Home Kitaifa Mwadini endelea kuvuta mshahara wa Azam ukiwa benchi au ingia kwenye darasa...

Mwadini endelea kuvuta mshahara wa Azam ukiwa benchi au ingia kwenye darasa la Manyika

7883
0
SHARE

Tayari klabu ya Azam imecheza mechi mbili za kwanza za ligi kuu Tanzania bara na kumshuhudia golikipa mkongwe wa klabu hiyo Mwadini Ali akiwa kwenye benchi huku golikipa mghana Razak Abalora akiwa kwenye lango.

Binafsi sikutarajia kumuona Mwadini akiwa kwenye ‘mbao ndefu’ akimpishsa golikipa mgeni wa ligi akicheza kama golikipa namba moja hususan kwenye mechi za mwanzo wa ligi.

Miaka sita iliyopita Mwadini alijiunga na Azam akitokea Zanzibar wakati huo Aishi Manula akiwa kwenye kikosi cha vijana. Baadae Manula akapandishwa kucheza kikosi cha wakubwa cha Azam.

Manula akapambana na kumtoa Mwadini kwenye reli na kuwa golikipa namba moja wa kutumainiwa ndani ya Azam kuanzia hapo Mwadini akafunga ndoa na benchi. Taratibu Manula akaanza kujitengenezea namba kwenye kikosi cha Stars hadi sasa ndio golikipa namba moja wa timu ya taifa.

Baada ya kuondoka kwa Manula ndani ya Azam niliamini ndio wakati wa Mwadini kutawala milingoti mitatu ya watoto wa Chamazi alipoanza kuanza kudaka kwenye mechi za kirafiki za kujiandaa na ligi hadi kuitwa kwenye kikosi cha Stars kilichocheza mechi ya kirafiki ya kalenda ya FIFA dhidi ya Botswana.

Hali imekua tofauti kabisa baada ya ligi kuanza, Mwadini amerudi tena benchi huku akiwa mzima wa afya. Ndanda vs Azam na Azam vs Simba mechi zote amekuwa kwenye benchi akimtazama Razak anavyofanya yake.

Huenda nikapishana na anachokifikiria Mwadini kwa sasa, kama anahitaji kucheza itakuwa sahihi kwake kuondoka Chamazi na kutafuta timu itakayompa nafasi ya kucheza mara kwa mara. Kwa umri alionao wa miaka 32  huenda ameamua kumalizia soka lake Azam, kama ni hivyo aendelee tu kuvuta mshahara wake wa kila mwezi na posho.

Chukua darasa kwa Manyika Jr

Kijana huyu ameshtuka na kuona kipaji chake kinafubaa akiwa Simba, aliletewa Vicent Ang’ban baadae Daniel Agyei mara zote alikuwa kipa namba mbili wa magolikipa hao kutoka nje ya Tanzania.

Licha ya kuwa kwenye klabu yenye jina kubwa Afrika Mashariki na Kati bado uwepo wake haukumsaidia kama mchezaji. Hakupata nafasi ya kucheza hali iliyo zorotesha kipaji chake.

Manyika aliamua kuachana na mabingwa hao wa zamani wa ligi baada ya mkataba wake kumalizika na kujiunga na Singida United timu iliyopanda daraja. Amefanikiwa kuanza kwenye mechi mbili za kwanza za ligi msimu huu Mwadui vs Singida United na Singida United vs Mbao FC.

Imekuwa bahati kwa Manyika kukimbia Simba kwa sababu ujio wa Manula ungemmaliza kabisa na angeishia kudaka kwenye mazoezi kama Manula angekua fit muda wote.

Kucheza ndio kila kitu kwa mchezaji

Wachezaji wengi wamekuwa wanashindwa kuondoka kwenye vilabu vya Simba, Yanga na Azam kwa kuhofia aina ya maisha watakayokumbana nayo nje ya timu hizo tatu.

Wanasahau kucheza ndio kila kitu, wanatakiwa warudi chini kupambana na ikiwezekana baadae warudi juu kucheza kwenye vilabu hivyo vikubwa wakiwa na uhakika wa kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

Mchezaji kama Boniface Maganga wa Mbao FC anaitwa kwenye timu ya taifa kwa sababu anapata nafasi ya kucheza kwenye klabu yake na kumshawishi kocha wa timu ya taifa kutokana na uwezo wake.

Kwa mchezaji kucheza ndio kila kitu mshahara baadae, Stamili Mbonde, Chidiebere, ni baadhi ya wachezaji waliopata timu nje ya nchi siku za hivi karibuni wakitokea Mtibwa na Stand United kwa sababu walionekana wanacheza. Kama upo Simba Yanga na Azam lakini huchezi upo kwenye hatari ukilinganisha na anayepata nafasi kwenye kikosi cha Ruvu Shooting.

Mwadini chagua mshahara wa Azam unaoupata ukiwa benchi au stuka ingia kwenye darasa la Manyika uondoke Azam ukacheze kulinda uwezo wako tukuone Stars na Zanzibar Heroes

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here