Home Kimataifa Everton kutembeza darasa kwa viongozi wa Club nchini.

Everton kutembeza darasa kwa viongozi wa Club nchini.

2919
0
SHARE

Kuelekea ujio wa Everton nchini, bado tuna mambo mengi ya kuzungumza na kukumbushana tukiwa kama wadau wa soka.

Kabla ya mechi itakayoigwa Julai 13 kwenye dimba la Taifa, sote tunatambua kuwa kutakuwa na semina za kuwajengea uwezo viongozi wetu wa soka nchini, makocha, wachezaji wa timu za vijana pamoja na waandishi wa habari za michezo zitakazofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kuelekea kwenye semina hizo ambazo zina maana kubwa sana katika soka letu, tueleweshane kidogo mambo muhimu ambayo yatazungumziwa kwa undani zaidi

Moja ya mambo ambayo Mkurugenzi Mkuu wa Everton, Robert Elstone aliyazungumzia kwenye ujio wao wa kwanza nchini mwezi uliopita ni kuhusu umuhimu wa klabu ya mpira wa miguu kuwa na miundombinu bora.

Miongoni mwa miundombinu hiyo ambayo Ndugu Elston alitilia mkazo ni pamoja na uwanja ambapo alisema kuwa kila klabu inatakiwa kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanja ikiwa ni moja ya miundombinu inayoingiingizia klabu pesa nyingi sana.

“Nafikiri kwa upande wa kibiashara, kitu kimojawapo ambacho tunataka kufanya ni kuwekeza katika ujenzi wa miundo mbinu. Miundo mbinu ni jambo la msingi sana kwenye mpira wa miguu.”

“Kama ukipata uwanja ambao unakufaa ukiwa na ukubwa ambao ni sahihi, ambao una miundombinu sahihi na pia katika mazingira mazuri kwa mashabiki ni muhimu sana. Kama una nafasi ya kuwekeza kwenye miundombinu bora ya soka basi huna budi kufanya hivyo”, alitilia mkazo Robert Elstone.

Hayo ni maneno ya kiongozi wa klabu ya mpira wa miguu ambaye ana maono ya kibiashara huku akiwa kwenye mpango kabambe wa kutumia paundi milioni 300 ambazo ni zaidi ya shilingi za kitanzania bilioni 866 ili kujenga uwanja mkubwa zaidi unaochukua mashabiki 60,000 ukiwa ni mbadala wa uwanja wa sasa wa Goodison Park unaochukua mashabiki 40,157 tu.

Everton wana kila sababu ya kufanya hivyo ikiwa kama klabu yenye malengo ya kujitanua kibiashara na. Lakini pia kwa sasa utaona jinsi ambavyo vilabu mbalimbali barani Ulaya hususani nchini Uingereza kama vile Chelsea, Tottenham Hotspurs, Liverpool na Manchester City vikiwa kwenye harakati hizo hizo kutokana na jinsi ambavyo wameona fursa kutokana na kuwa na viwanja vikubwa na wanataka kuitumia fursa hiyo ili kukuza uchumi wa vilabu vyao.

Bila shaka ukiwa na uwanja utaweza kuingiza pesa kupitia viingilio vya uwanjani, pia utaweza kukodisha maduka nje ya uwanja kwa wafanyabiashara mbalimbali, pia utaweza kukodisha kumbi zilizomo ndani ya uwanja kwa ajili ya mikutano na shughuli za mikusanyuiko kama vile harusi lakini pia bila kusahau ziara ambazo hufanywa na mashabiki katika viwanja vya mpira ambapo hulipia.

Hizi ni baadhi ya faida za kumiliki uwanja wa mpira ambazo Robert Elston anazizungumzia na bila shaka kwa sasa utakuwa umepata picha ya kwanini vilabu mbalimbali barani vinaumiza vichwa kupanua viwanja vyao na kuvifanya viwe bora zaidi ndani na nje.

Haya ni baadhi ya ‘madini’ ambayo viongozi wetu wa vilabu nchini watapewa kutoka kwa wataalamu wa biashara wa klabu ya Everton wakiongozwa na Mkurugenzi mkuu mwenye, Robert Elstone kwenye semina za kuwajengea uwezo zitakazofanyika pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) siku ya tarehe 12 na 13 Julai.

Umefika wakati kwa viongozi wetu wa soka kupigwa msasa ili hatimaye waweze kuhamia wenye ulimwengu wa soka wa kidigitali ambao soka ni biashara kubwa ya kiushindani kama zilivyo biashara nyingine kubwa.

Kwa klabu kubwa ya mpira kukaa miaka zaidi ya 80 bila ya kumiliki uwanja wa mpira sio jambo la kulifumbia macho hata kidogo. Kuna haja ya kuwaweka chini na kuwapa somo ambalo litawafumbua macho.

Hakika ujio wa Everton umebeba ‘madini’ mengi.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here