Home Kitaifa Simba wameshaanguka, TFF hatari zaidi kwa Yanga katika mbio za taji la...

Simba wameshaanguka, TFF hatari zaidi kwa Yanga katika mbio za taji la 3 mfululizo VPL

58150
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

KAMATI ya masaa 72 inajaribu kuingilia matokeo ya ndani ya uwanja na kumaliza mbio za Simba SC kurejesha ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo.

Ni ‘aibu’ kwa watu wa Kamati hiyo kutoa uamuzi wa upendeleo kwa timu ya Simba na kuyageuza matokeo ya ndani ya uwanja Kagera Sugar FC 2-1 Simba na kuwa Kagera 0-3 Simba.

Kwa jinsi suala hili la Kagera kupokwa ushindi wao katika ‘kamati ya kahawa’ lilivyo hakuna sababu ya kujisumbua kuhusu kuzungumzia kanuni kwa maana kanuni zilishavunjwa na ‘kamati hiyo ya mama nibebe mwanao.’ Kinachopaswa kufanywa na wadau wa mpira ni kupaza sauti zao na ‘kusema Kagera hawajatendewa haki.’

Nini maana ya kamati ya masaa 72?

Kama mwenyekiti wa kamati hiyo atatoka hadharani na kusema kwanini kamati yake ilishindwa kutoa uamuzi wa malalamiko ya Simba ndani ya saa 72 kuhusu mchezaji Mohamed Fhaki kucheza mchezo wao dhidi ya Kag era akiwa na kadi 3 za njano atakuwa ‘matatizoni.’

Nadhani uamuzi wa malalmiko ya Simba ulipaswa kutolewa uamuzi ndani ya siku tatu baada ya malalamiko kufika mezani kwao. Siku 3 ni sawa na masaa 72 na maana halisi ya kamati ya masaa 72 pale TFF ni kutoa uamuzi wa haraka kuhusu malalamiko yanayowasilishwa kwao.

Kama ripoti ya mwamuzi wa mchezo inapaswa kuwasilishwa Bodi ya ligi ndani ya masaa 48-siku mbili baada ya mchezo, kulikuwa na ulazima gani sasa kwa kamati ya masaa 72 kushindwa kutoa uamuzi?

Jibu ni kwamba ripoti hizo hazikufika Bodi ya ligi ndani ya muda ambao waamuzi na wasimamizi wa mechi walipaswa kuwasilisha. Mwamuzi kushindwa kuwasilisha ripoti yake ndani ya siku mbili baada ya mchezo husika, kikanuni ni makosa na Bodi ya ligi inapaswa kumuondoa katika orodha ya kuchezesha.

Kwa nini waliendelea kuchezesha? Lakini hilo halikufanyika kwa waamuzi hao walioshindwa kuwasilisha ripoti ya michezo lalamikiwa ndani ya masaa 48.

Niwaambie tu, ‘Muosha, huoshwa’. Kama ‘mlishangilia’ sana wakati ule Polisi Dar FC waliponyimwa ushindi wao wa haki dhidi ya Simba baada ya Novalty Lufunga kuchezesha mchezo wa hatua ya 32 bora katika FA Cup akiwa na kadi nyekundu, suala lililowanyima haki ni ‘MUDA.’

Japokuwa Maafande hao walipaza sauti zao katika vyombo vya habari na kusema walipeleka rufaa yao kudai ushindi dhidi ya Simba ndani ya muda mwafaka. Lakini majibu ya kamati iliyowahuku walisema rufaa ya Polisi Dar FC ilishindwa kutokana na muda. Simba wakashinda kesi na kuendelea mbele ya michuano kutokana na ushindi wao wa 2-0 walioupata ndani ya uwanja.

Wakashangilia sana kuishinda haki ya timu nyingine. Sasa ni wakati wao wa kushindwa, na muda ni suala la kwanza. Muda ambao ripoti za waamuzi wa michezo lalamikiwa ziliwasilishwa Bodi ya ligi mara baada ya michezo husika kumalizika.

‘Kamati ya Mama nibebe mwanao’ inasemekana ilifanya ujanja katika tarehe za rufaa ya Polisi Dar FC na mtindo huo ndiyo ulipelekea kamati ya masaa 72 kushindwa kufanya kazi yao ndani ya muda.

Bila Yanga kuwahi kusema hadharani mchezo uliokuwa ukichezwa amini Kagera ingepoteza pointi lakini sasa Simba haiwezi kuzipata tena, huku suala la ‘MUDA’ likiwaangusha japo liliwabeba vs Polisi Dar FC.

Kuyumbishwa kote huku kwa kanuni kuna maana ya ‘RUSHWA.’ Kuna upande unarubuni upande mwingine ili mahala fulani wapate faida. ‘Kama rais wa TFF ni msafi’ atoe ruhusa ya TAKUKURU kuchunguza kuhusu kukiukwa mara kwa mara kwa kanuni maana ndiyo kuna haribu mchezo wa soka.

Yanga nao wanapaswa waelewe wanapambana na timu mbili na zote haziko tayari kuona wanashinda taji la 3 mfululizo la VPL. Simba ni washindani wao wa karibu ‘wanaoonekana’ na timu ya ‘Kamati fulani ya kahawa’ inayopenda kujifungia katika ofisi za TFF.

Timu hii haionekani uwanjani na inaongoza ligi kwa alama tano zaidi, haijulikani inapofanyia mazoezi lakini inavaa jezi zinazoshahabiana na zile wanazotumia wapinzani wao wa karibu wanaoonekana machoni mwetu.

Matokeo ya Kagera 2-1 Simba yanapaswa kubaki kama ilivyokuwa Polisi Dar FC 0-2 Simba japo Simba wanapaswa kuwa mshindwa wa kila mechi.

Simba wameshaanguka, TFF hatari zaidi kwa Yanga katika mbio za taji la 3 mfululizo. Hawataki kuona Yanga inashinda taji hilo moja kwa moja wakati si kitu kigeni. Endeleeni kughushi email na PiiiPiii wenu.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here