Home Kitaifa Kama ilikupita Ngumu Kumeza ya Sports Extra June 9, 2017

Kama ilikupita Ngumu Kumeza ya Sports Extra June 9, 2017

9372
0
SHARE

Safari ya kwenda Gabon haikuwa rahisi jamani, huenda wale vijana waliyaona aliyoyaona Sinbad kwenye safari zake saba. Waliondoka waliondoka wakiwa na umri mdogo lakini ila wamerejea wakiwa na umri wa wahenga kutokana na kutumikishwa na kwa faida za siasa za mpira .

Timu ilianza kugawanywa hapahapa tangu safari ya kufuzu, ukolono ulitumika kugawanya ili uweze kuwatawala ilitumiwa vizuri sana dhana hiyo na uongozi wa TFF, na hiyo sumu uliwalevya mpaka wachezaji na ndyo maana wakasahau ile silaha kubwa kuliko zote duniani ‘umoja ni nguvu’ ndani ya Serengeti kulikuwa na timu mbili halafu bado tuliamini mtafikia malengo. Hivi kwa mpasuko ule halafu tupate mafanikio kweli?

Team Kim ambayo ilikuwa inaongozwa na Rais wa Shirikisho, alifanya hivyo ili kujivua gamba na kuvaa gwanda si unakumbuka alivyomfukuza Kim enzi zile bila kufikiria, lakini pia kulikuwa na team Shime ambayo iliponzwa na fikra nyeusi. Wao hata kama wangefanya zuri, lilifichwa na rangi ragi yao. Si unajua sifa moja wapo ya giza ni weusi usiong’ara na ndio maana hata mchimbaji mdogo wa Nyamongo hana thamani sawa na mchimbaji mdogo wa toka nje ya bara la watu weusi hata mitaji ikiwa sawa.

Kuna wachezaji wametengenezewa mazingira ya kuchagua upande na hata hilo ni moja ya mambo yaliyoiathiri timu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo. Mchezo wa kwanza Kim na Shime walipishana juu ya wachezaji Shabani Zuberi na Mohamed Rashid, Kim akitaka waanze ilhali wanamajeruhi huku Shime akitaka wasicheze kitu kilichosababisha timu kushindwa kufanya mabadiliko ya kiufundi badala yake ikafanya kuwatoa wagonjwa.

Alisikika mjumbe mmoja anasema, kama Shime hatotoka Stars akaenda na Serengeti Boys mi Gabon siendi, ndiyo maamuzi yakachukuliwa vinginevyo ‘Mchawi mweusi’ sfari ya Gabon angekuwa sehemu ya hadhira.

Pamoja na maandalizi ya muda mrefu bado timu iliamini kwenye ushirikina, timu haikuwa na mganga India wala kwingineko, naambiwa tangu awali timu ilianza na Mungu wengi tuliamini safari yetu itaendelea hivyo lakini lakini kuanzia kwenye mchezo dhidi ya Congo waumini wa ushirikina walimleta mganga na kwakweli tulianza kushinda kwa taabu tofauti na kabla hatujaanza kuroga ambapo tulikuwa tunashinda kirahisi.

Siku moja kabla ya mchezo wa mwisho wa makundi mtaalamu wa psychology anarudishwa nyumbani kama sehemu ya kubana matumizi, mdomo wangu ulikuwa wazi unaweza kuhisi mamba anaota jua yote ilikuwa mshangao.

Hivi ni bajeti gani mlikuwa mnabana wakati watanzania walikuwa wanachanga au lengo lilikuwa kubaki na chenchi, bajeti ya mtu wa saikolojia haipo eti tuliweka kwenye maandalizi tu ila ya mganga na masuala ya ushirikina ipo. Kwa joto la jiwe kuelekea mchezo wa mwisho dhidi ya Niger tulimuhitaji mtaalamu wa saikolojia kuliko mganga wala mchawi, wachezaji walipaswa kupunguziwa mzigo wa fikra na sio kutwishwa mzigo wa hirizi.

Mtu mmoja anasema hata mkuu alisikika akisema, wakati huu tunahitaji kuongeza wataalam kuliko wakati mwingine wowote. Wakati watu muhimu wanarudishwa nyumbani, washauri wa rais walibaki kutumbua fedha za wavuja jasho wa Tanzania nchini Gabon. Nikakumbuka shairi la Mohamed Seif Khatib ‘Wenye navyo watubana.’

Mnadanganya pesa pesa za watanzania zimetupeleka kambi Morocco, mnakosea kule kila kitu kiligharamiwa na shirikisho la soka la Morocco. Muda wote wa kambi ya kule wachezaji waliwahi kupewa dola 100 tu kwa safari nzima na kambi ya siku saba timu ilipokaa Cameroon iligharamiwa na wenyeji. TFF iligharamia siku tatu za nyongeza za kukaa Cameroon kuanzia Mei 11 timu ianza kugharamiwa na CAF kwa wachezaji 21 na viongozi saba.

Timu yetu ilikwenda na wachezaji 23 hivyo wawili ndio walikuwa wanagharamiwa na TFF, inamaana matumizi ya wachezaji wawili yalikuwa makubwa kuliko kuwalea wale mapacha wawili wa Rais? Natanika na pacha wake Natandua.

Hamasa bila taratibu za kisayansi ziliiua Serengeti Boys, unajua tulilazimisha kucheza michezo mingi kwa muda mfupi kitu kilichosababisha wachezaji kuchoka kabla ya mashindano na wengine kupata majeraha. Michuano inaanza Rais wa TFF anakwenda Gabon, wachezaji wakamtolea uvivu wanataka walipwe malimbikizo ya madeni yao yote, Rais aliahidi baada ya michuano.

Na kuanzia Mei 11 wachezaji walianza kupikea posho ya dola 20 sawa na 44,000 ya kitanzania ambayo walilipwa mpaka tarehe 21 siku waliyotolewa na Niger, najiuliza kwa nini bajeti ya timu iliishia kwenye makundi au inamaana hakuna kiongozi aliyeamini tutavuka kwenye makundi ndio maana posho ya bajeti ya timu iliishia hapo?

Pamoja na timu kurejea tarehe 26 lakini siku tano kati ya tarehe 21 mpaka 26 hakuna mchezaji aliyepewa posho, timu inarudi Tanzania kambi inavunjwa kwa wachezaji kupewa 20,000 kwa wale wanaoishi Dar, 30,000 kwa wa Morogoro huku wale wa Mwanza wanapewa nauli ya 45,000 bila kupewa malimbikizo ya madeni yao.

Wachezaji wanarudi majumbani mwao wakiwa na masikitiko makubwa, mifukoni jua kali ndiyo maana wengi wao leo wanacheza mechi za vichochoroni, wakati wakiwa kambini walikuwa wanachugua viwanja hata vya kufanyia mazoezi.

Yule mchezaji ambaye alirudishwa kwa kuumia kwenye mashindano Ally Makamba yupo kwao Dodoma ametelekezwa na timu hapewi matibabu yoyote, wachezaji wenzie wa Serengeti Boys wameanzisha harambee maalum ya kumchangia mwenzao japo hata wao hali zao sio njema.

Jamani eeh kwa anayejua namba ya huyu Abdallah Hashim basi aiweke hewani watanzania waanze kumchangia, kama tuliichangia Serengeti Boys wakati ule tutashindwa kumsaidia akiwa pekeake?

Kiufupi wachezaji wa Serengeti Boys hawajafaidika na michango ya wasakatonge wa Tanzania bali pesa ile imewasaidia zaidi wajumbe wa kamati kupishana angani kama watumishi wa serikali wa awamu iliyopita, maana walikuwa hawatulii kama vile kuku anaetaka kutaga mara siku moja mjumbe yupo Rabat siku mbli yupo Tanzania siku ya tatu kaenda Yaund Yaunde.

Watanzania tunapenda maigizo hilo alilithibitisha kiongozi wa msafara ‘mzee wa kuzimia’ aliyafuga machozi, hakulia pale tulipotolewa uwanjani eti kaja kulia alipomulikwa na camera za nyumbani jamani tuacheni masuala ya Kaole kwenye mpira.

Kamati kwa kushirikiana na TFF watanzania wanataka muweke wazi mapato na matumizi ya michuano yote, TFF ituambie ile dola 60,000 ya Serengeti kumaliza nafasi ya tatu kwenye kundi imeshatolewa na CAF au mshaibadilishia matumizi itumike kwenye uchaguzi.

Tahadhari kambi ya wachezaji waliopo Mwanza iangaliwe mara mbili kutokana na michuano ambayo tumetoka kupata somo, hivyo basi tuangalie namna ya kuwaandaa watoto bila kuwadhulumu kuelekea michuano ya mwaka 2019 ambayo sisi ndio wenyeji.

Najua baada ya kuweka uchafu huu hadharani, baadhi ya viongozi wa mpira wanatukana huko ila hivyo ndiyo ndoto ya Gabon mpaka kombe la Dunia ilivyoyeyuka na sasa yamebaki mashimo ya madeni kwenye nyongo za wahusika.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here