Home Kitaifa Uchambuzi wa Shaffih Dauda baada ya mechi ya klabu bingwa Afrika Yanga...

Uchambuzi wa Shaffih Dauda baada ya mechi ya klabu bingwa Afrika Yanga vs Zanaco

12869
0
SHARE

Yanga wameshindwa kupata matokeo ya ushindi kwa mara ya pili mfululizo kwenye uwanja wa taifa katika michuano ya klabu bingwa Afrika msimu huu.

Yanga ililazimisha sare ya kufungana goli 1-1 na N’gaya Club ya Comoro baada ya kutanguliwa na klabu hiyo lakini badae Haji Mwinyi akasawazisha.

Jana Jumamosi March 11, 2017 Yanga imelazimishwa tena sare ya kufungana 1-1 na Zanaco ya Zambia baada ya mwanzo kuongoza kwa goli lililofungwa na Simon Msuva.

Katika kipindi cha michezo cha Sports Extra cha Clouds FM, Shaffih Dauda ambaye ni mchambuzi katika kituo hicho alitoa mtazamo wake wa kilichopelekea Yanga kulazimishwa sare na Zanaco na kujiweka kwenye mazingira magumu ya kulazimika kupata ushindi ugenini Zambia licha ya kuwa wanaweza kufanya wakafanya hivyo.

Shaffih amezungumzia sana eneo la viungo wa Yanga ambapo jana walicheza Justine Zulu, Kelvini Yondani na Thabani Kamusoko kama viungo wa kati.

Kwenye eneo la kiungo la Yanga kulikuwa na wachezaji watatu wanaocheza katika nafasi moja, Kamusoko tumezoea kumuona akicheza kama kiungo wa nyuma, Zulu ‘Mkata umeme’ vilevile ni kiungo wa chini na Yondani ambaye pia alikuwa anacheza kama kiungo wa chini kwenye mchezo dhidi ya Zanaco.

Watatu hao walikuwa na majukumu yanayofanana hali iliyopelekea kugongana mara kwa mara, kukawa hakuna movements za mpira kutoka eneo la chini la Yanga kwenda eneo la kuwashambulia Zanaco.

Simon Msuva na Obrey Chirwa kwa sasa ndiyo wachezaji ambao wako physically fit kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na wachezaji wengine wakawa wanalazimika kutumia uwezo wao binafsi natimaye ukasaidia Yanga kupata bao kupitia kwa Msuva.

Lakini hakukuwa na muunganiko mzuri kutoka nafasi ya ulinzi ya Yanga kwenda mbele kwa sababu nafasi aliyokuwa anacheza Yondani na wenzake walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, kulitakiwa kuwe na mtu mwenye kazi ya kupokonya mipira na kufanya vurugu ili kuwanya Zanaco wasicheze kwa uhuru, mwingine alitakiwa kuchukua mipira iliyopokonywa na kupiga pasi nzuri kwa wachezaji wa mbele.

Kilichokuwa kinakosekana katikati ni mgawanyo wa majukumu, nani mwenye majukumu gani kwa wakati upi na mwingine afanye nini mwisho wa siku wakajikuta wanafanya majukumu yanayofanana kwa wakati mmoja. Wakatoa mwanya kwa Zanaco kutawala game na kuwashambulia sana Yanga, muda mwingi Yanga wakajikuta wakiwazuia Zanaco na unaweza kufikiri Zanaco walikuwa wanacheza kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Sikuona kama kulikuwa na ulazima wa kumpanga Donald Ngoma kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kwa sababu ndio kwanza ametoka kwenye majeraha ya muda mrefu hajapata mechi yoyote halafu akaanza kwenye mechi ngumu ya kimataifa.

Ngoma alikuwa muoga kwenye matukio mengi ambayo alikuwa anakutana one against one na wachezaji wa Zanaco kwa sababu bado anacheza kwa tahadhari kubwa akihofia kuumia tena, kwa hiyo hakuwa na mchango mkubwa kwenye mechi hiyo nadhani kama mwalimu alikuwa anakata kumtumia kwenye mechi ijayo ya ugenini basi ingekuwa vizuri kama angempa nafasi ya kuingia kipindi cha pili kwenye mechi ya hapa.

Kukosekana kwa kiungo mzoefu Haruna Niyonzima  pia ilikuwa ni tatizo kwa upande wa Yanga, Niyonzima ni mchezaji mwenye uwezo wa juu wa kuituliza timu na kupiga pasi za mwisho wakati timu inashambulia lakini ni mchezaji mwenye uzoefu na mashindano ya kimataifa kwa sababu ya ukongwe wake.

Mimi nikafikiri labda Yanga wameamua kutumia mbinu kama walizotumia kwenye mechi zao mbili dhidi ya N’gaya ya Comoro kwamba wanajilinda sana wakiwa nyumbani kuzuia kufungwa halafu wanapokwenda ugenini wanajiachia zaidi. Tulishuhudia Yanga ikipata ushindi wa magoli 5-1 ugenini Comoro lakini walipocheza nyumbani wakatoka sare ya 1-1 kwa hiyo tusubiri kuona kama Yanga wanaweza kupata matokeo wakiwa ugenini Zambia.

Yanga imekuwa na tatizo la kushindwa kulinda ushindi wao pale wanapoamua kufanya hivyo, mara kadhaa wamejikuta wanasawazishiwa pale wanapokutana na timu wanazolingana nazo uwezo. Dakika ambazo wanaruhusu magoli zimekuwa hazina tofauti sana walisawazishiwa goli na Simba kwenye mchezo wao wa ligi raundi ya kwanza goli ambalo lilifungwa dakika za majeruhi.

Wakaruhusu magoli mawili dhidi ya Simba dakika zilezile kwenye mechi yao ya raundi ya pili, jana wamesawazishiwa goli na Zanaco dakika zinazofanana na mechi zilizopita.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here