Home Kitaifa Jicho la 3: Manji amekuwa ‘mwanasoka mshindi’, ameiacha Yanga katika uelekeo

Jicho la 3: Manji amekuwa ‘mwanasoka mshindi’, ameiacha Yanga katika uelekeo

11277
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

‘TANGAZO la ghafla’ la kujiuzulu kwa mfanyabiashara Yusuf Manji katika nafasi yake ya uenyekiti klabuni Yanga huenda likaichanganya klabu hiyo bingwa mara 27 katika ligi kuu Tanzania Bara, lakini kwa ‘Jicho langu la 3’ naona mafanikio zaidi yanakuja ndani ya klabu.

Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Manji kwa kila alichoifainyia Yanga ndani ya misimu mitano aliyoisimamia klabu hiyo na kuiongoza kama mwenyekiti. Amejiuluzu kwa kile alichosema ni ‘sababu za kiafya.’

Manji amefanikiwa

Mara baada ya wanachama wa Yanga SC kushuhudia klabu yao ikichapwa 5-0 na mahasimu wao Simba, Mei, 2012 huku timu ikimaliza katika nafasi ya tatu katika ligi kuu Bara nyuma ya Simba na Azam FC wengi wao walihitaji kuona aliyekuwa mwenyekiti wa klabu wakili Lyod Nchunga akijiuzulu.

Hilo lilifanikiwa licha ya Nchunga awali kusema hawezi kuachia madaraka  ndani ya miaka miwili  tangu alipochaguliwa katika mkutano mkuu wa uchaguzi katikati ya mwaka 2010-shinikizo lilikuwa kubwa sana kwa utawala wake na atimaye aliamua kukaa pembeni baada ya wajumbe wa Kamati ya utendaji kuamua kujiuzulu.

Kujiuzulu huko kwa Nchunga kulifungua milango ya Manji kuingia klabuni hapo baada ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa dharura Julai, 2012. Nakumbuka msimu wa mwisho wa Nchunga kama mwenyekiti wa Yanga, wachezaji walikuwa katika kipindi kigumu sana. Walicheleweshewa mishahara yao mara kwa mara huku malipo ya posho zao yakiwa tatizo pia. Hilo lilichangia kwa kiasi kikubwa klabu kuyumba huku timu ikishindwa kuwa imara ndani ya uwanja.

Wachezaji mastaa wa timu hiyo kama Haruna Niyonzima ilidaiwa walikuwa karibu kutua Simba baada ya hali ya kiuchumi klabuni hapo kuwa si nzuri lakini kitendo cha Manji kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti kilibadilisha upepo na nyota wengi wa Afrika Mashariki walitaka kujiunga na klabu hiyo.

Kelvin Yondani alijhiunga Yanga akitokea Simba baada ya kupewa zaidi ya milioni 30-cash, Mnyarwanda,Mbuyu Twite alisajiliwa kwa zaidi ya milioni  60 akitokea APR ya Rwanda licha ya awali kuonekana mlinzi huyo ‘kiraka’ angejiunga Simba. Huo ulikuwa ni mwanzo tu wa harakati za Manji kama mwenyekiti wa klabu hiyo ambayo alianza kuifadhili miaka takribani 12 iliyopita.

Misimu mitano sasa Manji anang’atuka Yanga akiwa ameisaidia klabu kutawala soka la Tanzania. Ameshinda mataji manne ya ligi kuu,  mawili ya Ngao ya Jamii, moja la klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati, moja la FA Cup huku akiiwezesha timu hiyo kufika hatua ya makundi katika michuano ya Caf Confederation Cup 2016.

Kwa kiongozi yoyote haya ni mafanikio makubwa hasa ukizingatia yamepatikana ndani ya miaka mitano tu. Yanga wana kila sababu ya kumshukuru Manji kwa sababu amewasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ‘uhai’ wa klabu na historia yao ‘isiyoshindika.’

Mishahara ya juu 

Katika soka la kisasa si rahisi klabu kufanikiwa ikiwa wachezaji hawalipwi vizuri. Na licha ya kutokuwa na ufahamu mkubwa katika mambo ya soka wakati anaingia madarakani Julai, 2012, Manji alidhamilia kuifanya Yanga kutawala soka la ndani na kupiga hatua Kimataifa.

Hili afanikiwe kuhusu hilo aliamua kuwapa uhuru makocha na watendaji wa klabu kuwasaini wachezaji bora na hakusita kukubali kuwalipa mishahara mikubwa. Hii imewasaidia kwa kiasi kikubwa wachezaji kuimarisha maisha yao huku wakitoa mchango mkubwa kwa timu ndani ya uwanja.

Haruna Niyonzima, Kelvin, Mbuyu Twite ni baadhi ya wachezaji wa mwanzo wa Yanga kulipwa mishahara minono na sasa mishahara ya nyota kama Mtogo, Vicent Bossou, Mzambia, Obrey Chirwa,Wazimbabwe, Donald Ngoma na Thaban Kamusoko inaisimamisha klabu juu katika ulipaji wa mishahara ya wachezaji.

Wakati nyota hao wa kigeni wakilipwa zaidi ya milioni 7 kila mmoja kuna rundo la wachezaji wazawa pia wamekuwa wakilipwa mishahara mizuri. Ulipaji huu wa mishahara umeifanya klabu kuwa imara katika soka la ndani na hili nampongeza sana Manji kwa kuleta mapinduzi ya kweli katika soka la Tanzania.

Katikati ya mwaka 2008, Manji akiwa mfadhili tu wa klabu alisaidia usajili wa mlinda mlango Juma Kaseja kutoka Simba na kujiunga Yanga. Usajili wa Kaseja ulifungua ‘kufuri’ la wachezaji wa Kitanzania ambao awali walikuwa wakisajiliwa chini ya milioni 15.

Kaseja alisaini Yanga kwa zaidi ya milioni 35 mwaka 2008 na alikuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya VPL kulipwa mshahara wa milioni moja. Haya ni sehemu ya mapnduzi ya kweli ambayo Manji aliyaleta katika soka la Tanzania na ningependa kumpongeza kwa kila alichofanya kwa vijana wengi wa kiafrika-kuwapa maisha ya kukidhi mahitaji yako.

Alikubali kujifunza

Ndani ya miezi yake mitatu ya kwanza ya uongozi kama mwenyekiti wa Yanga, Manji aliwaajiri makocha wawili. Mbelgiji, Tom Saintfiet na Mholland, Ernie Brandts na hadi anatangaza kujiuzulu nafasi yake Jumanne hii, Manji alifanya kazi na makocha watano tofauti huku Mholland, Han van der Pluijm akifanya naye kazi kwa vipindi viwili tofauti.

Wengine ni Mbrazil, Marcio Maximo ambaye alifanya kazi kwa miezi isiyozidi sita tu klabuni hapo. Kufanya kazi na makocha watano ndani ya miaka mitano  ndani ya uongozi wake sitazami kama sababu ya kumlamu Manji bali kuna wakati alilazimika kufanya hivyo ili klabu ifanikiwe ndani ya uwanja.

Alimfukuza kazi Tom kwa sababu tu aliambiwa ‘yeye si mfanyabiashara wa kimataifa’, aliwaondoa Brandts na Maximo kwa sababu tu walipoteza michezo ya ‘Nani Mtani Jembe’ dhidi ya Simba, lakini  namna alivyofanya kazi na Hans misimu  miwili ya mwisho  ni wazi alionekana kujifunza mengi na bila shaka ‘ Manji alikuwa mwanafunzi mzuri’ ambaye alijitahidi kusahihisha makosa yake kila alipokuwa akisonga mbele.

Yanga itaendelea kusimama?

Miezi kadhaa iliyopita baada ya taarifa za kujiuzulu kwa Manji zilipotoka wanachama wa klabu hiyo walionekana kuchanganyikiwa sana na walimlaumu Mzee Akilimani na baraza lake la Wazee wa klabu . mzee Akilimali alipinga mpango wa Manji kutaka kuikodisha klabu hiyo kwa miaka kumi na kuwa ‘Yanga Yetu.’

Upande wangu niliwaunga mkono Wazee hao na nakumbuka niliandika makala ( humu www.shaffihdauda.co.tz) iliyokuwa na kichwa cha habari, ‘ YANGA INAWEZA KUISHI BILA MANJI ILA WATAMKUMBUKA, MANJI HAWEZI KUISHI BILA YANGA, ATAIKUMBUKA…’

Huo ndiyo ukweli na wana Yanga hawapaswi kusikitika hivi sasa zaidi ya kutafuta namna nyingine ya kuendelea kuishi, kuwalipa vizuri wachezaji wao na kuisapoti klabu. Jambo la muhimu na la haraka ni klabu kwenda kwenye uchaguzi mdogo na katika hili kaimu mwenyekiti wa klabu, Clement Sanga ni kuhitisha uchaguzi wa haraka wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Manji.

Huu ni wakati ambnao Yanga inapaswa kuwasaini wachezaji wake bora wanaomaliza mikataba na wale wapya ambao watapendekezwa na kocha Mzambia, George Lwandamina hivyo kwa namna yoyote ile wanapaswa kufanya uchaguzi haraka ndani ya miezi minne kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

Yanga inaweza kuishi bila Manji ikiwa tu uongozi wa sasa utaendelea kutafuta wadhamini zaidi. Si lazima wapate mdhamini mwenye uwezo wa kuwapa bilioni moja kwa mwaka,  hapana ili klabu ifanikiwe wakubali kuwafungulia milango wadhamini wengine wenye kipato  cha kati ambao wanaweza kuwapa hata milioni 500 kwa mwaka.

Kuwa na wadhamini wane wenye uwezo wa kuipa klabu walau milioni 500 kwa mwaka itamaanisha Yanga kuingiza bilioni 2 kwa mwaka na hilo linawezekana kama uongozi utaamua kuimarisha idara yake ya masoko na kuwapa nafasi wadhamini wadogo wadogo.

Yanga itamkumbuka Manji kwa mambo mengi kwa maana chini yake klabu ilikuwa ikifanya maandalizi ya uhakika kabla ya msimu, aliisafirisha timu kwa lengo la kujifunza mara kadhaa barani ulaya. Hakika Manji ni ‘mtu wa Yanga’ hasa na uamuzi wake wa kujiuzulu umekuja wakati mwafaka sana.

Amejiuzulu wakati mwafaka

Ingekuwaje endapo Manji angejiuzulu wakati timu ikiendelea kugombea ubingwa wa ligi kuu? Bila shaka ingekuwa tatizo ambalo lingewaathiri  sana wachezaji na kuathiri utendaji wao kama timu ndani ya uwanja.

Kila mwana Yanga anafahamu ni kiasi gani Manji anapitia nyakati ngumu katika maisha yake binafsi lakini kuendelea kubaki  na klabu hadi mwisho wa msimu  ni jambo la kufurahisha sana na kumshukuru pia. Manji amekuwa ‘mwanasoka mshindi’ na ameiacha Yanga katika uelekeo sahihi. Sasa ni wakati wa wanachama kuchagua mtu sahihi wa kushika kijiti kilichoachwa na Manji. Yanga SC-Daima mbele nyuma mwiko.

Hakutanga kuharibu malengo ya timu-kushinda taji la 3 mfululizo ndiyo maana licha kukumbwa na misukosuko  mingi hivi karibuni aliamua kuonyesha yuko nao.  Nadhani watu wa Yanga wanapaswa kumshukuru tu Manji licha ya kwamba kama mwanadamu alikuwa na mapungufu yake. Amejiuzulu wakati ambao anaona Yanga inaweza kupata kiongozi mpya na kusaidia sajili na maandalizi ya msimu ujao.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here