Home Kimataifa Kwanini nyota ya Verratti inang’aa hata kukiwa na mawingu mazito?

Kwanini nyota ya Verratti inang’aa hata kukiwa na mawingu mazito?

4805
0
SHARE

Na Salym Juma, Arusha

Jezi namba 6 ndiyo iliyokabidhiwa na PSG kwa kiungo mkorofi aliyezaliwa miaka 24 iliyopita pale Pescara. Hii ilikuwa baada ya kuwaniwa na vilabu kadhaa kama Napoli, Roma na Juventus mnamo mwaka 2012. Uwezo wake wa kutawala kuanzia chini (mbele ya mabeki) hadi eneo la ‘final third’ la timu pinzani uliwafanya Pescara kushinda taji la Serie B mwaka 2012. Kujiunga kwake PSG kumemfanya kupevuka na sasa, mbali na Barcelona, vilabu kadhaa vilitajwa kuwania saini yake kabla hata ya dirisha kufunguliwa na leo hii tujaribu kutazama kwanini Marco Verratti amekuwa akiwaniwa…

Kabarikiwa uwezo wa kuwa kiungo wa kati Mchezeshaji. Verratti ni miongoni mwa viungo wachache wenye kipaji hiki kwani tumezoea kuwaona viungo wengi wa kati wakiwa na kipaji kimoja cha kukaba ila linapokuja suala la kukaba na kuichezesha timu kwa wakati mmoja hauwezi ukawakuta viungo wengi, bila shaka wapo wachache na katika hao wachache Verratti ni miongoni mwao, kumbuka viungo wengi wachezeshaji hukaa juu kidogo ya eneo la katikati ila kwa Verratti ni tofauti. Uwezo huu unamfanya ‘afiti’ katika timu nyingi kama Barcelona, Arsenal na hata Chelsea.

Uwezo mkubwa wa kukokota mpira. Kimombo wanaita ‘dribbling skills’. Ni viungo wachache sana wanaomudu kazi hii ambayo ni nyepesi kwa washambuliaji kama akina Neymar, Hazard, Messi, CR7 na Dybala. Verratti ni mwepesi wa kupiga vyenga na ushahidi wa hili wanao Chelsea na Barcelona. Uwezo huu ni rahisi kuibeba timu hasa pale ambapo timu yake inapokuwa imetawala eneo la kiungo kwani Verratti hugeuka kiungo mshambuliaji na hapa ndipo alipotoa zile ‘assist’ na hata kufunga pia. Kipaji hiki ndicho kinamtofautisha na mkongwe Andrea Pirlo ambaye amekuwa akifananishwa naye.

Maamuzi ya haraka na uwezo mkubwa wa kuudhibiti mpira katika eneo lake. ‘Control’ ni uwezo ambao wachezaji wengi wanaocheza Ulaya wamejaaliwa ila kuwa na uamuzi wa haraka tena chanya ambao unainufaisha timu uwanjani ni jambo ambalo viungo wachache wamebarikiwa. Maamuzi ndiyo yaliyowafanya akina Xavi, Pirlo, Lampard na Gerald kuwa na heshima waliyonayo hivi sasa. Verratti ni mwepesi wa kumnyang’anya mpinzani mpira eneo lolote tena bila kucheza faulo. Marco pia anaweza kutoa pasi yenye madhara kwa wapinzani sehemu ambayo hukuitarajia.

Ni mzuri wa kupooza mashambulizi na kurudisha umiliki wa timu. Bila shaka eneo hili wengi wanalimudu. Siwezi kumuacha Herera, Wanyama au Kante katika kufanya kazi hii ila nahitajika kumzungumzia Verratti kwani shughuli aliyoionesha dhidi ya Barca haikuwa ya kawaida. Vilabu vya League 1 vinaujua uwezo wake hasa pale PSG inapokuwa katika hali ya kushambuliwa. Niliwahi kumuona akiwatesa Chelsea, Barca, Monaco na Lyon katika anga hii kwani ni mwepesi wa kumnyang’anya mpinzani mpira na kupiga vyenga hadi timu ikapunguza presha na kurudi katika hali ya kawaida.

Macho makali ya kupiga pasi ndefu na kuwatengenezea wenzake nafasi ni jambo lingine linalomfanya Verratti kucheza popote. kupiga pasi ndefu zenye madhara ni kazi ya watu wachache kama akina Fabregas, Alonso, Carick au Pirlo ila Verratti ni mtu sahihi katika eneo hili ambalo Barcelona wanahangaika kumtafuta Xavi wa zama hizi. ‘Assist’ 7 alizotoa katika michezo 31 na magoli mawili ni ishara tosha kuwa Macho yake hayahitaji miwani uwanjani. PSG imeshinda mara 9 katika michezo 10 ya mwisho huku Verratti akionekana kama mhimili mkubwa katika ushindi huu.

Japokuwa amekuwa na mapungufu kadhaa katika mipira ya juu na nidhamu mbovu ila mapungufu ni machache kuliko ubora wake uwanjani. Uwezekano wa Verratti kubaki PSG ni mdogo mno kutokana na kutajwa kuwa mrithi wa Cazola pale Emirates au kwenda kuboresha eneo la katikati pale Camp Nou. Usajili wa Bakayoko kwenda Chelsea utapunguza nguvu ya Verratti kuwaniwa darajani ila bado soko lake ni kubwa sana barani Ulaya kwani licha ya majina ya viungo wengi kutajwa kipindi hiki, Verratti anaweza kuwapiku kwa bei endapo atasajiliwa katika majira haya.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here