Home Kitaifa TFF Inapojitekenya na Kucheka Yenyewe

TFF Inapojitekenya na Kucheka Yenyewe

20041
0
SHARE
Rais wa TFF Jamal Malinzi (kushoto) na Ofisa mtendaji Mkuu wa Azam Media Rhyth Torrington (kulia) wakisaini mkataba

NA ABDUL DUNIA

Tumeshazoea kuwaona watoto wadogo wakicheza michezo tofauti kila kukichwa ikiwemo kujitekenya na kucheka wenyewe. Tunaona kawaida kwa kuwa ni watoto.

KITENDO cha Mtu mzima kujitekenya na kucheka mwenyewe kinaweza kuonekana kama ni mzaha lakini inawezekana kwenye maisha ya kila siku. Sio tu kwa wale watoto wadogo tunaokutana nao mitaani na hata majumbani kwetu.

Nadhani sijakosea naposema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeamua kujitekenya na kucheka lenyewe kuhusiana na hili la Kamati ya Saa 72 na ile ya Katiba. Hakuna asiyefahamu hilo.

Hivi Karibuni, Kamati ya Saa 72 iliyoongozwa na Hamadi Yahaya iliipa pointi tatu Simba baada ya kubainika beki wa Kagera Mohammed Fakhi alicheza akiwa na kadi tatu za njano ambazo alizipata kwenye mechi dhidi ya Majimaji, Mbeya City na African Lyon.

Siku chache zilizopita, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa ilitoa kauli ya kuwa pointi hizo zilitolewa kimakosa na kurudishwa kwa Kagera. Halikuwa tatizo ni kawaida ya rufaa kukubaliwa ama kukataliwa.

Tatizo ni uamuzi mara mbili uliofanya vichwa vya Watanzania, Mashabiki wa Simba, Yanga na Kagera kutaharuki kutoka na majibu hayo. Kuna pande iliyofurahi nyingine kuhuzunika na nyingine pia kukata tamaa juu ya soka la Tanzania.

Pande hizi zimegongana, TFF imegongana na Bodi ya Ligi imegongana. Kamati ile ya Yahya, Mwesigwa (Katibu) na Malinzi (Rais) pamoja na ile ya Bodi ya Ligi inayoongozwa na Wambura zote zimepishana na uamuzi wao.

Naanza kupata picha ya yule aliyesema kuwa Hakuna watu wanafiki kama wale tunaojiita watu wa Soka au Familia ya Soka. Naungana naye mkono mtu yule. Tuje kwenye Hoja Kuu.

Sipo hapa kuitetea Kagera, Simba, TFF wala Bodi ya Ligi bali nipo hapa kueleza ule ukweli niliouona juu ya zile Kamati zetu zinazoongozwa na Watu tunaojiita ama kuitwa Familia ya Soka.

FAKHI alikuwa na Kadi tatu za Njano (Kwa Sauti ya Mwesigwa). Kwa Mantiki hiyo Kanuni ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania inasema kuwa Mchezaji atakayebainika kuwa ana kadi tatu za njano kwenye michezo mitatu mfululizo na akacheza wa nne, timu yake itapokwa pointi na kupewa timu pinzani.

Mchezaji atakayebainika ana kadi tatu za njano hakuna rufaa itakayotendeka badala yake Bodi na Shirikisho lenyewe litatoa ufafanuzi juu ya hilo.

MSIMU uliopita Azam FC ilipokwa pointi 3 na kupewa Mbeya City baada ya kumchezesha beki wake

Erasto Nyoni aliyekuwa na kadi tatu za njano. Mbeya City haikukata rufaa. Bodi na TFF zilitoa adhabu hiyo baada ya kugundua hilo. Hapo ndipo Tatizo lilipoanzia.

Simba imepokwa pointi walizopewa awali kwa hoja tatu thabiti kutoka TFF ambapo ya Kwanza ilikuwa ni Rufaa kuwasilishwa nje ya muda. Hakuna rufaa kwenye kadi tatu za njano. Bodi na TFF zililazimika kutoa ufafanuzi mbali na rufaa ya Simba. Ni wajibu wao.

Kama Rufaa iliwasilishwa nje ya muda kwanini Kamati halali ya Saa 72 ilikaa? Walipata wapi taarifa, nani aliidhinisha uwepo wa kikao hicho na posho zake?

Kama rufaa ilichelewa ilitakiwa kutupiliwa mbali. Haikutakiwa kusikilizwa kabisa. Kamati ilikaa, wajumbe walialikwa, TFF wakatoa fedha za kugharamia kikao na kulipa wajumbe posho, leo inakuwaje rufaa kucheleweshwa? bila ya kupepesa macho kuna ubabaishaji hapa.

Hoja ya Pili ilikuwa ni Rufaa kutolipiwa Ada au Pesa. Kwa kawaida rufaa isipolipiwa haipaswi kusikilizwa inakuwa sio halali tena ‘Invalid’ (Haijatimiza viwango vya kuwa Rufaa). Zipo nyingi zilitopiliwa mbali ikiwemo ile ya Polisi Dar. Kwa nini hii haikutupiliwa mbali kama ile na kuamua kuijadili?

Hoja ya Tatu, Kamati ya Saa 72 kualika wajumbe kutoka nje ya TFF na Bodi ya Ligi. Kama ni kweli Kamati ya saa 72 ilialika wajumbe kutoka nje kimakosa je, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyotengua uamuzi ya ile Kamati ya Kwanza imetoa pendekezo la kuvunja kamati hiyo ili makosa ya namna hiyo yasijirudie tena baada ya kuundwa kwa Kamati mpya? Sijui labda tusubiri.

Turudi nyuma kidogo, Kagera Sugar hawakuandika barua ya kulalamika juu ya Simba kuwasilisha rufaa nje ya muda, Kutolipia Ada Rufaa yao na Uhalali wa ile Kamati ya Saa 72.

Waliandika Barua kupinga kuwa Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano, je, Fakhi alikuwa na kadi au hakuwa nazo? Hiyo ndiyo pointi ya msingi kujadiliwa kwenye Kamati.

Sihitaji kuzungumza sana, ngoja niweke akiba ya maneno yangu. TFF ilihitajika kutoa uthibitisho juu ya kadi tatu za Fakhi na kama kweli alikuwa na kadi tatu kama ilivyosema ile Kamati ya Kwanza basi Simba ilikuwa na uhalali wa kupewa zile pointi walizopewa hapo awali bila ya kukata rufaa.

Kwenye hili la Fakhi na kadi za njano. Naamini sijakosea naposema TFF inajitekenya na Kucheka yenyewe.

Sidhani kama Fakhi alikuwa na hizo kadi, maana navyoifahamu Ligi yetu ingekuwa kweli anazo basi uamuzi wake usingechukua siku nyingi. Ungekuwa ni sawa na kumsukuma mlevi kwenye mtaro wa Maji.

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here