Home Kimataifa Karibu Mbappe, Tumeona Nyama Alizokula Ronaldo, Tunawaza Mifupa Utakayoitafuna.

Karibu Mbappe, Tumeona Nyama Alizokula Ronaldo, Tunawaza Mifupa Utakayoitafuna.

24469
0
SHARE

Usiku wa tarehe 12 April, kinda huyu aliyewahi kuruka hatimaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kufunga mabao mawili katika mchezo mmoja kwenye hatua ya mtoano. Ndio, anaitwa Mbappe huyu ambaye anafananishwa na Thierry Henry ingawa moyo wake upo Madeira akijaribu kuyaishi maisha magumu kwenye soka ya Cristiano Ronaldo. Mbappe amepitia ukuaji wake akizibusu na kupiga magoti mbele ya picha za Cristiano Ronaldo, akiomba kila usiku unaopita aweze kuwa kama yeye.

Pengine Mbappe anaweza asiwe mbali na moja ya matukio ya ndotoni mwake, inawezekana kabisa akatupa shuka na kuanza kuzitumikia ndoto zake. Lakini kama mchezaji Lebron James alivyowahi kusema juu ya Michael Jordan kuwa anafukuza Zimwi, basi Mbappe naye kaingia katika mbio hizo, anafukuza Zimwi ambalo limekua, limeishi na likaifahamu damu inayoitwa mafanikio.

Haikuwahi kuwa rahisi kwa Cristiano kufika hapo, hakikuwa kitu rahisi kumfanya mwanamitindo Irina Shayk kumfanya ajute kuachana nae na wala sio jambo jepesi kwa mwanafasheni Georgina Rodriguez kuamua kuacha kazi kwenye kampuni kubwa kama Prada kwa sababu ya jina la Cristiano Ronaldo.

Haya ni maisha aliyoyapigania, ameyajenga na amestahiki kuwa hapo. Ikiwa katika usiku huo huo wa Mbappe, Cristiano Ronaldo akiubadili kuwa wake kwa kufikisha mabao 100 kwenye mashindano ya Ulaya anabaki kuwa jina la kipekee ambalo wino utatumika wa moto kuliandika kwenye vitabu vya soka.

Huyu ambaye wengi wanamfahamu Jorge Mendes kama binadamu anayemwongoza lakini ukweli unabaki kuwa kuna mwanaume anayeitwa Ricky Regufe ambaye aliamua kuachana na soka ili akasome namna ya kuendesha maisha kama ya akina Ronaldo na akafanikiwa kuokota almasi hii ya Madeira na kuifuta vumbi.

Huyu ndiye haswaa anayeamua mpaka mtindo wa kunyoa wa Ronaldo, huyu ambaye Ureno ilibidi wamuweke kwenye orodha ya watendaji wao ili aende kwenye mashindano ya mataifa Ulaya na Ronaldo. Anaishi Ronaldo, anapumua na kula Ronaldo.

Lakini ni Ronaldo huyu ambaye vitabu itabidi viandike kuwa ni mwanadamu pekee aliyezisalimu nyavu kwenye mashindano ya kombe la dunia ya 2006, 2010, 2014 na mashindano ya mataifa ya Ulaya ya 2004, 2008, 2012 na 2016 ambako alikuwa bingwa. Hakuna binadamu mwingine anayepumua aliyefanya hili.

Dunia imesahaulishwa na mabao 100 ya Ulaya kuwa huyu ndiye mwanadamu anayeongoza kwa hattricks kwenye La Liga alizofunga kwa wakati mfupi kuliko mtu mwingine yoyote, anazo 32 juu ya wote.

Kama kuna upande Mbappe atatakiwa kuuwaza pia ni kuwa mwanaume huyu amesimamisha dunia kwenye mitandao ya kijamii, watu wanamfuata kuliko mwanamichezo yoyote Yule, alipewa na muonekano huyu.

Aliishi kwenye historia za kina Figo, Nuno Gomes, Pauleta, na Eusebio lakini alivuka bahari ya shamu na fimbo ya Musa na kuzitenganisha zote hizi na kuweka zake, anaongoza kwa magoli kwa nchi hiyo.

Mashabiki wa Madrid waliishi katika zama za Raul, Alfredo Di Stefano na akina Carlos Santillana ambao wote waliishi Madrid kwa zaidi ya miaka 10 wakifunga wanavyojisikia, Ronaldo alifika na hakuacha hata jiwe moja likiwa halijageuka, ilimchukua miaka 6 tu kuwa mfalme.

Lakini huyu ndiye mchezaji aliyeshinda vikombe vyote katika ngazi ya klabu, na tuzo zote zinazohusu wachezaji akiwa na vilabu viwili tofauti, hakuna mwingine aliyewahi kufana hili. Ni huyu Ronaldo ambaye mama Dolores aliyekuwa mpishi na mzee Dinis ambaye alikuwa mtunza bustani waliamua kuongeza mtoto wa mwisho katika familia kumbe hawakujua wanaongeza malaika kwenye soka.

Bahati mbaya hata baba yake aliyepoteza imani na maisha na kufa kutokana ulevi na kuathiri hakufanikiwa kushuhudia ubora wa huyu malaika, hakufanikiwa kuziona nyakati mabazo hotel maarufu za Pescana ni za mwanae, nyakati ambazo sanamu maarufu Hispania ni ya mwanae na nyakati ambazo hata uwanja wa ndege wa kimataifa umepewa jina la mwanae.

Inawezekana Ronaldo akawa na makumbusho nchini Ureno lakini Mbappe anatakiwa kufahamu kuwa makumbusho ya kudumu Ronaldo amejenga vichwani mwetu na hilo la mabao 100 ni mojawapo tu. Ronaldo alikula nyama alivyojisikia, tungependa uende mbali zaidi ule na mifupa, lakini nina mashaka kama meno thabiti unayo.

Kumuishi huyu sio jambo dogo, Mbappe ana miguu inayofaa, ana ubongo wenye rutuba na ana kila kitu cha kuwa mchezaji bora. Lakini kuna jambo moja tu ambalo huwa ni gumu siku zote, kufuta mhuri wa moto na Ronaldo ameshaweka huu. Ahsante Ronaldo na Karibu Kylian Mbappe, macho yetu yatakuwepo kwenye Tv kwa miaka 15 ijayo.

By Nicasius Angwanda (Coutinho)

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here