Home Kitaifa Kama ulipitwa na ‘Ngumu Kumeza’ ya Sports Extra

Kama ulipitwa na ‘Ngumu Kumeza’ ya Sports Extra

8740
0
SHARE

Dhamira inaweza kuwa nzuri ila matendo yakakuangusha, ni fikra zilizonijia muda mfupi baada ya Mh. Waziri alipotaja kamati ya kuhamasisha Serengeti Boys pamoja na ile itakayosaidia kuhamasisha upatikanaji wa fedha za maandalizi ya michuano ya Olympic ya mwaka 2020.

Pamoja na vyama vyote kutaja dira ya kuelekea michuano hiyo, nilisikitika pale nilipogundua TFF haijajua hadi leo inakwenda vipi kwenye michuano hiyo, pembeni namsikia jamaa mmoja anasema, “mwaka wa uchaguzi huu, acha uchaguzi upite kwanza utawala mpya ndio utajua tunaingiaje kwenye michakato hiyo.”

Nahisi mwili umepata joto natoka nje kupata hewa, na hapo nakutana na mchezaji wa zamani wa Ushirika-Moshi anaanza kwa kuniambia,“TFF haijitambui kwenye mambo mengi tu achana na hilo alilotaja Waziri”, anasema bora hata ya hiyo dira wameshindwa kuiwasilisha kwa Waziri maana hawakawii kuigeuka. Kama walituaminisha kwenye maboresho mwaka wa kwanza walipoifanya, sasa hivi ile program imeishia wapi au pia ilikuwa ya kutoa shukrani kwa wajumbe waliokuwa karibu na uongozi enzi zile wanaingia madarakani na wajumbe wakapata fursa ya kutawanywa mikoani kutafuta wachezaji?

Baada ya pale kamati zote zimegeuka kuwa hatarishi kwa Rais wa TFF pamoja na kamati yake ya utendaji, mimi namwambia nimeshangazwa na ratiba ya kombe la FA. Mwanzoni walikurupuka kupanga ratiba juma nne ili Alhamisi timu zicheze wakasema moja ya kanuni ni timu za karibu kucheza, kweli Yanga wakaitoa Ashanti United, Simba ikawatoa Polisi Dar es Salaam kwa magumashi na timu za mikoani zikafanya hivyohivyo kwa timu walizokuwanazo karibu.

Hatua iliyofuata, Yanga wakacheza na wakaribu yao Kiluvya FC, Simba wao wakacheza na wakaribu yao African Lyon, Mbao dhidi ya Toto Africans, Mtibwa Sugar na Azam, Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons.

Sasa kwenye robo fainali kanuni inaonekana kuwa ngumu kutumika kwa kuhofia kuharibu mipango ya fedha, Simba timu waliyo karibu nayo zaidi ni Yanga lakini cha kushngaza, draw ambayo hatua kama hii mwaka uliopita ilifanywa mubashara kwenye luninga, mwaka huu mtu mmoja kajifungia chumani katoka na uozo ufuatao, hivi kutoka Msimbazi hadi Arusha ni karibu kuliko Msimbazi kwenda Jangwani? Au Mbeya ni karibu zaidi kuliko mtaa wa Msimbazi? Jamaa anasema, “unataka Madini atuwakilishe kwenye kombe la shirikisho, we mtoto koma, unafikiri Madini wakicheza na Enyimba tutapata mapato ya mlangoni kweli? Au unataka fainali ya kombe la FA iwe Ndanda na Kiluvya? TFF ipate nini milangoni unataka watoto wa viongozi washindwe kwenda maliwatoni?

Mbaya zaidi mwaka huu unaweza kuwa wa mwisho kwa baadhi ya watu pale, acha tupige fedha za mwisho za Simba na Yanga kwenye FA tupate kiinua mgongo chetu.

TFF msitufanye hatufikirii jamani, mbona kanda ya ziwa mlipatia? Hapa mnakwepa mechi ya mahasimu mapema si ndio? Yule mchezaji wa zamani wa Ushirika ananiambia, ujue michuano ya FA ni mikubwa kwa vile inatoa timu zinazowakilisha nchi ila inauozo mwingi mno, timu zinacheza na hazijagawiwa fedha kama ilivyokuwa kwenye makubaliano kuna timu zinadai fedha za msimu uliopita mpaka sasa hazijalipwa zingine mpaka zimeshushwa lakini imekuwa kimya.

Kwenye madeni huwezi zisikia Simba na Yanga wala Azam, wanaokomolewa ni Geita, Kimondo na kina Mlale. Wadhamini wamekaa kimya hakuna anayehofia kuchafuliwa kwa chapa yao, wadhamini wakileta kokoro watashindwa kusaini mikataba mipya wengine watakosa 10% ya usainishwaji wa mikataba.

Jamaa anasema, TAKUKURU wanapaswa kuwa macho sana na hizi mechi za ligi zilizobaki, marefa wananunuliwa sana pia fuko la fedha linatembea utupu kwenye mechi hizi zilizobaki. Jamaa anakuja ananiambia ngoja nikung’ate sikio, utaratibu wa kununua mechi siku hizi umebadilika ndugu yangu, mechi inanunuliwa mwezi mmoja kabla watu wanakuwa wameshapewa chao na siku hizi hawanunuliwi wachezaji watatu kama zamani, siku hizi fuko la fedha lazima lipitishwe kwa wachezaji tisa vinginevyo mnaweza kupata ugumu.

Ananiambia, ushawahi kushuhudia mchezo ambao timu A inajua timu B wana hela yetu na bado wanakaza? Kumbuka mechi ya Kajumulo na Tanzania Prisons mwanzoni mwa miaka ya 2000, Kajumulo wakishinda wanacheza ligi kuu ya Muungano, nafasi hiyo wanagombea na Simba. Simba walituma mtu na fuko la box 10 Kajumulo wakaweka box sita zote zikachukuliwa na Kajumulo wakafungwa kama kawaida.

Mechi ilipoisha, wachezaji wa Tanzania Prisons wakasema “tumeshinda kama desturi ya kazi yetu inavyosema,” mbaya zaidi yule mchezaji aliyepokea fuko la fedha akakutana na mwalimu aliyetoa mlungula kwenye timu nyingine msimu uliofata, akamwambia “hutacheza hapa mpaka urudishe box sita zangu” na kweli hadi leo sijui yule mchezaji alitokomeaga wapi. Watu wa mlango mmoja hapo Mwanza, msalimieni Hemed Mrisho.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here