Home Kitaifa Juma Liuzio: ‘Nilichokikimbia Zesco, nimekipata Simba, nimefanikiwa, tutafanikiwa FA Cup

Juma Liuzio: ‘Nilichokikimbia Zesco, nimekipata Simba, nimefanikiwa, tutafanikiwa FA Cup

13791
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

MSHAMBULIZI wa Kimataifa wa Tanzania, Juma Ndanda Liuzio anaamini kile alicho ’kikimbia’ Zesco United ya Zambia ‘amekipata’ kwa mafanikio makubwa klabuni Simba SC. Liuzio alisaini kujiunga na Simba mwishoni mwa mwezi Disemba, 2016 kwa mkataba wa mkopo wa miezi 6 akitokea Zesco.

Wakati anaondoka Zesco, mshambulizi huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar FC alisema ameichagua Simba kwa sababu ya kuhitaji nafasi ya kucheza baada ya miezi sita migumu kwa mabingwa hao wa zamani wa Zambia.

Liuzio alisumbuliwa na maumivu ya nyama za paja ambayo yalimfanya kushindwa kuichezea Zesco kwa miezi minne mwaka 2016 na hata pale alipopona na kurejea kikosini hakuwa katika kiwango cha juu kama awali.

Simba ambayo ilionekana kusumbuliwa na ufungaji katika michezo ya raundi ya kwanza waliamua kutumia nafasi ya usajili mdogo kumsaini Liuzio ili kusaidiana na Mrundi, Laudit Mavugo, Muivory Coast, Blagnon na kijana mwenzake Ibrahim Ajib.

Kuelekea michezo ya kukamilisha msimu mwishoni wa wiki hii, Simba ina asilimia 1 tu ya kushinda ubingwa wa VPL kwa maana wanahitaji angalau ushindi usiopungua magoli 12-0 dhidi ya Mwadui FC huku wakiomba ‘watani’ wao wa jadi Yanga wapoteze mbele ya Mbao FC katika uwanja wa Kirumba, Mwanza.

“Inawezekana kama timu tusiwe tumefanikiwa sana, lakini kama mchezaji naweza kusema nimetimiza malengo yangu. Wakati natoka Zesco niliamini Simba inaweza kunisaidia. Na msaada nilioutaka kutoka kwao ni kupata nafasi ya kucheza baada ya kushindwa kupata Zesco kutokana na majeraha yaliyoniweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.” Anasema Liuzio nilipofanya mahojiano naye wiki hii.

Wakati Simba ilipoamua kuingia sokoni kusaka mshambulizi-mfungaji wa nyongeza Mavugo alikuwa amefunga magoli manne tu, Ajib alikuwa na magoli matatu huku Blagnon akiwa amefunga goli moja tu hadi raundi ya kwanza inamalizika. Ukiachana na michezo ya kirafiki, Liuzio ameifungia Simba magoli matatu tu katika michezo 13 ya ligi kuu huku akipiga pasi nne za mwisho zilizozaa magoli. Amefunga kwa kiasi cha pungufu goli moja dhidi ya Mavugo ambaye katika michezo ya mzunguko wa pili amefunga magoli manne tu ambayo yanamfanya kufikisha jumla ya magoli 8 katika michezo 29 ya ligi kuu.

Inawezekana washambuliaji wote wa Simba wameshindwa kufikia matarajio kiasi cha kuzidiwa mabao na viungo watatu Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin na Mohamed Ibrahim ambao kiujumla wamefunga magoli 24 kati ya 48 ya timu yao katika VPL. Mavugo, Ajib, Blagnon, na Liuzio wamefunga jumla ya magoli 20 kati ya 48 yaliyofungwa na Simba katika michezo 29.

“Malengo yangu ni kurudi nje ya nchi mara baada ya mkataba wangu wa mkopo utakapomalizika hapa Simba. Tayari kuna timu zimeniomba video zangu nikiwa uwanjani na kila kitu kinaenda sawa hadi sasa.” anasema Juma ambaye amefunga jumla ya magoli 7 pamoja na yale aliyofunga katika michuano ya Mapinduzi Cup 2017 na michezo ya kirafiki.

“Nimejifunza mambo mengi mazuri nikiwa hapa. Unajua Simba ni klabu kubwa zaidi ya Zesco. Ukizingatia Simba ina mashabiki wengi inachoa mchezaji kujenga hali ya kujiamini. Nimejifunza kujiamini zaidi na kuhimili presha ya mashabiki.”

“Nimependa aina ya maisha ambayo wachezaji wamekuwa wakiishi-wanaishi kirafiki sana tofauti na nchi nyingine na hili limenifanya kuwa huru. Pamoja na yote sijafurahishwa na hali ya wachezaji kukaa kambini muda mrefu japokuwa tayari nimeshazoea.”

Licha ya kuonekana kushindwa kubeba ubingwa wa VPL msimu huu, Simba wana nafasi ya kushinda ubingwa wa kombe la FA kama tu wataifunga Mbao FC katika mchezo wa fainali mwishoni mwa wiki ijayo. Hili ni jambo linalomfanya Liuzio kuamini kuwa bado ipo nafasi ya kufanikiwa yeye kama mchezaji huku pia klabu ikinufaika.

“Napenda kuwaambia wana Simba wote, Kwanza nawashukuru sana kwa kuwa pamoja na sisi katika vipindi vigumu na raha. Na nawaomba sana waongeze upendo kwa wachezaji wao na wajitokeze kwa wingi kwenye mchezo wa fainali. Kila mmoja anataka kushinda ubingwa huo miongoni mwetu na naamini tutashinda. Naamini wao wana umuhimu mkubwa kuliko hata viongozi. Hatutawaangusha.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here