Home Kitaifa ‘Msimamizi Majimaji vs Yanga alimwambia mwamuzi ahakikishe Yanga inapoteza mechi’

‘Msimamizi Majimaji vs Yanga alimwambia mwamuzi ahakikishe Yanga inapoteza mechi’

1140
0
SHARE

IMG_0195

Na Baraka Mbolembole

HUSSEIN Athumani alishindwa kuwapa Majimaji FC mkwaju wa penalty katika mchezo uliopita dhidi ya mabingwa watetezi Yanga SC.

Mlinzi wa Yanga, Juma Abdul aliunawa mpira ndani ya eneo la hatari wakati Yanga ikiongoza 1-0 katika uwanja wa Majimaji, Songea. Upande wangu niliamini mwamuzi huyo alipaswa kuwapa Majimaji mkwaju wa penalty lakini hakufanya hivyo.

Majuzi-Shirikisho la Soka nchini TFF lilitangaza kumwondoa mwamuzi huyu mwenyezi wa Katavi katika orodha ya waamuzi wa ligi kuu Tanzania Bara kwa madai alipata alama za chini, lakini nyuma ya pazia Kamishna wa mchezo ule naamini naye anapaswa kuchukuliwa hatua.

“Kabla ya mchezo kuanza msimamizi wa mchezo aliwapa maelekezo waamuzi wa mchezo ule na kuwaambia wahakikishe Yanga wanapoteza mechi ama kutoa sare.” Nimaneno ya chanzo changu makini kikielezea sababu za nyuma ya pazia kuhusiana na adhabu aliyopewa mwamuzi huyo.

“Kamishna wa mchezo ni shabiki wa Simba na hakutaka kuona Yanga ikishinda mechi ile ili Simba iendelee kuongeza gepu la pointi katika msimamo wa ligi. Baada ya kuona mwamuzi amekiuka maagizo yake ndipo alipouamua kumkomesha kwa kumuandikia alama za chini Athumani ili aondolewe katika orodha ya waamuzi.”

Mara kwa mara kumekuwa na malalamiko kuhusu uchezeshaji na waamuzi katika soka la Tanzania hadi kufikia hatua ya wadau kuhoji ni kwanini hakuna mabadiliko licha ya waamuzi kadhaa kupewa adhabu na wengi kufungiwa kabisa kuchezesha.

Lakini kwa namna inavyoonekana nyuma ya uchezeshaji wao wa kiwango cha chini, waamuzi wengi wanakabiliwa na changamoto za kufanya kazi yao kwa kufuata maelekezo wanayopewa na viongozi wao.

Kama waamuzi wataachwa wachezeshe kwa kufuata sheria 17 zinazoongoza mchezo wa soka naamini malalamiko ya mara kwa mara yatapungua na tutawaona waamuzi wakichezesha vizuri michezo ya ligi kuu na hata ligi daraja la kwanza, la pili na ligi za madaraja ya chini zaidi ila kama TFF itaendelea kuwatoa ‘kafara’ ili kuficha siri zao ni wazi mpira wa Tanzania utaendelea kuanguka.

Mfano, Athumani ni kweli alishindwa kuwapa mkwaju halali wa penalty timu ya Majimaji lakini hata kabla ya kuanza kwa mchezo msimamizi wa mechi alimwambia afanyejuu chini kuhakikisha Yanga inapoteza mechi au kubalansi matokeo yawe sare.

Kwa kushindwa kutoa penalty ambayo pengine ingewasaidia Majimaji kusawazisha goli-mwamuzi huyo alimaanisha kukiuka maagizo ya kamishna wa mchezo na ili kumkomesha akaamua kumuandikia alama za chini katika ripoti yake ya mchezo ule.

“Athumani bado hajapewa barua rasmi kuhusu kuondolewa kwake katika orodha ya waamuzi lakini ameahidi kusema hadharani kila kilichotokea kabla ya mchezo ule mara baada ya kupewa barua yake ya kuondolewa katikaorodha ya waamuzi.”

Nadhani umefika wakati viongozi wa TFF, Bodi ya ligi na Chama cha waamuzi kuwapa uhuru waamuzi  ili wachezeshe mpira kwa kufuata sheria zake na si maelekezo kutoka kwao. Wajiulize wenyewe wataendelea kuwaondoa waamuzi hadi lini, wajiulize na kujijibu wenyewe.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here