Home Kitaifa Mo Ibrahim sio tu ananikumbusha Haruna Moshi “Boban”, bali yeye ndio ufunguo...

Mo Ibrahim sio tu ananikumbusha Haruna Moshi “Boban”, bali yeye ndio ufunguo wa magoli Simba Sc

16905
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

Haruna Moshi ‘Boban’ alisajiliwa Simba SC mwishoni mwa mwaka 2002 akitokea Coastal Union ya Tanga.

Boban hakuonekana mchezaji muhimu sana klabuni Simba katika misimu yake miwili ya mwanzo lakini taratibu kuanzia mwaka 2004 kiungo huyo mshambulizi akaanza kuonesha kiwango cha juu huku uchezaji wake wa uhakika na uwezo wa kumiliki mpira, kupiga ‘pasi rula’ na kufunga ‘magoli ya video’ ukimpatia mashabiki wengi.

Si tu mashabiki wa klabu yake, bali hadi wale wa mahasimu wao Yanga SC walikuwa wakikoshwa sana uchezaji wa kiungo huyo wa zamani wa Coastal Union, Simba, Gelfe ya Sweden na Mbeya City FC.

MOHAMED IBHAHIM SIO BOBAN, ILA ……….

Mohamed Ibrahim sio Boban, ila anaweza kuvaa viatu vilivyoachwa na mchezaji huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania.

MO ananikumbusha vitu vingi kutoka kwa Boban wakati ule Simba ikicheza bila mshambulizi halisi wa kati kutokana tu na uwezo wa Boban kuingia katika mifumo mingi kiuchezaji na kurahisha mambo kwa Musa Hassan Mgosi, Nico Nyagawa, Ulimboka Mwakingwe na hata Moses Odhiambo wakati Fulani.

 ATAIBEBA SIMBA HIVI KATIKA 4-4-2

MO anaweza kucheza katika mfumo wowote ule na kutoa matunda. Kama timu ikicheza mfumo wa 4-4 2 kiungo huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar FC anaweza kutumika katika nafasi tatu bila tatizo lolote.

Kwa aina ya uchezaji wake wa utulivu, upigaji wa pasi zinazofika na shabaha aliyonayo kila anapo-shuti kuelekea golini mwa wapinzani, namuona MO akicheza vizuri kama mshambulizi wa pili katika mfumo huu(namba 10.)

Kwa mfano katika kikosi cha sasa pale Simba, MO anaweza kucheza kando ya mshambulizi, John Bocco, Juma Liuzio ama Mghana, Gyan (ambaye siwezi kumzungumzia kwa sasa.) Ni ngumu, MO kucheza na Mavugo kama washambuliaji wawili-pacha katika mfumo wa 4-4-2 kutokana na kwamba, mshambulizi huyo wa Burundi anapenda kucheza kwa kuhama hama.

Lakini kama, Mavugo anaweza kucheza eneo la kati tu na kusubiri kutengeneneza nafasi za kufunga wakati wenzake wakimiliki mpira ni rahisi kwa kikosi cha kocha, Mcameroon, Joseph Omog kupata magoli.

Lakini si hivyo tu, MO anaweza kucheza upande wa kushoto japo hataweza kupiga krosi mara kwa mara ila anaweza kuwafanya washambuliaji wawili wa kati ( ama, Mganda, Emmanuel Okwi+Maguvo, Bocco+Liuzio) wapate mipira sahihi ya krosi-pasi ili kufunga.

Mfano katika mfumo huu ( 4-4-2) ambao MO atakuwa tumika kama kiungo wa kushoto (namba 11) katikati ya uwanja ningeweza kuwapanga, Mghana, James Kotei na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, huku upande wa kiungo wa kulia akicheza, Muzamiru Yassin.

Kama nitawapanga viungo hawa wanne, nafasi ya washambuliaji wawili wa kuanza mchezo nitawapanga, Okwi huku nikimtaka Mavugo asimame kati tu, Okwi akicheza kando yake. Nitawapanga washambuliaji hao wawili kwa sababu wanaweza kufunga magoli kutokana na move nzuri za timu ikitokea nyuma.

Kumbuka viungo wanne ambao watakuwa nyuma ya washambuliaji hao wote ni wabunifu, wanapiga pasi nzuri na wana uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi za magoli. Japokuwa mfumo huu unahitaji sana krosi, Kotei, Niyonzima, Muzamiru, Mavugo, Okwi, na MO wote wanapendelea kucheza pasi za chini na si wazuri katika upigaji wa vichwa.

MO anaweza kufanya vizuri pia katika mfumo huu akitokea wing ya kushoto hata na washambuaji Liuzio na Bocco kama tu wawili hao wataongeza kasi yao katika kuwahi pasi zinazopitishwa njiani kuelekea golini mwa timu pinzani wakati timu ikipasiana. Vinginevyo si rahisi.

 MO, OKWI, KICHUYA KATIKA 4-3-3

 Katika mfumo huu, ili mambo yaende sawa na kwa haraka wachezaji hawa watatu ( MO, Okwi na Kichuya) lazima waanze pamoja huku nyuma yao wakitokea Kotei, Muzamiru na Niyonzima. Wakati anaondoka Simba mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2014/15, Okwi alikuwa mfungaji bora wa klabu, akichezeshwa kati na kocha Mserbia, Goran.

 Hii inamaanisha kiungo huyo mshambulizi wa Uganda anaweza kucheza kama mshambulizi wa kati, huku tabia yake ya kucheza eneo lote la mbele ikiwa fursa kwa washambuliaji wa pembeni, Kichuya akitokea kulia na MO akitokea upande wa kushoto, ama Kichuya akitokea kushoto, MO upande wa kulia.

Hapa ningekuwa na wafungaji watatu wenye shabaha huku nyuma yao kukiwa na wapishi wazuri wa pasi za magoli na ziada ya wafungaji ( Haruna na Muzamiru) Hivyo hata katika mfumo huu MO anaweza kufanya vizuri kutokana na aina ya uchezaji wake  na baadhi ya wachezaji wa nafasi za mbele katika kikosi chao.

Kama mchezaji wa nafasi ya mbele anaingia katika mifumo hii, ni rahisi sana kumtumia katika mifumo  mingine kama 4-5-1, 3-5-2 ambayo hutumika zaidi.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here