Home Kitaifa MTAZAMO VPL: MO anavyopunguza uongo na kuibeba Simba

MTAZAMO VPL: MO anavyopunguza uongo na kuibeba Simba

927
0
SHARE

img-20161229-wa0040

Na Athumani Adam

Frank Lampard hakuwa mahiri sana kwenye kuchezea mpira kama alivyokuwa Austin Jay Jay Okocha, kwa lugha ya kisasa ya mpira kina Okocha wanaitwa ‘Waongo waongo’. Lakini licha ya Lampard kutokuwa muongo  ni miongoni mwa viungo ambao dunia ya soka itaendelea kuwakumbuka daima milele kutokana na mchango wake katika klabu ya Chelsea.

Lampard alishinda kila kila aina ya taji pale Stamford Bridge  kabla ya kuelekea Marekani. Alikuwa na tabia ya kufanya vitu muhimu uwanjani.

Kiungo wa Simba aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar wakati wa majira ya kiangazi, Mohamed Ibrahim ‘MO’  jana alifanya maamuzi magumu kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara dhidi ya maafande wa Ruvu Shooting. Mohamed Ibrahim ni moja ya viungo bora ambao wapo kwenye klabu ya Simba, ni Bingwa wa kuchezea mpira lakini staili yake ya uchezaji kwenye mchezo dhidi ya Ruvu ilionesha kwa kiasi gani alikuwa na malengo ya kuibeba Simba kwenye mchezo dhidi ya Shooting kuliko kufurahisha jukwaa.

Alipiga mashuti takribani manne kuelekea kwenye lango la Ruvu, bahati mbaya inaonesha mpira haukujaa sawa sawa kwenye mguu wake. Lakini akafanikiwa kufunga bao pekee dakika ya arobani na tano bao ambalo lilipelekea Simba kuendelea kuongoza ligi kwa tofauti ya Pointi nne dhidi ya mahasimu wao Yanga.

Anachoendelea kukifanya Mohamed Ibrahim ni kile ambacho kiliwafanya kina Lampard kukumbukwa daima kwenye ulimwengu wa Soka. Mo anafunga mabao muhimu, hadi sasa amefunga mara nne kwenye mechi za ligi kuu VPL  licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye mechi za mwanzoni mwa mzunguko wa kwanza ligi kuu msimu huu.

Hiki ndicho ambacho kinamfanya kocha Joseph Omog kuanza kumuamini na kumpa nafasi ya kuanza kwenye nafasi ya nyuma ya mshambliaji ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Ibrahim Ajib wakati wa duru la kwanza.

Unapokuwa na mchezaji wa nafasi ya kiungo ambaye anafunga mabao muhimu ni faida kwa timu. Inaonesha hivi ndivyo mwalimu Joseph Omog anavyotaka timu icheze, ukimuondoa Mohamedi Ibrahim pia hata wachezaji wengine wa eneo la Simba wamekuwa watu wa kujaribu wapokaribia nje ya eneo la kumi na nane la timu pinzani.

Tabia ya kiungo kufunga ni jambo ambalo lilikosekana kwa muda mrefu kwenye ligi ya Tanzania. Viungo wengi walipenda sana kuwa waongo waongo wa kuchezea sana mpira na kupiga pasi nyingi za nyuma wakati mwingine ambazo hakikuwa na faida.

Kama Mo ataendelea kucheza kwa staili hii ya kuwepo kwenye eneo la hatari la mpinzani pindi timu yao inaposhambulia bila shaka namtabiria makubwa zaidi kwenye mechi zilizobaki za ligi ya VPL msimu huu.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here