Home Kitaifa Naamini Manula atakuwa na wakati mgumu kuziba pengo la Kaseja Simba

Naamini Manula atakuwa na wakati mgumu kuziba pengo la Kaseja Simba

12567
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

GOLIKIPA, Aishi Manula, walinzi wa pembeni, Shomari Kapombe na Jamal Mwambeleko, na mshambulizi, John Bocco wamesajiliwa Simba SC wakati huu wa usajili ili kuboresha kikosi chao ambacho kilimaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita na kushinda taji la FA ambalo limewapa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Caf Confederation Cup 2018.

Aishi Manula  

Wakati Azam FC ilipokuwa katika maandalizi ya kuanza msimu wa 2014/15 nilipata nafasi ya kwenda kufanya mahojiano na wachezaji watano wa Azam FC na mmoja wa wachezaji ambao nilifanya naye mahojiano ni golikipa huyu kijana wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars.’

Alinieleza chimbuko lake, na jinsi alivyopata nafasi ya kusajiliwa Azam FC. Aishi alinieleza kuwa malengo yake si kucheza klabu za Simba na Yanga kama itatokea yeye kuondoka Azam FC basi ni kwenda kutafuta nafasi ya kucheza na kutengeneza maisha yake nje ya Tanzania. Karibia miaka mitatu sasa tangu nilipofanya naye mahojiano golikipa huyo amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba.

Tangu kuanza kwa tetesi za yeye kujiunga Simba, kukanusha kwake mara kwa mara niliamini Aishi hawezi kujiunga na mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara.

Lakini tofauti na matarajio yangu kipa huyo amekubali kusaini Simba kwa kile alichodai kutopewa thamani na klabu yake ya zamani (Azam FC) ambao licha ya kuelekea mwisho wa mkataba wake alikuwa tayari kuongeza mkataba wa kuendelea kuichezea timu hiyo iliyomsaini mwaka 2012 na kumuendeleza kielimu akitokea nje ya mkoa wa Morogoro.

Manula anadai alikuwa tayari kuendelea kufanya kazi yake Chamanzi Complex lakini kitendo cha uongozi wa Azam FC kutaka kumsaini kwa dau la chini ya milioni 20 kwake kilimsikitisha sana.

Kweli kabisa, hata kama Azam FC imeamua kuingia katika sera ya kubana matumizi lakini kwa mchezaji mwenye uwezo wa juu, nidhamu isiyo na mfano na kipa namba moja wa timu ya Taifa ni wazi hawakuthamini uwezo wake.

Siungi mkono hoja ya golikipa huyo eti ameamua kuichagua Simba ili kupata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa bali naamini mshahara wa milioni 3 kwa mwezi na dau la usajili lisilopungua milioni 50 ndiyo ‘kichocheo’ cha yeye kusaini Simba.

Usajili huu umekuwa na manufaa kwa kila upande. Simba imekuwa na tatizo la golikipa tangu alipoondoka Juma Kaseja katikati ya mwaka 2013.

Mganda, Abel Dhaira (Mwenyezi Mungu amerehemu,) Ivo Mapundb, Manyika Peter Manyika, Hussein Shariff, Muivory Coast, Vicent Angban na Mghana, Daniel Aggey wote hawa wameonekana kushindwa kuziba pengo lililoachwa na Kaseja ambaye aliachana na timu hiyo kwa kile kilichotajwa na uongozi wa Ismail Aden Rage kuwa ‘amekwisha.’

Katika tuzo za wachezaji bora wa msimu uliomalizika kwa Yanga kutwaa ubingwa wa tatu mfululizo, Aishi alishindana na Kaseja katika tuzo ya golikipa bora wa msimu na kijana huyo akafanikiwa kushinda tuzo hiyo.

Je, Aishi ataweza kuwasahaulisha Simba kuhusu uwezo wa Kaseja? Bila shaka kwa usajili wa golikipa huyu Simba imepata kipa bora na ni wakati sasa wa kijana huyo kuongeza uwezo zaidi na kuisaidia timu yake mpya.

Aishi hawezi kuwa ‘Kaseja Mpya’ lakini anaweza kutengeneza jina lake na kuwa kipa bora zaidi wa timu hiyo katika ‘muongo’ huu wa pili wa karne mpya kama ilivyokuwa kwa Kaseja katika muongo uliopita.

Wasiwasi pekee wa kukua kimchezo kwa golikipa huyo ni uongozi wa timu yake mpya ambao umekuwa ukiwanyanyasa wachezaji katika haki zao za kimsingi, ufanyaji wao kazi umekosa maelewano na kila timu inapoanguka hukimbilia kuwarushia lawama wachezaji hasa magolikipa.

Dhaira, Mapunda, Manyika, Shariff, Angban, na Agyei wote hawa wamewahi kushutumiwa hadharani na uongozi wa Simba ilipotokea wameruhusu magoli ambayo kwao huonekana ni ya kizembe.  Aishi ni kipa bora kwa sasa katika soka la Tanzania lakini ni namna gani ataendelea kuongeza ubora wake katika timu isiyo na umoja hilo ni jambo la kusubiri na kuona.

Agyei  ni kipa mzuri lakini tatizo lake si mzuri katika upangaji wa ngome, na Aishi ni kipa bora katika upangaji wa beki na kucheza mipira inayotokea mbele lakini bado hajakamilika katika uchezaji wa mipira ya krosi na kona hivyo ni jukumu lake mwenyewe kujiimarisha ili awe bora zaidi.

Ataifanyia nini Simba SC isiyo na ‘ustahimilivu’ kwa wachezaji wanaofanya makosa ya kimchezo? Tusubiri na kuona ila hadi sasa naamini kila upande umefanikiwa katika usajili huu.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here