Home Kitaifa Jicho la 3: Kama ningekuwa katika nafasi ya Aveva/MO Dewji ningefanya tafakari...

Jicho la 3: Kama ningekuwa katika nafasi ya Aveva/MO Dewji ningefanya tafakari kuhusu ‘kauli mbaya’ ya Manara

25517
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

Geofrey Nyange Kaburu ana nyadhifa ngapi katika soka la Tanzania? Tatizo la soka la Tanzania linaanzia hapo na msemaji wa klabu ya Simba SC, Haji Manara yuko sahihi kabisa kumshinikiza rais wa TFF kujiuzulu katika moja ya nafasi zake mbili za uongozi wa soka. Malinzi ni mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Kagera pia ndiye rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF).

SIMBA SC

Kuelekea michezo mitatu ya kumaliza msimu, Simba wameshapoteza ‘dira’ ya kushinda ubingwa na kinachofanywa sasa na uongozi wa klabu hiyo ni kuwaaminisha wanachama na mashabiki wa klabu hiyo ‘wameshindwa’ kwa sababu ya watu fulani waliopo katika Kamati mbalimbali za TFF. Kumbe Sivyo.

Simba imefanikiwa kuchukua alama nne kati ya sita dhidi ya washindani wao wa ubingwa msimu huu-Yanga SC (Simba 1-1 Yanga, Yanga 1-2 Simba). Wamefanikiwa kuchukua pointi tatu kati ya sita vs Kagera Sugar FC (Simba 2-0 Kagera, Kagera 2-1 Simba), wamefanikiwa kuchukua alama tatu mbele ya Azam FC (Simba 1-0 Azam, Azam 1-0 Simba), wakachukua alama nne dhidi ya Mtibwa Sugar FC (Simba 2-0 Mtibwa, Mtibwa 0-0 Simba), pia wameshachukua alama Tatu vs Mwadui FC (Mwadui 0-3 Simba)

Kwa mlolongo wa matokeo ya ndani ya uwanja dhidi ya timu 6 za juu katika msimamo wa ligi kuu ni wazi Simba ndiyo timu iliyofanikiwa zaidi kuliko Yanga, Azam FC, Kagera, Mtibwa na Mwadui katika mipambano iliyowahusisha wenyewe kwa wenyewe. Je, ni timu gani imebebwa kuliko nyingine kati ya timu hizi 6 za juu zaidi ya Simba?

Haji si mtu mwenye ufahamu kuhusu soka ndiyo maana amekuwa aki-ropoka bila mpangilio wala kuwa na kumbukumbu. Simba ndiyo timu yenye wanachama wengi hai ndani ya kamati za TFF.

KUHUSU POINTI 3 ZA KAGERA

Ndani ya uwanja Simba wameshapoteza mechi, wakakimbilia mezani kurudia mechi, wakashinda chini ya Kamati ya saa 72 ambayo naiita ‘Kamati ya Kahawa’ kwa sababu ni kamati iliyoshindwa kufanya kazi yake vile ilivyopaswa.

Ikumbukwe pia ndani ya Kamati hii ya saa 72, Wanakamati wengi ni wanachama/wapenzi wa Simba hivyo ni wazi Kagera isingeweza kupata haki hasa ukizingitia ‘umuhimu’ wa pointi 3 ambazo Simba wanazitaka bila ‘kuvuja jasho’

Ni aibu kubwa sana, kuona Simba ikizunguka na uongozi wote wa juu Kanda ya Ziwa na kuambulia pointi nne tu! Labda hili ndiyo linawauma lakini hawawezi kubadilisha ukweli kuwa walifungwa 2-1 na Kagera japokuwa ‘Wana-kamati wa saa 72’ walitumia ‘utashi’ wao kuwapa Simba pointi ambazo hazikustahili.

NILITABIRI SIMBA ITACHEZA MISIMU 6 MFULULIZO BILA TAJI LA VPL, NA BADO MSIMU UJAO

Kabla ya kuanza kwa msimu huu niliandika sababu Tatu ambazo nilisema ‘nitazitumia kama fimbo ya kuichapa Simba msimu wa 2016/17’ na fimbo hizo zote zinafanya kazi niliyotaraji. Naendelea kuichapa timu ambayo sikupaswa kufanya hivi lakini imenibidi niichape tu ili mambo yajerejee kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Sababu ya kwanza nilisema, Hamis Kiiza. Kumuacha mfungaji bora wa klabu aliye ndani ya mkataba kwa sababu tu alidai pesa zake za mshahara, kwa jicho langu la 3 niliona ni kosa kubwa. Lakini Zacharia Hans Poppe ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usajili klabuni hapo aliamini Simba inaweza kuziba pengo la Mganda huyo aliyefunga magoli 19 katika michezo 22 ya VPL msimu uliopita na nakudhani Mrundi, Laudit Mavugo atafaa kuziba nafasi ya Kiiza.

Poppe na hata tarajio lenyewe Mavugo wote wameshafeli. Na kufeli kwao ni kufeli kwa timu ndani ya uwanja. Katika magoli 43 waliyofunga Simba msimu huu huku wakisalia na michezo mitatu kabla ya kumalizika kwa msimu, mfungaji anayeongoza kwa ufungaji ni kijana Shiza Kichuya.

Huyu alisajiliwa akitokea Mtibwa Sugar na wakati wa tetesi za usajili wake June 2016 niliandika Simba inapaswa kumsaini winga huyo wa kulia na uwepo wa Kiiza ulikuwa ni sawa na kumaliza tatizo ambalo liliwaangusha kwa kiasi fulani wakati Mganda huyo alipokosekana katika baadhi ya michezo msimu uliopita.

Niliamini uwezo wa Kiiza katika ufungaji na kwa kweli kati ya wafungaji mahiri wa kigeni ambao nimepata kuwaona VPL, Kiiza ni mfungaji wa hatari hasa pale timu yake inapocheza kwa kushambulia. Kiiza alikuwa na njaa ya magoli na alijua kujipanga akiwa ndani ya eneo la hatari. Alifunga ‘hat-tricks’ mbili msimu uliopita akicheza katika timu isiyotengeneza nafasi nyingi za kufunga kama hii ya sasa.

Mavugo amekosa ‘msukumo’ japo wengi wana mtetea kwa kusema apewe muda. Atapewaje muda wakati kila msimu klabu inasajili mshambulizi mpya?

Kiiza aliingia Simba na kufunga magoli 24 katika michezo isiyozidi 30 msimu uliopita na alifanya hivyo akiwa mchezaji mpya kikosini. Ila hakupewa muda kwa sababu ya kudai stahiki zake ilikuwa ni kosa kwa watawala wa klabu na kumjumuisha katika ‘wahujumu klabu’ mzigo ambao uliambatatana na matusi kutoka kwa baadhi ya mashabiki na wanachama wa klabu.

Goli 11 za Kichuya na saba za Mavugo walizofunga hadi sasa kuelekea michezo mitatu ya mwisho ya klabu yao, bado wawili hao hawajafikia magoli aliyofunga Kiiza msimu uliopita wakati kama huu alikuwa tayari na magoli 19.

Kiiza ilikuwa ni muendelezo wa usajili ‘mbovu’ usiozingatia mahitaji ya timu. Aliachwa Amis Tambwe wakati akiwa mfungaji bora wa klabu, wakiamini katika Elias Maguli wakati wote wawili walipaswa kucheza hata kama si katika kikosi kimoja mchezoni.

Nilishasema Masvugo hawezi kufikia nusu ya magoli aliyofunga Kiiza msimu uliopita kwa sababu niliamini atahitaji muda, ndiyo maana nilitaka kuona Kiiza anasalia hata kama Mavugo angesajiliwa. Neno lilolowahi kumkera Rage ni pale nilipomwambia, Yusuph Manji ni mtihani wake wa kwanza mkubwa kwake na klabu kiujumla Julai, 2012.

Japo hajafanikiwa kwa kiasi kikubwa sana nje ya uwanja ila kati ya Agosti 2012 hadi sasa Manji ni mshindi wa kweli vs Simba ndani na nje ya uwanja. Mwenyekiti huyu wa Yanga amepevuka katika maeneo ya kibiashara na jambo pekee alilotaka kuona ni klabu ikishinda mataji ya ndani ya nchi na kupambana ‘kupenya’ katika soka la Afrika.

Chini ya Manji kama mwenyekiti, Yanga wamekuwa wamoja nje ya uwanja, wamekuwa washindi wa vikombe vitatu vya ligi kuu na huenda wakaenda kushinda kikombe cha nne ndani ya msimu wa tano Mei mwaka huu. Manji amewapa uhuru makocha kufanya sajili zile walizotaka na jambo hilo limeifanya timu kuwa bora ndani ya uwanja na kutawala soka la ndani.

Amefanya kazi na makocha wanne huko nyuma, Tom Saintfiet ambaye alimfukuza ndani ya siku 76 baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili Julai, 2012. Raia huyu wa Ubelgiji alimwambia Manji ‘amuache afanye kazi yake’ huku pia akimpiga kijembe kwa kumwambia, ‘wewe ni mfanya biasha, ila si mfanyabiashara wa kimataifa’

Akamleta Mholland, Ernie Brandts, kisha Babu Hans van der Pluijm, Mbrazil, Marcio Maximo kwa miezi 6, Hans na sasa Lwandamina. Ndani ya makocha hao licha ya kukosea mara kadhaa, Manji alijifunza kitu kuwa ili pesa anazozitoa zifanye kazi anayotaka ni lazima azipe uhuru. Ndiyo maana Hans alisema ‘toa milioni 200 kwa Obrey Chirwa aje hapa’ na Manji kama mwenyekiti alisema ‘pesa itolewe’

Lakini kwa Simba kila wakati wa usajili timu inakuwa haina kocha, hapo ndipo Poppe hufanya kazi yake na hajawahi kufanikiwa kwa sababu huwezi kumuacha mfungaji kama Kiiza kwa kutegemea mfungaji kutoka ligi kuu ya Burundi moja kwa moja. Kuna mechi nyingi msimu huu Simba imeangushwa na washambuliaji, na yote kwa sababu haikuwa na mbadala katika ufungaji kama Kiiza.

Leo hii, Basrcelona hawezi kumuuza Lionel Messi eti kwa sababu watakuwa na uwezo wa kumsaini Edinson Cavani kutoka PSG! Usajili wa Kamati ya usajili Simba ni sababu ya yote haya yanayotokea sasa upande wa timu hiyo. Sasa wanataka hadi ‘kuandamana’ hii ni kali sana, uandamane wakati wewe ni mfalme wa Top 6? Fikirini kabla ya kusema.

KOCHA OMOG

Nimekuwa shabiki wa klabu ya Simba kwa maisha yangu yote ya ufahamu na kamwe siwezi kuwa shabiki wa klabu nyingine hapa Tanzania japokuwa siridhishwi na mwenendo wa klasbu hii tangu msimu wa 2012/13.

Sijawahi kuona tumaini la kunyanyuka kwa Simba chini ya utawala huu wa rais Evance Aveva na makamu wake Kaburu. Na niliwahi kumwambia Ismail Aden Rage Jualai, 2012 kuwa ‘anaipeleka Simba katika anguko kubwa’ na hiki ndicho kinachoendelea kutokea.

SIMBA walimpa kazi Omog kwa sababu ni rafiki wa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo wakati akipewa nafasi iliyokuwa imeachwa wazi Dylan Kerr. Omog anaweza kuwa amefanikiwa kwa maana ya kushinda mataji akiwa AFC Leopard ya Congo Brazaville, na Azam FC lakini ukiniambia kocha ambaye Simba ilipaswa kumsaini ni Mganda, Jackson Mayanja chini yake Salum, Mayanga.

Mayanja alishathibisha ubora wake wakati aliposhika kwa muda nafasi iliyoachwa wazi na Kerr. Kama si sababu za kiutawala Mganda huyu angeipa Simba taji la VPL msdimu uliopita. Alishinda game 7 mfululizo huku timu ikicheza vile alivyotaka yeye.

Kumleta Omog ilikuwa ni sawa na kuanza upya kabisa huku mifumo yake ikihitaji wachezaji wapya zaidi na bahati mbaya alikuta timu imeshasajili. Vuta picha kama usajili wa Simba ungesimamiwa na Mayanja na Mayanga Juni, 2016 Simba ingekuwa na kikosi cha aina gani.

Bado siwezi kumsema kabisa Omog kwa sababu kama kocha amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kulingana na namna hali ilivyokuwa wakati akichukua kibarua hicho, ila naamini Mayanja na Mayanga wangekuwa mbali zaidi kama wangepewa timu hiyo.

UTAWALA

Nilisema kati ya fimbo zangu tatu za kuiangusha Simba msimu huu-utawala niliuzungumzia kama sababu ya kuanguka. Licha ya kwamba katika sababu zangu mbili za mwanzo uongozi unahusika ila hapa nitazungumzia ni kwa namna gani unahusika kuiangusha timu ndani ya uwanja.

Furaha yote ya Simba imeishia katika mchezo wao wa kwanza tu walipotembelea kanda ya Ziwa. Licha ya watawala wote hao kuambatana na timu Kagera-walichapwa 2-1 na wenyeji wao Kagera Sugar, wakashinda kiajabu vs Mbao FC, wakaangusha pointi mbili mbele ya Toto Africans.

‘Uongozi ni matendo si kujionesha’ inashangaza sana kuona msemaji wa klabu hiyo anaitisha mkutano na waandishi wa habari halafu anazungumzia kuhusu ‘ukabila’ Hii ni sumu ambayo haipaswi kutumika katika nchi yetu. Kuzaliwa mjini si kujua kila jambo. Kama unafahamu ukubwa wa Simba kwanini sasa wewe mwenyewe unaenda mbele ya wanahabari na kuzungumzia ukabila?

Kushindwa kutoa kauli yoyote rasmi kwa uongozi wa Aveva kuhusu kile alichokisema Haji Manara ni sawa na kuiaminisha jamii kuwa uongozi wa timu hiyo ulimtuma Haji kuzungumzia ukabila, na kama ni hivyo basi hilo ni kosa kubwa ambalo wamelifanya na kwa hakika linathibitisha kile nisemacho mara kwa mara kuhusu watu hao wanaoongoza klabu kama ‘genge la wahuni’

Msimu uliopita Manara huyu huyu anayejiita mtu wa mpira alishinikiza timu yake isicheze hadi Yanga na Azam FC wacheze michezo yao ya viporo. Nilishangaa sana kwa sababu Simba ilikuwa katika moto na kila timu ilikuwa inahofu kukutana nao. Leo hii Manara huyuhuyu anatupa ‘shimoni’ Simba katika wakati mbaya, lakini maalumu kwa wapinzani wao katika ubingwa. Simba wamepata matokeo stahili ndani ya uwanja na hawawezi kunyimwa haki yao mezani kama wangefuata kanuni.

Simba hawakuwa na sababu ya kusema yote waliyosema kupitia Manara, kitendo cha uongozi wa klabu kukaa kimya hadi sasa ni ishara kuwa ‘msimu kwao umeishia’ kanda ya Ziwa ndiyo maana walijaribu kulazimisha kupata pointi za ‘mezani’ wakati walipoteza uwanjani.

Wiki iliyopita nilisema, ‘muda’ ni suala lililowaangusha Polisi Dar FC wakati walipokata rufaa ‘nje ya muda’ kupinga ushindi wa 2-0 ambao Simba waliupata dhidi yao ndani ya uwanja. Polisi Dar FC walitaka ushindi baada ya Simba kumchezesha mchezaji Novalty Lufunga akiwa ndani ya adhabu ya kutumikia kadi nyekundu katika michuano ya FA Cup.

Nilisema, rufaa ya Simba dhidi ya Kagera kuhusu kadi tatu za njano za Mohamed Fakhi ilikuwa ‘nje ya muda’ hivyo haikuwa na nguvu tena japo kuna baadhi ya watu walibadilisha ukweli huo kwa maslai yao binafsi. Simba walifahamu kuwa walipeleka rufaa bila ada ya rufaa na ilikuwa nje ya muda, sasa kitu gani kilimfanya Manara ( Mr. Povu) kulalamika wanaonewa.

Nilimsikia aklisema kuna kiongozi wa juu wa TFF alijaribu kuzuia maamuzi ya Kamati ya saa 72 ambayo iliwapa ushindi wa mezani vs Kagera. Mimi nadhani mtu huyo mkubwa wa TFF alijaribu kuzuia kwa sababu alijua kanuni zimekiukwa hivyo hakutaka itangazwe ili kuhofia kutokea mkanganyiko kama uliopo sasa.

Manara kama unajua Simba ni kubwa, basi ‘umeitukanisha’ klabu kubwa kwa jamii na bila kuomba radhi wewe ‘ni mkabila’

Hata kama ni mimi ningekuwa katika nafasi ya Mohamed Dewji ningeanza kujiuliza ni kwanini timu imeshindwa ndani ya uwanja licha ya kujitolea kiasi kikubwa cha pesa. Ningekuwa katika nafasi ya MO Dewji ningejiuliza, huyu Manara aliisemea klabu au? na kutafakari kauli yake ‘ya kikabila’ na kutazama kuhusu ufadhili wangu na faida zinazopatikana klabuni.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here