Home Kimataifa Kwa kasi hii ya Ujerumani, Ulaya na dunia itazidi kupata manyanyaso zaidi...

Kwa kasi hii ya Ujerumani, Ulaya na dunia itazidi kupata manyanyaso zaidi ya waliyopata kwa Hitler

6659
0
SHARE

Na Salym Juma, Arusha

Ikiwa ni miaka minne tangu Wajerumani wafanye maangamizi pale Brazil, Wajerumani bado wameendelea kutoa dozi katika michuano mbalimbali huku wakiiaminisha Dunia kuwa bado ina vizazi vinavyoweza kufanya makubwa zaidi ya yale waliyofanya kule America hasa kwa kuzitoa timu kubwa za America, Brazil nusu fainali na Argentina fainali. Uwekezaji uliofanywa na Wajerumani haukuja kwa bahati mbaya, ni mipango thabiti iliyoanzia chini na huenda ikadumu miaka mingi ijayo hasa katika michuano iliyochini ya FIFA na UEFA. Wajerumani wamechukua vikombe viwili vikubwa ndani ya siku 4 barani Ulaya.

Uwepo wa mataifa makubwa kwenye michuano ya Mabara kama Chile, Ureno na Mexico haukumuogopesha Joachim Low kuwaacha vijana na badala yake majina mazito kama Aturo Vidali, Vargas, Sanchez, Christiano Ronaldo yaligeuka chachu kwa vijana wa Kijerumani kucharuka na kufanya maangamizi ndani ya ardhi ya Warusi. Ukitizama majina haya Ter Stegen, Ginter, Rüdiger, Kimmich, Goretzka, Süleat, Rudy, Draxler na Werne unaweza kuzani kwamba jamaa labda walitolewa kwenye makundi ila ukiambiwa wameitoa Chile iliyosheheni majina yote unaweza kubaki mdomo wazi.

Wanasoka walibaki midomo wazi kutoitwa kwa Manuel Neuer, Mesut Ozil na Thomas Muller kwenye michuano ya mabara ila mapengo yao yalizibwa vyema na Rudy, Draxler na Werne baada ya Joachim Low kuwapa majukumu na kuwaaminisha kuwa wanaweza. Miaka mingi Ujerumani ilikuwa ikiwategemea Miroslav Klose, Mario Gomez na Muller kwenye idara ya ushambuliaji ila umri na uwezo wao umezidi kudorora hali inayofanya vijana kuanza kupewa nafasi mapema kabla ya jua kuchomoza ili wasije kuaibika kwenye michuano ijayo.

Kiwango kikubwa cha vijana wa U-21 kilichoifunga Hispania ni alarm kuwa Wajerumani wana muda mrefu sana wa kulitawala soka la Ulaya na Dunia. Uimara wa akina Sammy Khedira, Ozil, Neuer na Muller ulianzia humuhumu walipo akina Draxler na Werne hivi sasa. Uwezo huu haukuja kwa bahati nasibu ila ni mipango thabiti iliyowekezwa na watu wenye dhamira ya kweli kwenye mpira na sio siasa kama ilivyo kwa wanaojiita wataalamu kutoka TFF. Kikosi cha U-21 kimechukua ubingwa mbele ya Hispania, England, Italia na Denmark mataifa yanayoaminika kuwa na timu bora za vijana.

DFB {Shirikisho la soka la Ujerumani} chini ya Reinhard Grindel wanajua nini wanachotakiwa kukifanya ili wazidi kulitawala soka la Dunia. DFB ina wanachama {mashirikisho ya ndani} 21 huku kukiwa na vilabu rasmi zaidi ya 25,000 vinavyoshiriki ligi mbalimbali zinazotambuliwa na DFB. Uwepo wa wanachama zaidi ya 6.8 million unalifanya shirikisho hili kuwa la kwanza kwa ukubwa na ufanisi duniani huku mashirikisho mengine yakiendelea kusubiri. Kuwepo kwa karibu timu 171,000 nchini Ujerumani kunafanya idadi ya wachezaji waliopo Ujerumani pekee kufikia zaidi ya millioni mbili.

DFB iliwahi kukaririwa ikisema kuna wachezaji takribani Millioni 6 wanaocheza kwenye michuano rasmi na ile isiyo rasmi huku kila wikiendi kukiwa na michezo rasmi zaidi ya 3000 nchini Ujerumani. Unadhani kwa mipango hii kuna cha kushangaa ukiona wajerumani wanachukua vikombe kwa jinsi wanavyotaka? Ukweli uatabaki daima, mafanikio hayawezi kuja kwa bahati mbaya hata siku moja bali ni mipango inayoeleweka hasa ya kutengeneza vijana na waalimu wa soka kama ilivyofanya DFB kwa ushirikiano wa karibu na serikali ya Ujerumani.

Naamini Joachim Low atakuwa na wakati mgumu wa kuchagua kikosi kwenye michuano ijayo hasa kutokana na uzuri wa wachezaji alionao kuanzia ngazi ya vijana hadi wakongwe. Endapo hatokuwa makini katika uchaguzi atalaumiwa na wajerumani kwani nchi yao ina kila kitu, kila aina ya mchezaji na uzoefu pia. Ni wakati muafaka kwa viongozi wa soka la Bongo kujifunza kitu kutokana na mafanikio ya wajerumani ndani ya siku hizi chache. Kutokana na mipango waliyoweka Wajerumani naweza kusema kwa kasi hii Ulaya na Dunia itazidi nyanyasika zaidi ya ilivyonyanyasika kwa Hitler.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here