Home Kitaifa Boniphace Maganga kufuata nyayo za Mwambeleko, Hozza kutimka Mbao FC

Boniphace Maganga kufuata nyayo za Mwambeleko, Hozza kutimka Mbao FC

6269
0
SHARE
Mlinzi wa kulia wa Mbao FC Boniphace Maganga (kushoto) amesema kama atapata ofa nzuri na kufikia makubaliano ataondoka Mbao kwenda kutafuta changamoto mpya

NA Baraka Mbolembole

Boniphace Maganga ni zao la MARSH Academy ya jijini Mwanza. Akiwa na umri wa miaka 22 hivi sasa mlinzi huyo wa kulia alikuwa na msimu mzuri katika ligi kuu Tanzania Bara baada ya kucheza michezo 26 kati ya 30 ya klabu yake ya Mbao FC ya jijini Mwanza huku akicheza michezo yote mitano ya timu yake katika michuano ya FA Cup.

Maganga ambaye amemaliza msimu wake wa pili katika ligi kuu Bara alicheza michezo isiyozidi 15 msimu wa 2015/16 akiwa na vikosi vya Simba SC na Mtibwa Sugar FC kwa sasa amemaliza mkataba wake na klabu ya Mbao.

“Msimu wangu wa kwanza katika ligi kuu haukuwa mzuri sana.” Anaanza kusema kijana huyo ambaye alisajiliwa Simba katikati ya mwaka 2015 na kocha Muingereza, Dylan Kerr baada ya kufuzu majaribio.

“Ndani ya kikosi cha Simba sikufanikiwa kupata nafasi ya kucheza na ulipofika wakati wa usajili wa dirisha dogo mwezi Disemba nilipelekwa kwa mkopo Mtibwa Sugar na kumalizia msimu wa 2015/16. Kiukweli haukuwa msimu mzuri sana kwa sababu nilicheza michezo ambayo haikuzidi 15.”

“Kwa sasa nipo nyumbani Mwanza nimepumzika baada ya msimu kumalizika. Kuna timu tayari nimezungumza nazo lakini siwezi kuziweka wazi hivi sasa hadi hapo usajili wangu utakapokamilika.” Anasema beki huyo ambaye aliisaidia sana Mbao FC kubaki katika ligi kuu na kuifikisha fainali ya michuano ya FA.

“Siwezi kusema kama huu ni wakati mwafaka kwangu kuachana na Mbao ila itakapokuja nafasi ya kujaribu changamoto mpya mahala kwingine nitaichukua nafasi hiyo na kuondoka Mbao. Nilikuwa na bahati kubwa sana kufundishwa na kocha Etienne kwa sababu ni kocha bora katika mbinu na ufundi, pia ana uwezo mkubwa wa kuwajenga wachezaji na kuwapandisha viwango vyao. Etienne amekuwa rafiki mzuri sana kwa wachezaji.”

Tayari Mbao imeshawapoteza wachezaji wake wane ambao wamejiunga na vilabu vikubwa vya Simba na Azam FC. Golikipa Benedict Haule yeye ameungana na kiungo Salmin Hozza kujiunga na Azam FC, huku mlinzi wa kushoto, Jamal Mwambeleko akijiunga na Simba.

Nahodha wa kikosi hicho, Mrundi, Yusuph Ndikumana, na patna wake Mghana, Ahsante Kwesi wanasakwa na vilabu vya Azam FC na Yanga SC hii inamaanisha kikosi hicho kilichopanda daraja msimu uliopita kitaendelea kubomolewa na vilabu vyenye nguvu na ushawishi wa pesa msimu huu wa usajili.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here