Home Kitaifa Stars itapigwa nyingi vs Uganga kwa beki ya Banda/Mbonde, Samatta ni namba...

Stars itapigwa nyingi vs Uganga kwa beki ya Banda/Mbonde, Samatta ni namba kumi…’

16234
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

WAKATI alipokutana na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza baada ya kutangazwa rasmi kubeba mikoba ya kuiongoza timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ mwanzoni mwa mwaka huu, kocha Salum Mayanga aliahidi mabadiliko.

Upande wangu niliamini hivyo pia lakini sikudhani kama mabadiliko hayo yamelenga kumaliza zama za Kelvin Yondan ambaye ni miongoni mwa mabeki bora wa kati waliopata kutokea nchini katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Kwa namna Abdi Banda na Salim Mbonde walivyocheza katika beki ya kati wakati Stars ilipocheza na Lesotho katika mchezo wa kwanza kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON 2019 ni wazi kocha, Mayanga anapaswa kutazama tena uamuzi wake wa kumuacha kikosini, Yondan na kutomtumia mlinzi mwenye uzoefu, Erasto Nyoni katika mchezo wa Jumamosi iliyopita.

Timu ya taifa ni mkusanyiko wa wachezaji bora

Kwa wakati ambao kocha yoyote huteua kikosi cha timu ya Taifa, wachezaji waliofanya vizuri katika klabu zao hupewa nafasi kisha kocha hufanya kazi yake ya kukisuka kikosi kimbinu na kiufundi.

Uteuzi wa kwanza wa Mayanga mwezi April wakati Stars ilipocheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Botswana na Burundi ulikuwa mzuri. Na kikosi alichokiteua sasa si kibaya lakini ukitazama kwa umakini unaweza kuona ni kama kocha huyo ameamua kumaliza nyakati za baadhi ya wachezaji kuichezea Stars licha ya kwamba wanaweza kutoa mchango mkubwa kuliko waliopo sasa.

Kumekuwa na ‘ukiritimba’ mkubwa katika uteuzi wa timu ya Taifa. Kumjumuisha kikosini mshambulizi, Thomas Ulimwengu ulikuwa ni uamuzi mzuri kwa sababu niliamini, Mayanga amefanya hivyo ili kutaka kujua maendeleo ya mchezaji huyo wa zamani wa TP Mazembe hasa ukizingatia Stars itakuwa na michezo mingine dhidi ya Uganda na Cape Verde.

Lakini kitendo cha kumuanzisha na kumpa nafasi ya kucheza kwa zaidi ya saa moja vs Lesotho yalikuwa ni makosa makubwa kwa sababu, Ulimwengu hajacheza mchezo wowote wa ushindani tangu alipoichezea Mazembe vs Yanga SC katikati ya mwaka uliopita.

Mayanga hawezi kukwepa lawama katika hili. Ulimwengu hakucheza katika michezo miwili ya mwanzo ya Mayanga kama kocha wa Stars na hilo lilitoa nafasi kwa Ibrahim Ajib kuanza na nahodha, Mbwana Samatta katika safu ya mashambulizi.

Kuwapanga Samatta na Ulimwengu katika mfumo wa 4-4-2 haukuwa uamuzi sahihi na haupaswi kutumiwa tena. Pia kumpanga Samatta kama mshambulizi wa kwanza katika mfumo wa 4-3-3 pia si sahihi ingawa amekuwa akipangwa mara kadhaa katika nafasi hiyo akiichezea klabu yake ya KRC Genk.

Samatta ana uwezo wa kumalizia mashambulizi, na anaweza kupambana na mabeki wa kati katika mipira ya juu lakini kuendelea kumfanyisha kazi hiyo kwa dakika 90 akiwa Stars inamaanisha kupoteza uwezo wake usio wa kawaida.

Samatta ni namba 10

Hata kama Stars inakabiliwa na mapungufu katika utengenezaji wa nafasi na upigaji wa pasi za mwisho, Samatta anaweza kupewa mpira na yeye akajua cha kufanya ili timu ipate matokeo. Mayanga amepata bahati ya kufanya kazi na ‘mvumbuzi mkubwa’ wa mambo katika timu yake.

Samatta ana uwezo wa kuzunguka nusu ya uwanja na ‘kutumbukia’ katika sehemu ambazo mabeki hawatarajii uwepo wake huku akifanya kazi ya kuichezesha na kuikimbiza timu, huku akipachika magoli kwa mashuti yake ya mbali.

Huyu si tu ndiye mchezaji mbunifu zaidi katika kikosi cha Stars bali ndiye mchezaji ‘mzalendo’ anayejituma zaidi. Ili kunufaika naye na kupata mchango wake mkubwa kwa timu, Mayanga anapaswa kumpa uhuru Samatta acheze anavyotaka.

Kumpanga namba 9 ni kumnyima nafasi ya kufurahia mchezo na kumpanga namba kumi itakuwa ni sawa na kumfanya awe huru kucheza na hilo litaisaidia sana Stars. Mayaoga anapaswa kuanza kufikiria namba bora ya Samatta anapokuwa uwanjani na asijaribu kumuweka katika mfumo utakaomnyima uhuru.

Itakuwa vyema sana kama mifumo ya kiuchezaji ya Mayanga itamwachaitamwacha Samatta afanye chochote anachoweza kufanya akiwa uwanjani.

Tatizo la beki ya kati

Shomari Kapombe na Gadiel Michael walicheza mchezo wa nguvu na kusaidia kupeleka mashambulizi mbele kadri ilivyowezekana wakitokea katika beki za pembeni lakini kwa Banda na ‘patna’ wake Mbonde mambo yalikuwa tofauti sana kwa sababu walinzi hao wa kati walishindwa kumdhibiti mfungaji wa goli la kusawazisha la Lesotho kwa sababu tu ya ‘uvivu’

Walinzi hao walikabia macho kuanzia krosi inapigwa kutokea upande wa kulia wa Stars na kumuacha mfungaji akiwa huru japo kulikuwa na wachezaji watatu wa Stars karibu yake. Ili kucheza vizuri vs Uganda ambao waliishinda 1-0 Cape Verde siku ya Jumapili, Mayanga anapaswa kubadili mfumo wake na huu ni wakati wa kutumia mfumo tofauti ili kupata uimara zaidi katika ngome.

Banda na Mbonde hawawezi kucheza pamoja kwa sababu stahili yao ya uchezaji inafanana na hakuna anayeweza kumtuma mwenzake. Nakumbuka mika ya Mbrazil,Marcio Maximo kocha huyo alitamani sana kuona Victor Costa na Hamis Yusuph wakicheza pamoja lakini wawili hao walishindwa kutoa matunda mazuri kila walipopangwa pamoja katika beki ya kati kwa sababu wote walikuwa wakicheza stahili moja.

Ili kuleta balansi katika timu ni lazima uimara uwe kila idara, katika golikipa Aishi Manula yuko vizuri na alijitolea sana vs Lesotho na kuisaidia Stars isiangushe pointi zote nyumbani. Mayanga anapaswa kutazama upya uwezo wa Kelvin na kumuamini Erasto vinginevyo atapigwa nyingi Namboole Stadium atakapoenda kuivaa Uganga inayoshambulia sana.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here