Home Kitaifa Jicho la 3: Si kila timu inaweza kununuliwa, ila nilichokiona Mbao 2-3...

Jicho la 3: Si kila timu inaweza kununuliwa, ila nilichokiona Mbao 2-3 Simba ni…

40875
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

KWANZA niwapongeze Simba SC. Kutoka nyuma 2-0 hadi dakika nane kabla ya kumalizika kwa mchezo, kisha kushinda 3-2 baada ya dakika 90 ni jambo la kujivunia kama timu. Hasa ukizingatia walikuwa ugenini dhidi ya Mbao FC ambao tayari walishawaangusha vigogo kama Azam FC na Mtibwa Sugar katika uwanja wa Kirumba, Mwanza.

MBAO FC

Walikaribia kupata ushindi wao wa nane msimu huu baada ya kuongoza 2-0 hadi dakika ya 82, lakini mbinu zao za kujilinda katika kipindi cha pili hazikusaidia kutokana na kukosa ‘ustahimilivu.’

Katika kipindi cha kwanza timu hiyo ya Mwanza ilifanikiwa kudhibiti kiungo na jambo hilo lilipelekea Simba kushindwa kucheza mchezo wao uliozoeleka-kutafuta goli wakitokea katikati ya uwanja huku wakipasiana pasi fupifupi.

Salmin Hoza, mfungaji wa goli la kwanza, George Sangija, Boniface Maganga na Pius Buswita waliweza kucheza mchezo wa nguvu na pasi za uhakika kwa dakika 30 za mwanzo na kuwafanya viungo wa Simba, Mghana, James Kotei, Mzamiru Yassin na Mohamed Ibrahim kutumia muda mwingi kukaba badala ya kupanga mashambulizi.

Mchezo wa nguvu kuanzia kwa walinzi, Mghana, Asante Kwassi, Mrundi, Yusuph Ndikumana, Vicent
Phillipo na David Mwasa ulikisaidia sana kikosi cha kocha Mrundi, Ettiene. Nawasifu Mbao kwa mchezo mzuri wa kushambulia na kuzuia kwa uhakika.

Na siwezi kuwalaumu kwa kushindwa kupata walau alama moja katika mchezo huo kwa maana walicheza kadri ya uwezo wao, walijitolea lakini mwisho wa siku wakapoteza mechi kutokana na ubora wa kimbinu wa wapinzani wao.

SIMBA SC

Nilishangazwa na uamuzi wa kocha Joseph Omog kuwaanzisha nje washambuliaji Ibrahim Ajib na Laudit Mavugo. Kitendo cha kuruhusu goli la kwanza dakika ya 19 na aina ya mchezo waliokuwa wakicheza Mbao nadhani kulimshtua kocha huyo wa Simba na yeye mwenyewe alijutia kosa lake la kuwapanga Pastory Athanas na Juma Liuzio katika safu ya mashambulizi.

Washambuliaji hao walishindwa kufanya jambo lolote, walishindwa kukaa na mpira, walishindwa kujipanga katika maeneo ambayo yangewarahisishia kutengeneza nafasi za kufunga. Walikuwa wakimya sana uwanjani na utulivu wao ukawapa uhuru walinzi wa Mbao kuanzisha vizuri mashambulizi ya timu yao wakitokea nyuma.

Kumtoa Pastory na kumpa nafasi kiungo Said Ndemla mara baada ya kufungwa goli la kwanza ulikuwa ni uamuzi mzuri lakini haukusaidia kitu kwa sababu Mbao waliendelea kucheza kwa kasi ileile tu, huku
Simba ikionekana kukosa mshambuliaji ambaye angeweza kuwafanya walinzi wa Mbao kutopanda mara kwa mara ndiyo maana wakaruhusu goli la pili dakika ya 34.

Kumpumzisha mlinzi wa kulia Ahmad Juma dakika ya 36 na kumpata nafasi Mavugo ilikuwa ni badiliko sahihi lakini bado mipira ilishindwa kukaa mbele na jambo hilo liliwapa wakati mgumu viungo na walinzi wa Simba.

Omog alikosea katika upangaji wa timu yake lakini badiliko la mwisho alilofanya robo saa ya mwisho ya mchezo kwa kumpumzisha Liuzio na kumpa nafasi Muivory Coast, Blagnon liliimaliza Mbao.  Nadhani aligundua ugumu wa timu yake kupata goli kama wangeendelea kucheza mchezo wa pasi fupifupi.

Kwa kutambua uwezo wa mshambuliaji wake huyo katika uchezaji wa mipira ya juu ndio kulimpa mafanikio.

Blagnon alifunga kwa kichwa cha kuparaza akimalizia mpira mrefu uliopigwa na
Kotei dakika ya 83, na akamalizia kwa ustadi mpira ulioshindwa kudhibitiwa na golikipa wa Mbao, Erick Ngwegwe dakika ya pili ya nyongeza kufuatia mpira mwingine mrefu uliopigwa na mlinzi, Besala
Bokungu.

Mipira ya juu ilionekana kuwasumbua sana Mbao ndio maana kila walipookoa haikuwa ikienda mbali. Mzamiru akatumia faida hiyo kufunga goli la ushindi katika dakika ya 6 ya nyongeza baada ya walinzi wa Mbao kushindwa kuondoa vizuri mpira uliokuwa ukizagaa katika eneo lao la hatari.

SI KILA TIMU INANUNULIWA

Wakati mwingine inabidi tukubaliane na ukweli kuwa soka ni dakika 90. Msimu wa 2011/12 Manchester United walitumia dakika 30 za mwisho kutoka nyuma 3-0 na kutengeneza sare ya 3-3 vs Chelsea katika uwanja wa Stamford Bridge, Simba ilitoka nyuma 3-0 na kutengeneza sare ya 3-3 vs Yanga SC msimu wa 2013/14 na hakuna aliyewahi kusema mechi hizo ziliuzwa zaidi ya kuwasifu Manchester United na Simba kutokana na kusawazisha magoli yote matatu.

Sasa kipi kinawafanya baadhi ya watu kusema kipa wa Mbao aliibeba Simba? Makosa ya wachezaji ndani ya uwanja ndio yanaleta tofauti katika mechi na lazima yafanyike. Mbao hawawezi kuuza mechi huku ukizingatia wapo katika nafasi mbaya katika msimamo.

Ni matokeo tu ya mchezo na hata Yanga walifanya makosa wakati walipofungwa na Simba pungufu mchezaji mmoja wakati waliongoza mechi kwa dakika 70. Je, Yanga nao waliwauzia Simba?

Si kila timu ina uza mechi, matokeo mengine yanatokea kwa sababu za kimpira tu. Simba walijituma sana na kuboresha mbinu zao katika kipindi cha pili ndiyo maana wakapata matokeo.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here