Home Kitaifa Jicho la 3: Kwanza jiulize MO ni nani hasa ndani ya Simba,...

Jicho la 3: Kwanza jiulize MO ni nani hasa ndani ya Simba, kwanini anakopesha kwa maandishi?

20858
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

MUNGU anawapenda sana watu masikini, angekuwa hawapendi asingekuwa anawaumba wengi namna hii. Mungu anawapa hekima na busara viongozi ili waweze kuwaongoza masikini ili wasitumiwe na ‘mabepari’ na kukandamizwa. Ni dhambi mbaya sana kumkandamiza masikini.

Heshima inaombwa? Uhuru unaombwa?

Yanga SC inasubiri ‘muujiza’ tu kushindwa kutetea ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya 3 mfululizo mwishoni mwa wiki hii watakapokuwa ugenini kucheza mchezo wa mwisho vs Mbao FC katika uwanja wa Kirumba, Mwanza. Hili nilitaraji, tangu mwanzo wa msimu huu nimekuwa nikiandika na kusisitiza kuwa Simba haikidhi vigezo vya kushinda taji la VPL msimu huu.

Niliamini hivyo na sikutaka kuvunjwa imani yangu na yeyote yule. Je, nimekosea wapi? Wako wapi wale ambao walikuwa wakipinga hoja zangu kwa kashfa na matusi? Nimekuwa mshindi kwa mara ya tano mfululizo kwa sababu ndani ya misimu mitano Yanga inaelekea kushinda ubingwa wa nne huku timu ‘changa’ katika soka la Tanzania-Azam FC ikishinda taji hilo mara moja.

Simba si nguvu moja

Busara na hekima ni tatizo pekee lililobaki klabuni Simba, na ili wafanikiwe kupata mafanikio ya ndani na nje ya uwanja-Simba kama klabu wanatakiwa kujitazama wenyewe katika vioo vyao na kurudisha kumbukumbu ya mafanikio yao yaliyopita.

Ilifanyaje hadi ikapata jengo ambalo ni makao makuu ya klabu hivi sasa, ilifanyaje ikaweza kushinda mataji 19 ya ligi kuu ndani ya miaka isiyozidi 60, walitumia njia gani kutengeneza kikosi kilichoweka rekodi isiyofikiwa hadi sasa-klabu pekee ya Tanzania kufika nusu fainali ya Caf Champions League (historia tuliyozaliwa na kuikuta ni kwamba timu hiyo kutoka Mitaa ya Msimbazi ilifanikiwa kufika nusu fainali ya klabu bingwa Afrika mwaka 1974)

Ni lazima kwanza ‘wahitaji-mabadiliko’ wajiulize kilitokea nini hadi wakayumba kwa miaka karibia 20 katika soka la Afrika na kurejea hadi kufika fainali ya michuano ya Caf Confederation Cup mwaka 1993? Naweza kuielezea Simba kuanzia hapo hadi sasa yapata miongo miwili na nusu.

Majibu ya maswali ilipotoka Simba unayaweza kuyajibu hata wewe msomaji wa makala haya lakini unaifahamu Simba SC? Siamini katika njia ya mabadiliko inayotaka kutumiwa na ‘kikundi’ cha watu wenye maslahi yao binafsi.

Unawezaje kubadili taasisi iliyojiendesha kwa miaka zaidi ya 80 ndani ya mwaka mmoja baada ya wazo hilo la mabadiliko kuwasilishwa? Unawezaje kubadili mfumo wa uendeshaji ulioifanya klabu kuishi kwa miongo nane mfululizo bila kuwashirikisha waasisi?

Kizazi chetu hiki kina matatizo makubwa sana. Kwanza tunashabikia mambo ambayo hatuyajui kiundani. Tunafahamu njia za mabadiliko kuliko wakubwa zetu.

Mabadiliko gani yanatakiwa?

Nimeshangazwa sana na mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu Zacharia Hans Poppe kubembelezwa arejee madarakani siku moja baada ya kuwasilisha baraua ya kujiuzulu nyazifa zake klabuni hapo kisa tu uongozi wa Rais wa klabu, Evance Aveva na makamu wake kuingia mkataba mnono hivi karibuni na kampuni ya SportPesa.

Kujiuzulu kwa Poppe kulikuja muda mfupi baada ya Mohammed Dewji kutaka klabu hiyo ya Simba imlipe kiasi kisichopungua bilioni 1.4 ambazo alikuwa akiikopesha klabu hiyo ndani ya miezi isiyozidi kumi iliyopita.

Unakumbuka makala haya niliyowahi kuandika?

Mara baada ya baadhi ya wanachama wa klabu ya Simba kukubali ‘mabadiliko’ katika mkutano mkuu wa mwaka wa klabu hiyo, tajiri/mfanyabiashara na mwanachama wa klabu hiyo Mohammed Dewji ‘MO’ aliusaidia uongozi wa timu hiyo kiasi kisichupungua milioni 100 ili kusaidia usajili wa baadhi ya wachezaji.

Hakuishia hapo, tajiri huyo mkubwa barani Afrika ameendelea kutoa msaada wa kifedha na inasemekana hadi sasa amekwisha saidia zaidi ya milioni 600-fedha ambazo zimekuwa zikisaidia klabu kuwalipa mishahara wachezaji na baadhi ya viongozi walioajiriwa klabuni hapo.

Kumbuka Simba haina mdhamini yeyote hivi sasa baada ya kumalizika kwa mkataba wao na bia ya Kilimanjaro.

Kitu kinachonishangaza ni kwanini uongozi wa timu haufanyi jitihada zozote za kufanikisha klabu kupata wadhamini mara baada ya mkataba wao na Kilimanjaro kumalizika?

Nadhani ‘wamepumbazwa’ au wameridhika na misaada ambayo MO amekuwa akiitoa katika miezi ya karibuni. Inawezekana viongozi wa sasa klabuni hapo wameshindwa kuyashiwi makampuni kujitangaza kupitia klabu yao!

Inashangaza sana, timu kubwa kama Simba kukosa mdhamini hata mmoja na kutegemea misaada kutoka kwa mwanachama kuendesha timu!

Najiuliza, ni kwanini MO anaisaidia sana Simba katika utaratibu wa ufadhili na si kuingia nao mkataba? Nadhani hata yeye anatoa msaada hivi sasa kwa kuwa naye anaamini klabu inakwenda katika mabadiliko makubwa kiuendeshaji.

Nimenukuu sehemu tu ya makala yale yaliyopita, na sasa naamini

Ukimsikiliza MO, sehemu ya mazungumzo yake mara baada ya kuibuka katika vyombo vya habari hivi karibuni utagundua ni ‘mtu mbinafsi, ndiyo maana alisema kuna kampuni ipo tayari kuingia mkataba na Simba SC kwa kiasi kisichopungua bilioni 2 kwa mwaka, lakini hapo hapo anasema-watakuja baada ya klabu kubadili katiba yake na kukubali mabadiliko ya kiuendeshaji.

Aveva anaonekana hataki kubeba ‘msalaba’ ambao wenzake wote waliukwepa ndiyo maana anatafuta wadhamini wenfgine ambao wataendelea kusaidia uendeshaji wa klabu wakati huu suala la mchakato wa mabadiliko likiendelea.

Ningekuwa na mamlaka ya kubadili katiba ya Simba kitu cha kwanza na muhimu ni kuweka kamati ambayo itatambulika kikatiba kama yenye mamlaka ya mwisho kikatiba kukubali jambo kubwa la klabu lililopitishwa na mkutano mkuu wa wanachama. Angalau watu 100 wanatosha kuingia katika kamati hiyo na hawa wanaweza kutoka kila mkoa wa Tanzania mahala ambako Simba ipo kikatiba.

Kuwaacha wanachama tu wapitishe jambo lolote katika mkutano mkuu si vyema kwa sababu wanachama wengi wa kizazi cha sasa hawajui chochote kuhusu Simba zaidi ya kuwa ‘bendera fuata upepo tu.’

Wanachama wengi wa klabu ya Simba hawajui ni kwanini klabu inakwama na hawajiulizi ipi ni njia sahihi ya kuifanya klabu kujiendesha bila kutegemea nguvu ya watu binafsi.

Baada ya MO kutoka hadharani na kusema anahitaji kulipwa pesa alizoikopesha Simba msimu huu kisa tu hakushirikishwa katika mkataba wa SportPesa, kulinifanya nijiulize sana, HUYU MO NI NANI HASWA NDANI YA SIMBA ukiachana na uanachama wake? Eti, msomaji  wa makala haya unaweza nisaidia jibu, MO ni nani hasa ndani ya Simba hadi alalamike kutohusishwa katika mikataba halali ya klabu na wadhamini?

Kwanini MO aliweka makubaliano ya kulazimisha ashirikishwe katika makubaliano yoyote ya klabu na wadhamini watakaojitokeza wakati yeye anaikopesha klabu na ndani ya muda mfupi deni limefikia bilioni 1.4? ni kwanini amechukia baada ya Aveva kumwambia watamlipa pesa zake mara baada ya kuingia mkataba na SportPesa?

Je, wakipatikana wadhamini wengine watatu au wanne wanaokaribia au kupita thamani ya SportPesa Simba haitaweza kujiendesha? MO anataka kuwekeza nini wakati tayari ni mshindwa? Simba inaweza kumlipa chochote anachotaka MO sababu ni tajiri na maarufu zaidi ya MO na hili lingewezekana ikiwa idara ya masoko ingekuwa inafanya kazi kwa ajili ya klabu na si watu binafsi kama ilivyo sasa.

Kabla ya kukaa meza moja na MO viongozi wa klabu wangejiuliza huyu MO ni nani hasa katika klabu? Mimi nafahamu ni mwanachama anayesaidia na kuwakopesha Simba kwa maandishi ili waweze kujiendesha. Anakopesha ili pesa zake zirudi. Kwanini mkataba wake na wadhamini itakuja baada ya mabadiliko? Kabla ya mabadiliko Simba iendelee kumkopa yeye au itafute njia nyingine ya kujiendesha?

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here