Mcameroon, Youthe Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Kelvin Yondan na Andrew Vicent. Hapa amewaingiza wachezaji wawili wapya ambao wanachukua nafasi ya Deo Dida (Rostand) na Mwinyi Hajji (Gadiel)

Lakini katika kiungo Lwandamina bado anashindwa kumpata mchezaji mmoja wa kuchukua nafasi iliyoachwa na Haruna Niyonzima ndiyo  maana katika michezo mitatu ya kimashindano msimu huu Rafael Daud aliyesajiliwa kutoka Mbeya City FC ameanza mara mbili na Mahadhi mara moja huku wakipokeza kutoka au kuanza mchezo katika michezo dhidi ya Simba,Lipuli na Njombe Mji FC.

Mahadi alianza katika kikosi kilichoshinda 1-0 ugenini dhidi ya Njombe Mji na alicheza kwa dakika zote 90’ katika uwanja wa Sabasaba ambako hakuna presha kubwa ya mashabiki wa timu yake. Kuanzishwa kwake na kumaliza dakika tisini kulionesha kumfurahisha Mahadhi na hilo ndilo analotaka Lwandamina kwa kutambua atapa kile ambacho timu inahitaji kutoka kwa Mahadhi.

Papy Kabamba Tshishimbi ameingia haraka na kujikita katika kikosi cha kwanza cha Yanga. Kujiamini kwake ndiyo kumembeba na Mahadhi anapaswa kujiamini tu ili watu waone uwezo wake ambao ulimfanya Yanga ikamsaini kutoka Coastal msimu uliopita.

Mzimbabwe, Thaban Kamusoko pia amekuwa na namba ya kudumu na kitendo cha Mahadhi kupewa nafasi ya kucheza dakika 90 sambamba na ‘Wa-kimataifa’ hao kunaweza kumuongezea utulivu na kufanya vitu vyake. Kutawala kiungo na kupiga pasi safi za mwisho kwa washambuliaji wake.

Hiki ndicho kinachomfanya Lwandamina kumng’ang’ania Mahadhi, lakini hataendelea kumsubiri wakati Pius Buswita atakapoanza kucheza kwa maana anaweza kurahisha vitu vingi kwa washambuliaji na kuwasaidia kufunga magoli majukumu ambayo bado yanawapa changamoto Rafael na Mahadhi.

Kumuanzisha tena Mahadhi vs Majimaji FC katika uwanja wa Majimaji, Songea kunaweza kumfanya Mahadhi kujrejesha kujiamini kwake lakini itambulike wazi kuwa licha ya Lwandamina kumpa nafasi hiyo Yanga inapaswa kupata matokeo na hilo lazima litambulike kwa Mahadhi.

Unapoaminiwa na kocha wako ni jambo zuri sana kwa mchezaji,  na huu ndiyo wakati wa Mahadhi kurejesha kujiamini kwake ili kuipaisha Yanga kwa maana  nafasi ya mchezesha timu inaonekana  imepelekwa mikononi mwake. Kama atashindwa sasa, Rafael, Buswita watampiga bao la ‘tobo’ japokuwa ushindi upo upande wake. Mahadhi hii ni nafasi yako ya mwisho, itumie sasa kutukumbusha pasi zako ‘rula’ na magoli ya ‘video.’

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here