Home Kitaifa INASIKITISHA: Soka la Tanzania limepoteza mchezaji mwingine, ni golikipa wa VPL

INASIKITISHA: Soka la Tanzania limepoteza mchezaji mwingine, ni golikipa wa VPL

2237
0
SHARE

Wakati soka la Tanzania likiwa bado halijasahau kifo cha mchezaji wa Mbao FC (U20) Ismail Mrisho, leo January 30, 2017 imetoka taarifa nyingine ya kifo cha golikipa wa Kagara Sugar David Buruhani.

David Buruhuni amefariki wakati akipatiwa matibabu kwenye hospitali ya Bugando jijini Mwanza.

Taarifa zinasema kwamba, golikipa huyo alianza kuumwa ghafla wakati akiwa safarini na timu yake kwenda Singida kwa ajili ya mchezo wa Azam Sports Federation Cup. Wakati wanarudi Kagera, hali yake ilizidi kuwa mbaya ndipo akakimbizwa hospitali ya Bugando.

Kwa mujibu wa chanzo chetu ndani ya Kagera Sugar, inadaiwa golikipa huyo alianza kuhusi dalili za Malaria lakini baadae ikagundulika alikuwa na tatizo kwenye ini.

“Ilianza kama Malaria, lakini walivyoendelea na vipimo wakagundua ini lilikuwa limekufa,” anasema mmoja wa viongozi wa timu ya Kagera Sugar ambaye hakupenda kutajwa jina.

“Mwili wa marehemu bado upo hospitali ya Bugando huku taratibu za kusafirisha kuelekea kwao Iringa zikiendelea.”

“Ametuachia pengo kubwa kwenye kikosi chetu, tulikuwa tunamtegemea, inauma sana lakini yote ni mipango ya Mungu.”

Kifo cha David Buruhani kimekuja siku 57 baada ya Ismai Mrisho kufariki (December 4, 2016) akiwa anaitumikia timu yake ya Mbao FC kwenye michuano ya ligi ya vijana chini ya miaka 20 kwenye uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Burhani amewahi kuvitumikia vilabu vya Mbeya City, Majimaji ya Songea na kabla ya kufikwa na mauti alikuwa akiitumikia Kagera Suga ya mkoani Kagera.

Marehemu alikuwa ni mwenyeji wa Iringa ambapo ameacha mke na watoto wa wawili.

Kwa mujibu wa ratiba ya VPL, leo January 30, 2017 Kagera Sugar inatakiwa kucheza na Mtibwa Sugar lakini uongozi wa Kagera unafanya taratibu za kuomba mchezo huo usogezwe mbele ili wapate fursa ya kukamilisha taratibu za mazishi ya golikipa wao.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here