Home Kitaifa ‘Bora niondoke kuliko kutolewa kwa mkopo’ – Juma Mahadhi

‘Bora niondoke kuliko kutolewa kwa mkopo’ – Juma Mahadhi

13728
0
SHARE

Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Yanga Juma Mahadhi amesema, hayuko tayari kutolewa kwa mkopo kwenda timu nyingine, kama itatokea klabu yake inataka kumtoa kwa mkopo ataomba imuache ili akatafute maisha sehemu nyingine.

Hiyo inatokana na tetesi ambazo zimekuwa zikienea kwamba, klabu ya Yanga huenda ikamtoa nyota huyo kwa mkopo kwenda klabu ya Singida United ambayo imepanda kucheza ligi kuu Tanzania bara msimu ujao.

“Sipo tayari kutolewa kwa mkopo, kama itatokea hivyo nitaomba waniache niende kutafuta maisha sehemu nyingine. Mimi sijui lolote kuhusu hilo, klabu yangu haijaniambia chochote na kama wataniambia, msimamo wangu ndio huo,” amesema Juma Mahadhi alipozungumza na Sports Extra.

Mahadhi pia amesema alitamani kucheza mechi nyingi katika klabu yake lakini imekuwa tofauti na mipango pamoja na matarajio yake.

“Nilijipanga nicheze mechi nyingi na kuisaidia klabu yangu zaidi ya hapo lakini malengo yangu hayakutimia. Kulikuwa na ushindani mkubwa kwenye kikosi na kila mchezaji aliyepata nafasi alitaka kuonesha anapaswa kucheza kila mechi.”

“Najipanga kwa ajili ya kufanya vizuri katika msimu ujao ili nipate nafasi ya kucheza mechi nyingi tofauti na msimu huu.”

Kuhusu klabu ambazo zinahitaji huduma yake kwa ajili ya msimu ujao Mahadhi amesema zipo klabu kadhaa za ndani na nje lakini kwa sasa hawezi kuzitaja kwa sababu bado yupo ndani ya mkataba na Yanga.

“Nimepokea ofa kutoka vilabu mbalimbali ndani na nje ya nchi, kwa sasa siwezi kuzungumzia lolote kwa sababu nipo ndani ya mkataba. Waende wakaonane na manager wangu na viongozi wa klabu wakikubaliana nitafanya maamuzi kwa sababu mpira ni kazi yangu.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here