Home Kitaifa Yanga itaendelea kubebwa na washambuliaji, kikosi chao kimebalansi

Yanga itaendelea kubebwa na washambuliaji, kikosi chao kimebalansi

22038
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

Nilitazama pambano la kwanza la kujipima nguvu kwa kikosi cha Yanga SC siku ya Jumamosi. Na baada ya mabingwa hao mara tatu mfululizo wa ligi kuu Tanzania Bara kukamilisha usajili wa mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael kutoka Azam FC mara baada ya mchezo huo walioshinda 3-2 dhidi ya Singida United, ni wazi kikosi cha Mzambia, George Lwandamina ‘kimebalansi’ na kukidhi ubora wa ‘bingwa mtetezi.’

Machi mwaka huu nilipendekeza majina ya wachezaji nane ambao niliona wanahitajika katika kikosi cha Yanga ambacho kilionesha udhaifu hasa baada ya kusumbuliwa na majeraha kwa wachezaji wao wa nafasi muhimu.

GADIEL ATAZIBA NYUFA 

Gadiel  ni chaguo nililopendekeza. Mlinzi huyu wa kushoto wa Taifa Stars anashambulia kwa nguvu huku akiwa mwepesi kurudi katika nafasi yake baada ya kupeleka shambulizi mbele. Gadiel anakuja kuziba nyufa katika beki ya kushoto-sehemu ambayo imekuwa ikichangia sana magoli ya timu pinzani wanapocheza dhidi ya Yanga.

Oscar Joshua alikuwa imara, alipendelea kushambulia kwa mipira mirefu na kubaki katika nafasi yake. Majeraha yaliathiri sana kiwango chake na hivyo akajikuta akipoteza namba yake kwa Mwinyi Haji. Mwinyi ni mlinzi mzuri sana, lakini uchezaji wake wa kushambulia  ulimsahulisha mara kwa mara na kujikuta akishindwa kucheza kama beki halisi wa kushoto ambaye atakuwa na jukumu la kuzuia mipira ya krosi.

Wakati Mwinyi hakuwa akitumia nguvu nyingi katika kuzuia, Gadiel yeye ana uwezo wa kushambulia kwa nguvu na kuzuia kwa nguvu pia huku akionekana ni mchezaji mwenye pumzi ya kutosha.

GOLINI SAFI

Kumsaini golikipa Mcameroon, Youthe Rostand na kijana U17, Ramadhani Kabwili kama wabadala wa Deo Munishi ‘Dida’ aliyejiunga na Pretoria University ya Afrika Kusini na Ally Mustapha aliyejiunga Singida United pia ni usajili mzuri kwa maana kipa huyo wa zamani wa African Lyon anaweza kufanya kazi nzuri kwa kushirikiana na Beno Kakolanya ambaye alifanya vizuri katika michezo ya mwishoni mwa msimu uliopita.

BEKI YA KATI INAHITAJI KUMUONA PATO NGONYANI

Wasiwasi mkubwa unweza kuibuka kama Abdallah Haji Shaibu atashindwa ‘kuichezea Yanga’ baada ya kusajiliwa kutoka Jang’ombe Boys ya Zanzibar. Katika mchezo uliopita vs Singida United safu ya ulinzi wa kati iliyokuwa chini ya nahodha, Nadir Haroub na Kelvin Yondan ilionesha udhaifu wa kushindwa kujipanga.

Hakutakuwa na tatizo kwa kuondoka Mtogo, Vicent Bossou kama vijana Shaibu na Pato Ngonyani watajiimarisha na kuwa tayari kuchukua nafasi za Kelvin na Nadir, lakini kama wawili hao ( Shaibu na Pato) watashindwa kuwa tayari naona Yanga ikipata wakati mgumu hasa ikitokea majeraha kwa wazoefu hao wanaoingia msimu wa sita wakicheza pamoja katika beki ya kati ya Yanga.

RAFAEL DAUD KUWASAHAULISHA NIYONZIMA

Jonas Mkude, Ken Ally na Rafael Daud ni majina mengine matatu ambayo niliyapendekeza na kuwatazama kama wachezaji ambao wangeweza kuimarisha safu ya kiungo katika kikosi cha Lwandamina. Yanga ilijaribu kuwasaini wote hao lakini baadae ikafanikiwa kumpata Daud ambaye alifunga magoli nane msimu uliopita akiichezea Mbeya City FC.

Kumpoteza Haruna Niyonzima ni pengo, lakini hakuna tatizo kwa kikosi ambacho kitajengwa kama timu. Haruna aliiisaidia sana Yanga msimu uliopita lakini kuna kitu kipya Yanga inahitaji katika uchezaji wao. Kucheza mpira wa kushambulia moja kwa moja. Licha ya uwezo wake katika upigaji wa pasi na kumiliki mpira, Niyonzima kuna wakati alikuwa akichelewesha sana ushindi kwa pasi zake za pembeni.

Daud hucheza kwa kupiga pasi za kwenda mbele, na yuko haraka katika upigaji wa pasi hivyo japo si mahiri sana kama Haruna katika kumiliki mpira ila namuona akiharakisha sana ushindi wa timu yake. Anaweza kuleta kitu kipya kikosini.

Ili Yanga iendelee kuwa imara ni lazima wachezaji wengine kama Juma Makapu, Juma Mahadhi wawe tayari kimazoezi kuchukua nafasi za Mcongoman, Tshishimbi,Mzimbabwe, Thaban Kamusoko. Wana viungo watatu mahiri wa kati,huku Shaibu, Pato wakiweza pia kucheza katika nafasi ya kiungo-mlinzi.

WASHAMBULIAJI WATAENDELEA KUTIKISA SANA NYAVU 

Kumpoteza mchezaji aliyefunga magoli 46 katika misimu mitatu pekee ya ligi kuu ni jambo baya hasa ukizingatia tayari timu hiyo imepoteza injini muhimu katika safu za golikipa, beki ya kati na kiungo. Lakini ilikuwa ni lazima Saimon Msuva aondoke Tanzania na kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Morocco.

Lwandamina amemsaini kjana Baruani Akilimali ambaye ni mchezaji huru na VIUNGO WASHAMBULIAJI Pius Buswita kutoka Mbao FC na Ibrahi Ajib kutoka Simba SC. Ukitoa Akilimali ambaye hajawahi kucheza ligi yoyote ya juu, Ajib na Buswita ni maingizo ambayo yanaweza kuimarisha sana timu hiyo katika mashambulizi.

Uwepo wa washambuaji wane wenye uwezo wa juu,Mrundi, Amis Tambwe, Mzimbabwe, Donald Ngoma, Mzambia, Obrey Chirwa na kijana Matheo Anthony moja kwa moja unafanya kocha Lwandamina kuwa na wigo mpana wa kufanya machaguo katika safu ya washambuliaji wa kati.

Emmanuel Martin, Ajib, Buswita wote hawa wanaweza kuondoa ‘kivuli’ cha Msuva ndani ya Yanga na kuwasahaulisha mashabiki wa timu kutokana na mifumo ya kuchezaji.  Yanga wana kikosi kizuri sana na kilicho pamoja kwa muda mrefu kuliko vikosi vyote vya ligi kuu msimu ujao. Hii inamaanisha ‘wapo katika umbo sahihi’ kuelekea msimu mpya.

Kufunga magoli matatu katika mchezo wao wa kwanza wa kujiandaa na msimu ni dalili kuwa Yanga itaendelea kufunga magoli kadri itakavyowezekana lakini tayari Lwandamina anaonekana kuwa na kazi kubwa ya kufanya katika safu yake ya ulibnzi wa kati hasa ukizingatia iliruhusu magoli mawili na kusabibisha mikwaju miwili ya penalty walipocheza dhidi ya Singida United.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here