Home Kitaifa Jicho la 3: Simba SC v Yanga SC, balaa likukute, usilifuate…

Jicho la 3: Simba SC v Yanga SC, balaa likukute, usilifuate…

1301
0
SHARE

simba-vs-yangaNa Baraka Mbolembole

GEORGE LWANDAMINA anapaswa kufanya mabadiliko ya wachezaji kutoka katika kikosi ‘kilichosambaratishwa’ 4-0 na Azam FC katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi itakapowakabili ‘mahasimu-watani wao wa jadi’ Simba SC katika game ya nusu fainali-Mapinduzi Cup 2017 itakayofanyika kwenye uwanja wa Aman, Zanzibar.

Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa ligi kuu Tanzania Bara, watakutana na Simba yenye kikosi kilekile kilichoifunga Jang’ombe Boys 2-0 siku ya jana Jumapili katika mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi. Mechi ya Jumanne hii itakayowakutanisha ‘wababe’ wa soka la Tanzania mjini Unguja inataraji kuwa na mvuto wa aina yake.

YANGA  ilikutana na kipigo cha kwanza ‘kizito’ tangu Mei, 2012 walipochapwa 4-0 na Azam FC katika mchezo wa hatua ya makundi katika michuano inayoendelea-Mapinduzi Cup 2017, Zanzibar siku ya Jumamosi iliyopita. Miaka minne na nusu iliyopita Simba SC iliifunga Yanga 5-0 katika mchezo wa kufunga msimu katika ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2011/12.

Januari  7, 2017 ni siku ‘mbaya’ kwa mashabiki wa Yanga baada ya kushuhudia timu yao ‘ikidhalilishwa-kimpira na kimatokeo’ katika uwanja wa Amaan, Zanzibar na timu ya Azam FC ambao walitawala sehemu ya kiungo kisha kuonyesha udhaifu mkubwa wa walinzi, Mwinyi Hajji, Vicent Andrew na Kelvin Yondan ambao waliteswa sana na kiungo-mshambulizi, Joseph Mahundi.

Kocha wa Yanga, Mzambia, Lwandamina, hapaswi kupanga timu ileile iliyokosa nidhamu ya kujilinda katika kipigo walichokipata siku ya Jumamosi kutoka kwa Azam FC

kama anataka kuanza vyema katika mipambano ya ‘Dar es Salaam-Pacha.’

Nahodha, Nadir Haroub anapaswa kurejea katika kikosi cha kwanza ili kuimarisha ngome iliyo-yumbishwa sana na Joseh Mahundi, Yahya Mohamed na John Bocco katika mchezo uliopita dhidi ya Azam FC.

Ndiyo, Simba wamekuwa wakisumbuliwa sana na tatizo la washambuliaji-wafungaji katika michezo ya karibuni lakini namna walinzi Kelvin Yondan na Vicent Andrew walivyocheza siku ya Jumamosi kiasi cha kumruhusu kiungo wa Azam FC kupita katikati yao kiurahisi akiwa ndani ya eneo la hatari na kutoa pasi iliyokosa mmaliziaji ni dalili za wawili hao kushindwa kucheza pamoja hasa dhidi ya timu inayoshambulia mara kwa mara.

Yanga kuruhusu magoli mawili vs Azam FC si jambo geni, lakini 4-0 ni ishara ya kwamba mambo hayapo vile yanavyotakiwa kuwa.

Mshambulizi ‘mchovu’ Mrundi, Laudit Mavugo alifunga mara mbili katika ushindi wa timu yake-Simba 2-0 Jang’ombe. Alifunga goli la kwanza baada ya kukimbilia kwa haraka mpira uliogonga mlingoti wa chini wa goli na kuupeleka nyavuni, na akafunga goli la kiki kali ya juu akiwa upande wa kulia-upande wa kushoto wa Jang’ombe Boys.

Hilo ni jambo zuri kwa makocha Mcameroon, Joseph Omog na msaidi wake Mganda, Jackson Mayanja ambao walikuwa wakisema mara kwa mara wanaumizwa na namna washambuliaji wao wanavyoshindwa kufunga magoli licha ya timu yao kupata ushindi katika baadhi ya michezo.

Uwepo wa Nadir utamfanya Kelvin kucheza vizuri kwa sababu-tofauti na Dante, nahodha Nadir ni mtu mwenye uwezo wa kuongoza safu ya ulinzi. Yanga ilikosa kiongozi katika ngome.

Kutokuwapo kwa Mtogo, Vicent Bossou, Nadir na mchezaji aliyemaliza mkataba wake mwezi uliopita Mbuyu Twite kwa wakati mmoja kulichangia safu ya mashambulizi ya Azam FC kutawanya mipira kila upande na jambo hilo lilichangia walinzi wa Yanga kupoteza mwelekeo hasa Azam walipocheza kwa kasi na kukimbia vizuri katika nafasi wazi.

ZILIPOTOKA

Katika michezo minne ya kundi la kwanza lililokuwa na timu tano, timu ya Simba ilishinda michezo mitatu na kupata sare moja, ilifunga magoli matano na kuruhusu goli moja katika mchezo walioshinda 2-1 vs Taifa Jang’ombe.

Katika magoli yao matano washambuliaji wawili wamefanikiwa kufunga magoli matatu ( Juma Ndanda Liuzio-goli moja na Mavugo magoli mawili,) magoli mengine mawili yamefungwa na kiungo Muzamiru Yassin.

Yanga wao wamefuzu nusu fainali baada ya kushinda michezo miwili kati ya mitatu ya kundi la Pili na kupoteza mchezo mmoja. Wamefunga magoli 8 na kuruhusu magoli manne kati nyavu zao.

Kama ilivyo kwa Simba ambao hawakufunga goli katika mchezo mmoja wa makundi ( URA 0-0 Simba), Yanga nao baada ya kufunga magoli nane katika michezo miwili ya mwanzo hawakufunga katika game ya mwisho ( Yanga 0-4.)

Huku kiungo wake mshambulizi, Msuva akifunga magoli manne katika michezo miwili ya mwanzo. Mshambulizi Donald Ngoma yeye tayari amefunga magoli mawili na viungo, Mzimbabwe, Thaban Kamusoko na Juma Mahadhi pia wakifunga goli moja moja. Hii inamaanisha kila timu inaweza kufunga hata kama washambuaji hawatafunga.

VIKOSI

Katika mchezo vs Jang’ombe Boys, kocha wa Simba Joseph Omog aliwapanga,Mavugo, Pastor Athanas na Liuzio katika mashambulizi. Anaweza kumuondoa mchezaji mmojawapo na kumpanga Ibrahim Ajib kutokana na kuhitaji uzoefu wa ‘Dar Pacha’.

Nahodha, Jonas Mkude, Muzamiru na Shiza Kichuya wanaweza kuanza katika kiungo huku Besala Bokungu, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, Abdi Banda na Method Mwanjali wanataraji kumlinda kipa Nana Agyei.

Ili Yanga watawale mechi ni lazima kwanza wachezaji wenyewe  wawe tayari kuichezea timu yao na kuacha ‘ulalamishi’ kuhusu mazoezi magumu.

Mpira ni mazoezi  na sidhani kama Lwandamina anawapa mazoezi ili washindwe kufanya vizuri uwanjani. Kila kocha anahitaji kufanikiwa katika kazi yake ndiyo maana  huwapa mazoezi ya kutoka wachezaji, kwa maana bila kufanya hivyo wachezaji hawawezi kuzalisha kile anachokitaka.

Nilidhani Lwandamina ataendelea kuichezesha Yanga ileile ya mtangulizi wake Hans van der Pluijm kama alivyofanya katika michezo miwili ya mzungo wa pili katika ligi kuu. Simlaumu kwa kumuingiza kikosi cha kwanza Mahadhi katika michuano ya Mapinduzi kwa sababu ni sehemu ya kuwatambua na kujua viwango vya wachezaji wake.

Kuelekea mchezo wa kesho vs Simba nadhani kocha huyo kwa kushirikiana na msaidizi wake Juma Mwambusi wanapaswa kuwapanga washambuaji wawili na viungo wanne, mabeki wanne ( 4-4-2). Amis Tambwe anahitaji goli moja tu ili kuwa mfungaji bora wa muda wote katika mipambano ya Simba vs Yanga.

Japokuwa bado hajafunga goli katika michuano ya Mapinduzi, Lwandamina anapaswa kumpanga Tambwe na Ngoma katika safu ya mashambulizi. Msuva katika wing ya kulia na Deus Kaseke katika wing ya kushoto. Niyonzima na Kamusoko katika eneo la kati na safu ya ulinzi licha ya kufanya makosa mengi katika mchezo uliopita anapaswa kumbadili Dante tu na nafasi hiyo ampe nahodha Nadir.

NANI MSHINDI?

Siku zote ni heri balaa likukute pale ulipo na si kulifuata kule lilipo, Yanga walitambua kitendo cha kushindwa kuifunga Azam  FC na kukubali kichapo kingewafanya wamalize katika nafasi ya pili katika kundi B, na hilo lilikuwa na maana ya kukutana na mshindi wa kwanza wa kundi A.

Inawezekana walishajiandaa na rekodi yao ya karibuni dhidi ya Simba ni bora kwa maana katika michezo mitatu iliyopita wameshinda mara mbili na kupata sare mara moja.

Hata kabla ya kuwavaa Jang’ombe Boys siku ya jana, Simba walifahamu nafasi waliyopo inawakutanisha na Yanga katika nusu fainali. Wakashinda 2-0 na kudhihirisha wapo tayari kukabiliana na mabingwa hao wa Bara ambao wamekuwa wakiwanyanyasa hivi sasa-kimataji na kimatokeo.

Kete yangu bado naiweka upande wa Yanga kwa sababu naamini wana washambuaji ambao wanaweza kufunga-huku Tambwe akifunga katika michezo mitatu mfululizo ya mahasimu hao wa soka la Tanzania.

Simba hawana safu imara ya ulinzi licha ya kuruhusu goli moja katika michezo minne ya makundi. Uchezaji wa Mwanjali na Banda utaathiriwa kwa kiasi kikubwa na kasi watayokuwa nayo Yanga wakati wakishambulia.

Yanga walipwaya sana katika ngome vs Azam FC na kama watajirekebisha katika hilo  watakuwa salama kwa sababu Simba haina washambuliaji wasumbufu. Liuzio, Mavugo hata Ajib hawana kasi ya kuwasumbua walinzi wa Yanga. Hatari pekee ya Simba katika mchezo huu ni Muzamiru, Kichuya na Mohamed Ibrahim-viungo hawa watatu wanapenda kufunga.

Simba walikutana na mtihani mzito walipocheza na URA, lakini wakavuka mbele ya Waganda hao pasipo kuruhusu goli. Hilo halikuwa jambo la kushangaza kwa sababu timu hiyo ya Uganda haikuwa katika kiwango kizuri katika michuano ya mwaka huu. Dhidi ya Yanga, mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara wanapaswa kuongeza kasi na umakini.

Yanga watakuwa na mchezo mgumu sana Jumanne hii na hili waweze kufanya vizuri wanatakiwa kuongeza umakini katika ngome, na Lwandamina anapaswa kuelewa Yanga si timu inayoanza kujijenga bali ni timu iliyokamika kiuzoefu,kiubora na kiushindani.

Kama ataipanga timu yake vizuri, Lwandamina atakuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi katika mchezo wake wa kwanza vs Simba kutokana na kuwa na vipaji vya kutosha na wachezaji wenye ubora wa kusaka ushindi.

NANI KALIFUATA BALAAAA?

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here