Home Kitaifa Dkt. Jonasi Tiboroha ametaja mbinu 8 za kupata matokeo katika michezo

Dkt. Jonasi Tiboroha ametaja mbinu 8 za kupata matokeo katika michezo

642
0
SHARE

TIBOROHA (1)

Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga SC Dkt. Jonasi Tiboroha amepost andiko kwenye ukurasa wake wa facebook kueleza namna ambavyo timu inaweza kupata matokeo kwenye mechi.
Nasikiliza redio, natazama TV na kusoma mambo mengi juu ya matokeo ya vilabu vya VPL, nimesoma taarifa zikielezea matokeo haya nami nikaona nishiriki katika kutoa tafakuri hii.

Katika fikra zangu za leo nataka kujaribu kuweka maono ambayo ya mwaka mzima bali ni katika kuzikumbusha klabu zetu za Tanzania kuwa na utaratibu wa kuweka vipaumbele iwe katika matokeo ya timu au kucheza na kuchukua ubingwa lakini pia katika mambo mengine ya maendeleo ya timu zao.

Kuna vitu vingi sana ambavyo vinaweza kutoa taswira ya muelekeo wa matokeo ya timu katika ligi inayoendelea kati ya timu na timu.

Mambo haya yakizingatiwa basi timu husika si ajabu ikashangilia wakati wote japokuwa kwa kipindi fulani inaweza ikajikwaa na kupata matokeo hasi.

1. HISTORIA – Tukumbuke kwamba tunaishi katika karne ya 21 na kwa hakika karibu kila taifa, kila klabu katika nchi yoyote imekuwa ikiheshimiana historia ya klabu nyingine kwa matokeo na kwamba yaliyotokea ni sababu ya kuheshimu sayansi na ufundi hususani katika kufanya tathmini ya nini kinatakiwa ili matokeo yawe mazuri.

Ninachokisema hapa ni kwamba kama tathmini ikifanywa bila weledi matokeo mabaya huendelea au hujirudia na yakiendelea husababisha kitu wenzetu wanachokiita “mental block” au kuzuia akili kufanya kazi ipasavyo kwa upande wa timu ambayo nafasi ya kushinda dhidi ya timu nyingine ni kidogo sana.

Timu zenye historia ya udhaifu hucheza kwa woga mkubwa na litokeapo jambo wao hulalamika. Hii ni kwa sababu kichwani mwao rekodi ya matokeo ya zamani inawagharimu.

Lakini inawezekana pia wakati mwingine wao wakapata matokeo ya kushangaza isivyo kawaida. Ninacho sema hapa ni kwamba, timu ziwe na wataalamu wenye uwezo wa kufanya tathmini za namna hii hata kama zimezungukwa na watu wasio sahihi katika kusaka mafanikio ya timu.

2. WACHEZAJI MUHIMU – timu inapokuwa na wachezaji mahiri wenye uwezo kama vile wafungaji ambao wao wanaweza kubadili matokeo hata kama timu inacheza vibaya; viungo wazuri wachezeshaji na wakabaji ambao muunganiko wao unaweza kutengeza nafasi nyingi kwa timu yao kupata ushindi lakini pia kuzuia adui kuiathiri timu yao; ukuta imara na kipa mahiri vitu hivi huwa ni chachu ya kupata matokeo.

Lakini ikumbukwe kwamba wachezaji wa aina hii lazima wawe na kitu wenzetu wanaita “Consistency” kucheza mechi vizuri kila wiki na kushika maelekezo ya mwalimu na sio wachezaji wasioaminika kama umeme wetu wa pale Ubungo na wasiwe wale wasioweza kushika maelekezo utafikiri wanatumia madawa ya kulevya.

3. KOCHA – Timu yenye wachezaji wengi mahiri au timu ambayo imejengwa na wachezaji wengi vijana, na yenye kocha mahiri mwenye falsafa inayoelekeza timu yake icheze namna gani, inaweza kuishinda timu yoyote ile.

Kocha mwenye weledi ni kitu muhimu sana hususani anayeweza kujua ni wakati gani timu yake inapoteza au kushinda mchezo, ni wakati gani afanye mabadiliko na kwa sababu gani ni wakati gani abadili mbinu hata kama mchezo unaisha ni nguzo katika mafanikio ya klabu yoyote.

Watu kama hawa wanapaswa kuenziwa na kupewa muda zaidi ili waweze kufanya kazi vema na kuleta mafanikio katika timu zao. Mizengwe dhidi ya watu wa namna hii ni matatizo na timu hatoshangaza kama inapata matokeo tofauti na inavyotarajiwa.

4. VIONGOZI – mafanikio katika klabu yanategemea aina ya viongozi ambao wamekabidhiwa kuendesha shughuli za kila siku.

Sio ajabu kwa vilabu vikubwa duniani kusikia kwamba viongozi wasiojielewa wanaadhibiwa kwa sababu ya matokeo mabaya katika majukumu yao ya kila siku.

Moja ya majukumu hayo ni kuwa na uwezo wa kuajili watendakazi (makocha, wachezaji, nk) ambao wanaweza kuifanya timu ikawa na ushindani. Ikumbukwe kwamba mchezo wa mpira japokuwa Tanzania tunauchukulia poa, ni mchezo ambao unahitaji watendaji wenye weledi wa hali ya juu na wenye taaluma katika kufanya mambo haya.

Mfano ili kupata kocha au mchezaji mzuri, viongozi lazima wawe na taaluma ya kuvumbua vipaji, kuchagua vipaji na kuendeleza kama ni wachezaji. Lakini pia lazima wawe na uelewa wa “career transition” kwa tafsiri sasa ni kazi mpito kitu ambacho ni kipimo kikubwa katika kujua ninaye muajiri ni mtu wa namna gani? Ana historia gani katika kazi hii ninayompatia kuifanya?

Nini uwezo wake, amefanikiwa nini na namna gani? Je mafanikio aliyoyapata anaweza kuyapata katika mazingira yetu (context?) Kinyume na kufanya hivyo tutakuwa tunaendesha biashara serious kiholelaholela tu na mwisho wa siku hakutokuwa na mabadiliko zaidi ni kudidimia kila kunapokucha na matokeo kuwa mabaya kila kunapokucha.

5. NJAA NA MIHEMKO YA MATOKEO – Haijalishi ni kushinda mchezo, kikombe au mashindano fulani endapo wachezaji watapoteza njaa na muhemuko wa kupata ushindi basi timu haiwezi kushindana na kupata matokeo tarajali.

Chukua mfano wa timu zozote duniani ambazo zinafanya vema katika ligi zao ni njaa za wachezaji kupata mafanikio kutokana na maelekezo wanayoyapata katika vilabu vyao zinazofanya timu zao ziwe za ushindani na zishinde mataji na michezo kwa wingi.

Timu lazima iwe na uwezo wa kuwafanya wachezaji kujitoa 100%, katika kufunga magori, kucheza kwa bidii na kujituma bila kufikiria majeraha yanayoweza kutokea kwa kucheza kwa ushindani.

6. BAHATI – Watu wengi sana huongelea bahati, lakini nasema ingekuwa bahati pekee inasaidia basi wanaocheza kamali na wazee wa mikeka wangecheza soka na timu zetu Tanzania tungekuwa washindani.

Nasema bahati hupatikana kwenye miguu yenye mbinu za kusakata kabumbu. Unatakiwa kujua kwanza ndipo bahati ije na si vinginevyo.

Ukikaa mbele yangu na kusema hapa Bongo timu zetu hazina bahati nitakuambia “negative, they are simply not good enough!”

7. PESA – Hapa najua walio wengi walikuwa wanasubiri kusikia nitasema nini. Nasema pesa ni muhimu wakati fulani na lakini sio kila kitu katika kuleta mafanikio ya mpira wa miguu.

Ingekuwa pesa ni muhimu sana katika kupata matokeo Manchester United angekuwa na point 52 katika EPL. Au Madrid ya Zidane ingekuwa imevuna point zote Hispania.

Matokeo ya timu ni zaidi ya fedha. Fedha itumike kusaidi mambo muhimu katika timu ili iweze kucheza kwa ushindani. Lazima dhana ya ushindani tuiweke mbele kwanza na tuache kuongea mambo ambayo hayana maana na sio mustabali wa mpira.

8. MAANDALIZI – Kuna timu chache sana duniani ambazo zinaweza kucheza kwa kutumia mbinu ya aina moja na zikafanikiwa zinapocheza nyumbani na ugenini.

Ninachosema hapa matokeo yanweza kuathirika sana kwa kuisoma na kuitathmini timu pinzani na kufanya maandalizi kwa maana hiyo kama umejifunza vema Game analysis unaweza kwenda kwenye mchezo ukiwa na mbinu zaidi ya moja ili upate matokeo mazuri.

Swali langu nimekuwa nikijiuliza sisi hapa nyumbani huwa tunafanya home works zetu kweli? Lakini pia swali la msingi, timu yako ina wachezaji ambao wanaweza kucheza kwa kutumia mbinu mbalimbali?

Maandalizi ninayoyasema pia ni pamoja na maandalizi ya timu kabla ya msimu (pre-season), maandalizi kiakili kabla ya mchezo (pre-game mental preparation), maandalizi ya kila mchezaji binafsi katika stamina, ujuzi, kucheza kama timu na mawasiliano, taarifa za uwezo wa timu pinzani ikiwa ni pamoja na kujua namna timu hiyo inavyocheza (style), mbinu zao na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja katika timu hiyo.

Je, kuna msaada wa kutosha kwa timu yenu mfano madawa, muda wa kutosha kupumzika, lishe maridhawa, nk.

Ningependa nieendelee ila muda wa kutosha sina na nafikiri niishie hapa kwa leo kwa kuuliza haya ninayoyasikia, yako katika mtazamo huu katika michezo yetu hapa Bongo? Timu ngapi zinafanya mambo haya na zikakosa matokeo??

NAOMBA NIKUMBUSHE KATIKA HAYA SIDHANI KAMA TIGOPESA IMO. TUACHE UHAINI TUJIPANGE KUSHINDANA.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here