Home Kitaifa Mbaraka Yusuph, Singano, Mkude na nyota hawa watano wataipaisha zaidi Yanga…

Mbaraka Yusuph, Singano, Mkude na nyota hawa watano wataipaisha zaidi Yanga…

29115
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

KABLA ya kuanza ‘kutupa macho’ sehemu nyingine, kocha George Lwandamina anapaswa kuangalia ni wachezaji gani wanapaswa kusajiliwa tena na Yanga SC miongoni mwa wale waliopo kikosini hivi sasa.

Kwa mtazamo wangu, Yanga inahitaji kufanya usajili wa beki namba tatu, viungo wawili wa mashambulizi, mmoja wa ulinzi, viungo wawili wa pembeni-kulia na kushoto, na washambuliaji wawili watakaokuwa na uwezo wa kucheza eneo lote la mbele kwa usahihi.

Lakini kabla ya kusaini wachezaji wapya ningependa kuona kocha Lwandamina akiwasaini tena mlinzi wa kati, nahodha Nadir Haroub ambaye ameendelea kuonesha uwezo wake wa kuzuia, kuipanga safu ya ulinzi na kuongoza mchezo.

Licha ya umri wake wa miaka 33, Nadir ni mchezaji ambaye anatengeneza umoja wa ndani na nje ya uwanja kwa timu yake na kiwango chake katika kila mchezo anaopata nafasi kimekuwa juu. Anajituma muda wote na hajaonesha kuridhishwa na mafanikio na aliyopata klabuni hapo tangu alipojiunga 2006 akitokea Zanzibar.

Kuna wachezaji wengine ambao mikataba yao inamalizika mara baada ya msimu huu kumalizika.
Naamini kocha huyo raia wa Zambia atakuwa anafuatilia kwa umakini viwango vya Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Mtogo Vicent Bossou, Said Juma Makapu, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mzimbabwe, Thaban Kamusoko, Matteo Anthony.

Pia , Geoffrey Mwashuiya, Deus Kaseke, Mzimbabwe, Donald Ngoma, Mrundi, Amis Tambwe, Malimi Busungu ambao mikataba yao inakaribia kumalizika na ni yeye atakayeamua ni wachezaji gani wasajiliwe tena na wapi waachwe.

GADIEL MICHAEL

Yanga haina tabia ya kusaini wachezaji kutoka Azam FC lakini wanaweza kuimarisha beki yao kwa kumsaini mlinzi huyu wa kushoto wa Azam FC.

Gadiel anauwezo wa kupeleka mashambulizi mbele, pia ni mwepesi kurudi katika nafasi yake. Hapotezi hovyo mipira na amekuwa na umakini mkubwa kila anapokuwa uwanjani. Huyu ni mchezaji ambaye ataimarisha safu ya beki wa kushoto ambayo sasa inashikiliwa na Mwinyi  na Oscar Joshua. Lwandamina anapaswa kumfuatilia kijana huyu.

JONAS MKUDE

Bado hajasaini mkataba mpya katika klabu yake ya Simba SC na kufikia mwisho wa msimu atakuwa huru kujiunga na timu yoyote atakayokubaliana nayo. Kuwa na Justine Zulu na Makapu ni vizuri lakini Mkude ataongeza nguvu, ufundi na uwezo wa idara ya kiungo kupanga mashambulizi ya uhakika wakitokea katikati ya uwanja.

Naamini Lwandamina ameshamwona mara kadhaa nahodha huyu wa Simba, kama anapatikana kiurahisi Yanga inapaswa kumsaini katika usajili ujao ili kuimarisha kiungo chao chenye mapungufu. Mkude ameshapevuka kimchezo na sasa yuko katika kiwango kizuri. Ataimarisha sehemu ya kiungo mlinzi na Yanga inamuhitaji mchezaji mkomavu kama nahodha huyu wa Simba.

RAFAEL DAUDI, KENNY ALLY  

Wanacheza vizuri katika kiungo cha timu ya Mbeya City FC. Wachezaji hao wawili wanaweza kuongeza ubunifu katika timu ya Lwandamina endapo watasajiliwa. Wote wawili wana uwezo wa kucheza
nafasi zote katika eneo la kiungo na kufanya vizuri.

Niyonzima, Kamusoko ni viungo wazuri ila wanapokosekana timu imekuwa ikiyumba sana eneo la kiungo. Kuwasaini nahodha wa City, Kenny na Alpha si tu kutaongeza viungozi katika timu bali uimara na ubora. Lwandamina anaweza kuwatazama vizuri wakati atakapokutana na kikosi cha City katika mchezo wa marejeano mwezi huu.

HASSAN KABUNDA

Ni kiungo mzuri wa pembeni na amekuwa na misimu miwili ya kuvutia katika kikosi cha Mwadui FC. Licha ya uwepo wa Juma Mahadhi na Msuva katika wing ya kulia, Kabunda ni mchezaji ambaye anaweza kuifanya Yanga kutengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga kutokana na uwezo wake wa kupiga pasi
sahihi katika wakati mwafaka.

RAMADHANI SINGANO

Katika michezo ya karibuni kiungo huyu mshambulizi wa kushoto wa klabu ya Azam FC amekuwa katika kiwango bora sana. Atakuwa huru mara baada ya kumalizika kwa msimu huu. Lwandamina ameshamuona Singano na ukitazama kikosi chake utaona kabisa kuwa Yanga inamuhitaji mchezaji kama Singano ili kuleta balansi ya mashambulizi kutoka kila upande.

Mwashuiya ni mchezaji mzuri lakini bado Yanga inamuhitaji kiungo aliyepevuka zaidi katika wing yao ya
kushoto na Singano ndiye mtu sahihi kwa wakati huu.

IBRAHIM AJIB

Anamaliza mkataba wake klabuni Simba mara baada ya msimu kumalizika. Yanga hawapaswi kujivunga zaidi ya kujitosa kuwania saini ya mshambulizi huyo kijana mwenye uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga magoli. Ajib atakuwa msaada mkubwa kwa Tambwe, Ngoma na Mzambia, Obrey Chirwa kama Lwandamina atapendekeza watatu hao wote kuendelea kuichezea Yanga msimu ujao.

MBARAKA YUSUPH

Si kutokana na magoli yake matatu katika michezo mitatu vs Yanga na Simba, bali uwezo wake wa kufunga, kumiliki mpira, kutengeneza nafasi na target yake anaposhuti mpira kuelekea golini. Yusuph ameshafunga magoli 11 katika VPL msimu huu. Huyu anaweza kuibeba Yanga na anakidhi vigezo vya kuvaa jezi ya timu hiyo.

Naamini wachezaji hawa nane niliowataja wanaweza kuifanya Yanga kuwa moto zaidi msimu ujao na wanapatikana kiurahisi kutokana na kwamba mikataba yao inafikia tamati mwishoni mwa msimu
huu.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here