Home Kitaifa ‘Simba inapaswa kuachana na Omog na kumtazama mkali huyu wa mbinu’

‘Simba inapaswa kuachana na Omog na kumtazama mkali huyu wa mbinu’

30669
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

NAAMINI moja kati ya mabadiliko muhimu katika kikosi cha Simba SC ni kuachana na kocha wake Mcameroon, Joseph Omog.

Licha ya kuisaidia Simba kushida ubingwa wa kombe la FA na kushindwa kwa tofauti ya magoli na mabingwa Yanga SC katika ligi kuu Tanzania Bara 2016/17, makosa binafsi ya Omog yaliigharimu sana timu hiyo na yalikaribia kuwaangusha katika fainali ya FA vs Mbao FC.

Omog inawezekana alifanikiwa kama kocha wakati alipoisaidia AFC Leopard ya Congo Brazaville kushinda ubingwa wa Caf Confederation Cup 2012, na akashinda ubingwa wa VPL 2013/14 akiwa kocha wa Azam FC, lakini Mcameroon huyo ameonyesha wazi udhaifu wa kimbinu huku suala la ufundi likinipa shaka mara kwa mara.

Kupoteza uongozi wa 2-0 walioupata Azam FC vs El Merreikh ya Sudan katika uwanja wa Azam Complex kisha kuondolewa katika Caf Champions League kwa jumla ya magoli 3-2 baada ya pambano la marejeano jijini, Khartoon Machi, 2015 nitaendelea kuamini kulisababishwa na mabadiliko ya kocha huyo ambaye alimtoa mshambulizi Kipre Tchetche katika kipindi cha pili.

Kipre aliwamiliki walinzi wa El Merreikh ambao waliogopa kusogea mbele wakimuhofu Muivory Coast huyo ambaye alipotolewa Azam FC wakapigwa presha kisha wakapoteza mwelekeo na kuchapwa 3-0 na kuondolewa katika michuano.

Mapambano matatu vs Hans, Lwandamina 

Ndiyo, Simba haikupoteza mchezo wowote dhidi ya ‘watani’ wao wa jadi Yanga katika michezo miwili waliyokutana katika ligi kuu na mmoja wa Mapinduzi Cup 2017  lakini kuna sababu kadhaa za kimsingi zinazonifanya niamini kocha huyo hana uwezo wa kuifanya Simba ipate ubingwa wa VPL na kuleta changamoto katika michuano ya Caf Confederation Cup mwaka ujao.

Mfano, katika mchezo wa Oktoba Mosi, 2016 ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana 1-1 vs Yanga. Watu wanaweza kuendelea kumlaumu aliyekuwa mwamuzi wa mchezo huo Martin Saanya lakini kwa namna Simba ilivyocheza katika eneo la ulinzi na jinsi walivyopanga mashambulizi ni wazi hawakuwa bora kuliko Yanga.

Upangaji mbovu wa kikosi 

Kuwaacha nje ya kikosi walinzi kama Abdi Banda, Mganda, Juuko Murishid na kumuanzisha Novaty Lufunga lilikuwa ni kosa la kiufundi na liliwagharimu.

Kilichowanusuru Simba na kichapo ni kuwahi kuchoka kwa viungo wa kati wa Yanga lakini bado mbinu zao ndogo zilishindwa kuwapatia nafasi ya kutengeneza magoli na wakasubiri hadi dakika tatu za mwisho kusawazisha kwa mpira wa kona ya moja kwa moja iliyopigwa na Shiza Kichuya.

Kikosi cha Mholland, Hans van der Pluijm kilikuwa katika uchovu baada ya kucheza mfululizo kwa miezi zaidi ya 24 (kuanzia Kagame Cup, Julai, 2015 hadi Makundi Caf Confederation Cup , Septemba, 2016.) Hivyo wachezaji wake wengi walikuwa wakicheza huku wamechoka.

Mashabiki wa Simba waling’oa viti wakati ule na kusahau mapungufu muhimu katika timu yao. Waliamini wana timu iliyokamilika. Game ya nusu fainali Mapinduzi Cup 2017 ilimalizika kwa suluhu-tasa.

Yanga ilikuwa chini ya Mzambia, George Lwandamina tena akiwa ndani ya mwezi wake wa kwanza tangu alipopewa kibarua kilichokuwa kimeachwa na Hans.

Lwandamina hakuwa na kikosi imara kutokana na wachezaji wake wengi kuwa na majeraha lakini aliweza kumtoa jasho Omog na kustahimili pambano ambalo wengi waliamiani Simba ingeshinda rundo la magoli hasa ukizingatia Yanga ilikuwa imetoka kuchapwa 4-0 na Azam FC siku mbili nyuma.

Ushindi wa Mbinde 2-1 Februari, 2017 dhidi ya mahasimu  wao Yanga bado hauwezi kuficha madhaifu ya kocha Omog. Yanga haikuwa na makali lakini walimudu pambano kwa robo tatu ya mchezo.

Makosa yaleyale aliyofanya Omog katika mchezo wa mzunguzo wa kwanza akayarudia tena. Licha ya kucheza kwa dakika zaidi ya 50, Lufunga alionekana wazi kwenye nafasi ya beki wa kati hucheza akiwa na mashaka makubwa.

Lufunga si mzuri katika kucheza ‘tackle’ na anapojaribu kufanya hivyo hucheza faulo. Kasi yake pia ya kukimbia si nzuri ndiyo maana alionekana ‘kumilikiwa’ na Mzambia, Obrey Chirwa. Wakati mechi ikiendelea, Omog akamtoa Lufunga nafasi yake ikachukuliwa na kiungo wa kati nahodha wa timu, Jonas Mkude.

Mcongoman Besala Bokungu akaenda kucheza kati na Banda yalikuwa ni mabadiliko mazuri hasa ukizingatia Lufunga alikuwa na kadi ya njano. Kutokana na kiwango bora kabisa cha Muzamiru Yassin alichokionyesha kabla ya mchezo huo vs Yanga, uamuzi wa Omog kumpeleka Muzamiru katika beki namba 2 ulikuwa ni wa ajabu sana kwa maana aliwaacha Mghana, James Kotei na Mkude katika dimba la kati.

Viungo hao wawili si watengenezaji wa nafasi za kufunga. Kama ni ‘bahati’ basi ilikuwa kwa Omog ila mabadiliko yake ya kumtoa Lufunga na kumpa nafasi Mkude yalipaswa kumbakisha Muzamiru katika eneo la kiungo na si kumpeleka katika beki ya kulia.

Omog alinufaika sana na mbinu ya kushambulia pembeni, lakini mabadiliko yake ya kiufundi mara kwa mara yamekuwa si sahihi. Kwa namna walivyokuwa kikosi cha Omog kisingeweza kufunga magoli mengi kwa sababu alishindwa kutengeneza safu ya kwanza na ile ya pili ya washambuliaji kati ya Ibrahim Ajib, Mrundi, Mavugo, Muivory Coast, Blagnon na Juma Liuzio.

Vs Mbao FC

Kwenye mchezo wa fainali ya FA Cup, Omog aliamtumia Kotei na Mganda, Juuko Murshid katika beki ya kati. Jambo hilo liliwafanya Simba kuwa na nguvu ya ziada na ufundi katika safu yake ya ulinzi.

Mbinu hiyo ya kiufundi iliweza kuleta matunda kwa sababu mwisho wa dakika 90′, Omog aliweza kupata matokeo aliyostahili-kikosi chake kutoruhusu goli. Kotei aliweza kuwaonyesha watazamaji ni jinsi alivyokuwa bora katika beki ya kati, huku akiwa kiunganishi kizuri cha safu ya ulinzi na kuwa msaada mkubwa katika ngome ya mabeki wanne.

Lakini kama kocha angekuwa amejipanga vyema angempanga Kotei katika eneo la kiungo na kumpa nafasi Abdi Banda kucheza na Juuko katika beki ya kati kwa sababu kujipanga vyema katika safu ya ulinzi ni vizuri zaidi kama timu itamtumia Kotei kwenye sehemu ya kiungo kama kweli Omog alitaka kuona timu yake ikienda mbele kushambulia, na hili litamfanya Mkude kupoteza nafasi yake kikosini.

Kwa mechi kama ile ya fainali ambayo timu inahitaji kufunga japo goli moja, Kotei angeweza kuipatia Simba nguvu kubwa ya kushambulia ikianzia kwenye idara ya kiungo. Omog alishindwa kimbinu na kocha wa Mbao, Mrundi, Ettiene Ndayiragije.

Lakini kama kocha angekuwa amejipanga vyema angempanga Kotei katika eneo la kiungo na kumpa nafasi Abdi Banda kucheza na Juuko katika beki ya kati kwa sababu kujipanga vyema katika safu ya ulinzi ni vizuri zaidi kama timu itamtumia Kotei kwenye sehemu ya kiungo kama kweli Omog alitaka kuona timu yake ikienda mbele kushambulia, na hili litamfanya Mkude kupoteza nafasi yake kikosini.

Kocha huyo wa Mbao aliingiza timu yake kuanza mchezo kwa stahili ya kujilinda huku wakishambulia kwa kustukiza. Aliwapanga walinzi wanne, viungo watano na kumuacha mshambulizi mmoja mbele.

Omog ambaye aliwapanga washambuliaji watatu mbele, viungo watatu na walinzi wanne alishuhudia timu yake ikimiliki mpira kwa kiasi kikubwa lakini hawakuwa na mbinu za kupeleka mipira sahihi kwa washambuliaji.

Mbao walikuwa wagumu katikati ya uwanja na ili Simba ipitishe mipira walimuhitaji kiungo kama Kotei ambaye ni mchangamfu, mwenye ubunifu na pasi za uhakika. Mkude ni mzuri lakini stahili yake ya uchezaji inachelewesha sana ushindi huku akihatarisha usalama wa timu yake kutokana na upigaji wake wa ‘pasi mkaa.’

Ettiene alipogundua Simba haina makali akawaruhusu wachezaji wake kushambulia mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili. Jambo hilo liliwafanya Simba kuwa katika presha. Kilichowaangusha Mbao ni kutokuwa na wachezaji wengi wenye maarifa binafsi. Ettiene ameijenga timu yake kucheza kitimu huku ikiongozwa na mbinu zake ndiyo maana walipoona zimesalia dakika 15 kabla ya kumalizika kwa dakika 90′ akairudisha timu yake kucheza mchezo wa kujilinda kwa tahadhari ya hali ya juu.

Akafanikiwa kumaliza dakika 90 kwa suluhu-tasa. Alikuwa makini pia katika ufanyaji wake wa mabadiliko na hakupoteza heshima kwa wapinzani licha ya kuonekana kuwamudu.

Blagnon alipofunga goli la uongozi upande wa Simba dakika ya 109′, Etienne akaamua kuwapa uhuru wachezaji wake kushambulia na baada ya kusawazisha goli hilo wakarudi kujilinda kwa lengo la kuivusha mechi hadi katika hatua ya mikwaju ya penalti.

Kama kocha huyo wa Mbao FC angekuwa na kikosi chenye ubora mpana angefanikiwa zaidi lakini Omog ameendelea kudhihirisha si kocha mwenye mbinu bora zaidi hasa katika michezo muhimu.

Nadhani Simba inahitaji nyongeza ya wachezaji lakini kabla  inapaswa kumuondoa Omog na kumpa kazi mmoja kati ya makocha Mecky Mexime ama Etienne ili kuungana na Mganda, Jaclson Mayanja makocha ambao wana mbinu na ufundi huku vikosi vyao vikicheza vile wanavyotaka.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here