Home Kimataifa Ifahamu zaidi Baroka FC, timu iliyomsajili Abdi Banda wa Simba 

Ifahamu zaidi Baroka FC, timu iliyomsajili Abdi Banda wa Simba 

16038
0
SHARE

Na Salym Juma, Arusha

Nikinukuu kauli ya Abdi Banda katika maandishi kwamba, wachezaji wajitume na wanatakiwa kuwa makini na nafasi, hasa zinapotokea nafasi za kutoka kwenda kucheza nje ya nchi na wasiangalie nyuma. Kauli ya Beki huyu wa zamani wa Simba inawagusa Wachezaji ambao wanaamini Simba na Yanga ndio sehemu pekee ya mafanikio ambayo wanapaswa kufika. Ukweli ni kwamba hata hao akina Samatta na Ulimwengu walifika hapo walipo baada ya kuondoka Tanzania na kwenda kujaribu bahati zao nje.

Kufanya vizuri kwa Abdi Banda msimu uliopita kumemfanya mchezaji huyu kupata nafasi ya kusajiliwa na timu iliyoshiriki ligi kuu ya South Afrika msimu uliomalizika. Banda ambaye tayari alishasaini mkataba wa kujiunga na klabu hiyo wakati akiwa kwenye michuano ya COSAFA Cup 2017 iliyofanyika South Afrika anakwenda kucheza kwenye ardhi ya Mandela na kama akikitumia vyema kipaji chake huenda akapata shavu kwenye vilabu vikubwa vya South Afrika.

Banda ni aina ya wachezaji ambao hupenda sana kuuchezea mpira na mara nyingi hujaribu kupiga mashuti ya mbali langoni mwa mpinzani. Kitu cha msingi cha kuzingatia ni nidhamu kwani wachezaji wetu wanapaswa kuiga nidhamu ya akina Samatta au Himid Mao. Japo Banda amekuwa na nidhamu yenye mashaka na makosa ya hapa na pale ila naamini anao muda mzuri wa kurekebisha haya kabla ya kuanza kukipiga klabuni.

Watanzania wengi wanatamani kuijua kwa undani timu hii anayokwenda mchezaji huyu wa zamani wa Simba na Taifa Stars kwa sasa.

Baroka F.C ni klabu iliyopo South African inayotokea Ga-Mphahlele karibu na Polokwane, Limpopo. Timu hii ni miongoni mwa timu zilizoanzishwa hivi karibuni na imekuwa na mwenendo wa kuridhisha kadiri siku zinavyosonga. Tangu mwaka 2007 ilipoanzishwa ilijitahidi kupanda daraja kwenye msimu wake wa kwanza ila mechi ya mwisho kabisa iliwakwamisha baada ya kutoka sare na Thanda Royal Zulu. Baroka ni Timu changa ambayo inaweza kuwa na uhai mrefu huko tunapoelekea.

Baada ya mwaka 2011 kufika nusu fainali ya michuano ya Nedbank Cup, Baroka FC ilijizolea umaarufu nchini South Africa hasa kutokana na kiwango cha juu ilichokionesha kwa kuvitoa vigogo kama Moroka Swallows na Kaizer Chiefs kabla ya Orlando Pirates kushinda 3–1 dhidi ya Black Leopards katika uwanja wa Mbombela. The black ones waliiwakilisha South Africa kwenye Kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kushinda. Endapo Baroka wangefika fainali wangekuwa na nafasi kubwa ya kucheza CAF.

Msimu wa 2015–16 Baroka walikuwa mabingwa wa ligi daraja la kwanza na kupanda ligi kuu ya South Afrika, ligi yenye thamani kubwa kusini mwa jangwa la Sahara. Uwanja wa Peter Mokaba uliochezesha mechi nne za Kombe la Dunia 2010 upo Mashariki umbali wa Kilometa 4 pekee kutoka uwanja wa Pietersburg unaomilikiwa na Baroka FC. Uwanja huu wa Baroka unachukua takribani Watazamaji 15000 walioketi vitini.

Banda anakwenda kukutana na wachezaji wasumbufu kwenye michuano mbalimbali nchini South Afrika mfano Lebogang Manyama, Tendai Ndoro wa Orlando Pirates, Rodney Ramagalela wa Polokwane Gabadinho Mhango na Jeremy Brockie wa Super Sport. Polokwane City FC ndio wapinzani wa jadi wa Baroka kutokana na kutoka ukanda mmoja. Kumbuka Polokwane City FC wanashiriki katika ligi kuu ya Afrika Kusini na kipindi cha karibuni wamekuwa wakifanya vyema.

Baroka FC walichukua ubingwa wa ligi daraja la pili kanda ya Limpopo mwaka 2010–11.  Abdi Banda anatakiwa kwenda ‘kukaza’ kwa timu hii ni miongoni mwa vilabu vinne vilivyoruhusu zaidi ya magoli 40 msimu uliopita kwenye ligi kuu ya South Afrika.  Banda hatokuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kwani kiungo wa Gor Mahia FC Khalid Aucho pia alisaini mwaka jana. Baroka inavaa uzi unaofanana na ule wa Yanga au Singida United.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here