Home Kitaifa Jicho la 3: ‘Si Kamusoko, Lwandamina, Ndemla ndio waliipoteza...

Jicho la 3: ‘Si Kamusoko, Lwandamina, Ndemla ndio waliipoteza Yanga’

25894
0
SHARE

Na Baraka  Mbolembole

KOSA la kwanza la kocha, George Lwandamina ni kumuacha benchi nahodha, Nadir Haroub na kumuanzisha Vicent Andrew katika nafasi ya beki wa kati.

Kocha wa Simba, Joseph Omog hasingeweza kuepuka kumpanga Novatus Lufunga kama mlinzi-pacha wa Abdi Banda kutokana na majeraha ya Mzimbabwe, Method Mwajale.

Kabla ya mechi niliandika katika ‘Jicho la 3’ kwamba, Simba hawapaswi kuwaanzisha washambuliaji wake watatu, Laudit Mavugo, Juma Liuzio na Ibrahim Ajib. Pia nilisema ili ‘kujaribu’ kuifunga Yanga, Omog anapaswa kuwapanga James Kotei, Said Ndemla, Muzamiru Yassin na Mohamed Ibrahim.

PENALTI DAKIKA YA 5′

Mzambia, Obrey Chirwa alilazimisha kumpita mlinzi wa kati wa Simba, Lufunga. Akitambua fika yupo ndani ya eneo la hatari huku Lufunga akiwa nyuma yake, Chirwa alikimbia ‘kikakamavu’ lakini ‘alilegea’ na kuanguka baada ya mguu wa kushoto wa Lufunga kumgonga kwa nyuma katika mguu wake wa kushoto. Ilikuwa penalti dhahiri iliyoambatana na kadi ya njano kwa mlinzi huyo wa Simba.

MABADILIKO YA KWANZA-KUMTOA LIUZIO NA KUMPA NAFASI NDEMLA DAKIKA YA 26′

Kitendo cha kuwapanga kwa wakati mmoja Mavugo, Liuzio na Ajib ndiyo kulifungua nafasi ya Justine Zulu, Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima na Msuva kutawala kiungo cha Simba. Nilisema awali kuwa
washambuliaji hao watatu wa Simba huwa hawana msaada mkubwa kiukabaji.

Zulu alikuwa akikaba na ‘kuua’ njia zote za viungo wa Simba kupeleka pasi kwa washambuliaji wao. Kamusoko aliichezesha timu kwa kasi huku pia akiwa makini katika ukabaji, ili kuwarudisha mchezoni wachezaji wake ambao waliopotezwa na mkwaju wa mapema wa penalti, kocha Omog alichukua uamuzi sahihi ambao alipaswa kuufanya kabla ya kuanza kwa mchezo.

Kitendo cha kocha huyo kumtoa Liuzio na kumpa nafasi Ndemla dakika ya 26′ kilimpa faida kama kocha kwa kufanya mabadiliko yaliyokuwa na faida. Ndemla ni kiungo mwenye uwezo wa kupiga pasi za umbali mrefu na kuwafikia walengwa.

Baada ya kuingia kwa Ndemla, Simba ikabadilika kiuchezaji. Walipata nyongeza ya pasi ndefu zilizofika. Kotei, Muzamiru na Mohamed Ibrahim wote si wazuri katika pasi ndefu ndiyo maana walisumbuliwa sana na viungo wa Yanga kwa sababu ya uchezaji wao wa pasi fupifupi.

KUUMIA KWA THABAN KAMUSOKO DAKIKA YA 45′

Awali raia huyo wa Zimbabwe alionekana kuwa na siku njema. Lakini mambo yakaja kubadilika mara
baada ya kuingia uwanjani Ndemla ambaye aliituliza safu ya kiungo ya Yanga kutokana na mchezo wake wa kupiga pasi ndefu ambazo ziliwafanya hata wachezaji wa Yanga kuanza ‘kukimbizwa.’

Kamusoko alijikuta akitumia nguvu nyingi zaidi na jambo hilo likapelekea kujitonesha maumivu yake ya enka. Japokuwa alijikaza na kuendelea kucheza kwa dakika tano lakini kadri Simba walivyoongeza kasi katika uchezaji wao, Thaban akalazimika pia kuongeza spidi na matumizi ya nguvu jambo ambalo lilimuongezea maumivu zaidi. Dakika 15 za mwisho kuelekea muda wa mapumziko Simba walitawala mchezo.

KAMARI ILIYOZAA HASARA NA FAIDA KWA SIMBA

Dakika 6 baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, kocha wa Simba, Omog aliamua ‘kucheza kamari.’ Alimpumzisha mlinzi wa kati, Lufunga na kumpa nafasi kiungo mshambuliaji wa pembeni, Shiza Kichuya. Nadhani Omog alifanya hivyo ili kuilinda timu yake isicheze pungufu kwa kuhofu huenda Lufunga angepata kadi nyekundu.

Mlinzi wa kulia, Mcongoman Besala Bokungu akaenda kucheza beki ya kati sambamba na Banda, Muzamiru akarudishwa chini zaidi katika beki namba mbili na kwa vile katikati ya uwanja walikuwepo Mohamed Ibrahim, Ndemla na Kotei, kocha huyo hakuona hatari yoyote kumpa nafasi Kichuya kwa sababu upande wa kushoto wa Yanga haukuwa na madhara.

Dakika nne baada ya Bokungu kuhamia nafasi ya beki wa kati akalambwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea vibaya Chirwa ambaye alishamuacha mlinzi huyo wa Simba na bila kuchezewa faulo bila shaka angeenda kufunga. Kile ambacho Omog alikihofia kumtokea Lufunga kikamtokea Bokungu na kuwaacha wakibaki pungufu huku wakiwa nyuma 1-0.

ALICHOPASWA KUFANYA LWANDAMINA BAADA YA SUB YA LUFUNGA

Simba walimtoa beki na kumuingiza kiungo mshambuliaji, lengo lao lilikuwa ni kuongeza nguvu katika mashambulizi. Kama kocha huku pia timu yake ikiwa mbele, Omog alipaswa kumpa nafasi Geofrey Mwashuiya ambaye ni wing mzuri mwenye mbinu, kasi na uwezo wa kumiliki mpira.

Kwa kutambua kuwa Muzamiru ni mchezaji wa kiungo, Mwashuiya angeweza kumsumbua sana na pengine kumfanya hadi Kichuya arudi nyuma kumsaidia beki wake namba mbili.

Lakini wala kocha huyo raia wa Zambia hakuwa na habari. Kuondolewa uwanjani kwa Bokungu huku Simba wakiwa hawana mchezaji mwingine wa nafasi ya beki, Lwandamina alipaswa kumpa nafasi Emmanuel Martin na mambo yangekuwa vizuri upande wao.

Baada ya kushindwa kupanga timu yake vizuri, Lwandamina alishindwa pia hata katika ufanyaji wa mabadiliko na yale aliyoyafanya hayakukidhi ubora wa mechi na alifanya katika muda mbaya.

KOTEI, NDEMLA, KICHUYA ‘NAWAPA  TANO’

Mara baada ya kuondolewa uwanjani kwa Bokungu, Mghana, Kotei alienda kucheza katika beki ya kati sambamba na Banda. Uchezaji wake ulikuwa zaidi ya beki, alizuia na kuipeleka timu mbele kwa kasi kasha alirudi haraka katika eneo lake la ulinzi. Na alipogundua nguvu ndogo ya Yanga katika mashambulizi akaamua kucheza kama namba 6.

Huyu ni mchezaji wa ukweli. Ndemla aliendelea kuthibisha kuhusu ninachokisema mara kwa mara kuwahuyu ndiye kiungo   bora zaidi Mtanzania kwa wale wachezesha timu. Alipiga pasi zilizofika, alikaba na kuichezesha timu.

Nilipenda pia moyo wa kipiganaji wa Kichuya ambaye aliamua kuutafuta mpira kila mahali, kusaidia kukaba. Pasi yake ilizaa goli la kusawazisha na baadae akafunga goli la ushindi zikiwa zimesalia dakika 9 mchezo kumalizika.

Kutoka nyuma 1-0 huku wakiwa pungufu kuanzia dakika ya 55’ na kushinda 2-1 dhidi ya Yanga, sawa kuna vikosi vya Simba vilishafanya hivyo dhidi ya Yanga lakini ushindi huu wa juzi, niliona jitihada kubwa za wachezaji, benchi la ufundi, Simba walitumia ‘udhaifu’ na uwezo mdogo wa kocha Lwandamina katika usomaji wa mchezaji na wakashinda kwa haki.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here