Home Kimataifa Soka La Basque; Jimbo Linaloleta Mapinduzi Ya Kisoka Hispania.

Soka La Basque; Jimbo Linaloleta Mapinduzi Ya Kisoka Hispania.

2701
0
SHARE

Katika hali ya ajabu kabisa, lakini ikiwa imesalia miezi miwili La Liga kufikia kikomo msimu huu, timu zote 4 kutoka Basque zipo kwenye kinyang’anyiro cha kufuzu michuano ya Ulaya, mapinduzi ya ajabu ukizingatia eneo hilo lina watu milioni 2 pekee.

Vilabu vinavyotokea kwenye jimbo hilo na ambavyo vinasaka nafasi za Ulaya ni Alaves, Eibar, Athletic Club na Real Sociedad, huku hiyo ya mwisho ikiwa tayari katika nafasi ya 6 ambayo inawaruhusu kuingia Europa, vinavyobaki vipo jirani kabisa na kutwaa nafasi hizo.

Inawezekana kabisa, Alaves wakafuzu michuano ya Ulaya iwapo wataifunga Barcelona kwenye mechi yao ya fainali ya Copa del Rey ambayo ni mara ya kwanza wanafika fainali. Uwezekano upo kwani waliifunga Barcelona kwenye mchezo wa ligi pale Camp Nou. Ingawa hata wasipofanikiwa kushinda itamaanisha nafasi ya 7 itapeleka mwakilishi Ulaya ambayo bado inapiganiwa na Athletic Bilbao waliopo mbele ya Eibar kwa pointi 3 na Alaves kwa pointi 4.

Inakuwaje sasa vilabu hivi vya eneo moja vinafanikiwa hivi?

Mafanikio yao haya hayajatokana na bahati, bali ni mipango endelevu na yenye kueleweka ya muda mrefu ndio imewafikisha hapa.

Kifedha, akaunti za vilabu hivi vinne zipo chini; Eibar na Alaves wapo chini ya nusu ya vilabu vyenye fedha nchini humo, huku  Athletic na Real Sociedad vikiwa na ziada kiasi.

Kwa upande wa ufundi, vilabu vyote vinaonekana vilipatia kuchagua makocha wenye muono wa mbali na siku zote kuwapatia nafasi ya pili.

Athletic Club na Real Sociedad waliamua kuwaamini Ernesto Valverde na Eusebio baada ya kuonekana kufanya vibaya kwenye vilabu vya Valencia na Barcelona B.

Huku Eibar, Jose Luis Mendilibar aliletwa baada ya kuwa ametimuliwa na klabu ya Levante na ni wazi kuwa ubora na matunda kwa upande wa Eibar (Los Armeros) umepanda huku Levante wakishuka daraja.

Lakini ukishuka zaidi katika uwanja wa Estadio Mendizorrotza, Alaves wao walichukua maamuzi magumu ya kumfukuza kocha Jose Bordalas baada ya kuwapandisha daraja msimu wa 2015/16.

Uongozi wa klabu ulitambua kuwa falsafa yao ya soka ilikuwa ngumu kiasi na kulikuwa na matokeo mengi sana ya ushindi mwembamba wa 1-0, hivyo nafasi yake wakampa kocha aliyeonekana hafai Valencia, Mauricio Pellegrino, ambaye amewapa zawadi ya fainali ya kombe la ligi na kuwaweka kwenye nafasi salama kwenye msimamo wa ligi kuu.

Hatimaye matumizi ya vijana yakalipa pia. Huku vilabu vya Eibar na  Alaves vikinufaika na matumizi ya wachezaji bora vijana waliokuja kwa mkopo, kwa upande wa Athletic na Real Sociedad wanamiliki moja ya akademi mbili bora nchini Hispania.

Ukweli kuwa wachezaji 7 kati a 20 walioitwa kwenye kikosi cha vijana cha Hispania maarufu kama La Rojita wanatoka kwenye vilabu vya jimbo la Basque inajieleza kuwa wanafanya vyema likija suala la vijana.

Ni wazi kuwa, katika hili inabidi uitaje klabu inayoshikilia mkia ya Osasuna, klabu ya Navarre ambayo ni sehemu ya Greater Basque lakini haifanyi vyema msimu huu.

Hata hivyo kitendo cha wao kurejea hata ligi kuu msimu huu ilikuwa ni mafanikio yaliyopitiliza kutokana na ukosefu wa rasilimali na ukata walionao.

Kupanda kwao daraja msimu uliopita ilimaanisha kuwa jimbo la Basque kwenye masuala ya soka limebeba imani za waliokuwa wengi kuwa nyakati bora zinakuja hasa kutokea Kaskazini mwa Hispania.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here