Home Kitaifa Jicho la 3: Nilichokiona baada ya dadika 90’ za kwanza Pastory Athanas...

Jicho la 3: Nilichokiona baada ya dadika 90’ za kwanza Pastory Athanas akiichezea Simba

1427
0
SHARE

pastory-athanas

Na  Baraka Mbolembole

DAKIKA zake 90’  za kwanza  kama mchezaji  wa Simba SC zilimalizika vizuri, na zimemuachia  kumbukumbu  nyingine nzuri  katika maisha yake ya soka.

Alianza katika safu ya mashambulizi  na kusaidia upatikanaji wa goli pekee la Simba vs JKT Ruvu ambalo lilifungwa  dakika ya mwisho kabisa ya kipindi cha kwanza na Muzamiru Yassin akimalizia kwa kichwa ‘hafifu’ mpira  mrefu  uliopigwa na Pastory Athanas kutokea  upande wa kulia mwa uwanja.

Baada ya usajili wake kutoka Stand United kujiunga na Simba kukamilika siku moja kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo  niiandika makala ya kuuponda usajili wa Pastory na nilisema halikuwa ‘ingizo’ bora katika  kikosi  cha  Joseph Omog kwa  sababu  niliamini Simba ‘inamuhitaji  mfungaji na si mshambuliaji mzuri.’

Niliukataa usajili wa magolikipa  wawili wa kigeni  na nikaandika  nafasi  hiyo ya mchezaji wa kigeni ibaki wazi kuliko kuwa na Muivory Coast, Vicent Angban na Mghana alisajiliwa Disemba hii, Daniel Agyei kwa wakati mmoja.

Kwa vile  kocha Omog alihitaji nyongeza ya golikipa, upande wangu  nilihitaji kuona Aghban anaondolewa kutokana na makosa yake mengi kiuchezaji-kucheza mechi akiwa mbali na lango lake, kushindwa kucheza mipira ya krosi, kona na umakini  mdogo alionao katika upangaji wa safu  yake  ya ulinzi.

Omog alihitaji pia kiungo, ndiyo maana akasajiliwa Mghana, James Kotei usajili huu kama ilivyo ule wa Pastory sikuona umuhimu wake kwa aina ya mapungufu yaliyoonekana katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza.

Aliposajiliwa Juma Ndanda Liuzio kutoka Zesco United ya Zambia niliona usajili huu wa mkopo unaweza kukidhi mahitaji, lakini mimi nilimuhitaji zaidi mfungaji wa Mtibwa Sugar FC, Rashid Mandawa.

DAKIKA 180 HAKUNA MSHAMBUAJI ALIYEFUNGA MZUNGUKO WA PILI

Baada ya Laudit Mavugo kushindwa ‘kufurukuta’ siku ya mchezo dhidi  ya Ndanda FC katika uwanja wa Nangwanda, Mtwara (Simba ilishinda 2-0 kwa magoli ya viungo, Muzamiru na Mohamed Ibrahim) benchi la ufundi la Simba lilimuanzisha kijana mpya kikosini katika mchezo dhidi ya timu iliyowabana sana katika mzunguko wa kwanza JKT Ruvu wakati huo wakiwatumia, Mavugo na Ibrahim Ajib kisha Muivory Coast, Blagnon katika safu ya mashambulizi lakini wakaambulia suluhu  (0-0).

Pastory ambaye anasimamiwa na meneja wake Muhibu Kanu tangu mwaka 2013 katika kikosi cha Toto Africans U20 kilichokuwa kikinolewa na Mkurugenzi huyo wa zamani wa ufundi katika klabu ya Stand United ya Shinyanga.

Akiwa tayari amefunga magoli mawili na kusaidia magoli nane katika VPL msimu huu, kijana huyo mzaliwa wa Maswa, Simiyu anaweza kujiendeleza vizuri akichezeshwa kama mshambuaji wa pili kwa sababu ana uwezo wa kupiga pasi sahihi na kwa wakati mwafaka.

Katika mchezo wa Stand 1-0 Yanga, Pastory alifunga goli pekee la timu hiyo ya Shinyanga, lakini nilivutiwa zaidi na uhakika wake katika kila alichotaka kukifanya katika mchezo wake wa kwanza akichezea moja kati ya timu mbili kubwa zaidi nchini-Simba.

Hakufunga kama ilivyokuwa kwa Mavugo na Ajib walianza pamoja katika game vs Ndanda ila mbio zake uwanjani, ushirikiano aliuonesha kwa wachezaji wenzake, na uchezaji wake wa kukimbia eneo lote la mbele akitafuta mbinuza kutengeneza nafasi ni kitu kinachoweza kumbeba zaidi.

Ana miaka 23 tu, nadhani ni umri sahihi wa kupambana ili apate nafasi ya kucheza na kuendeleza kile alichonacho-kupiga pasi za mwisho na kufunga pale inapobidi.

Anaweza kufanya vizuri akicheza nyuma ya mshambuaji wa kwanza, na kama mshambulizi huyo wa kwanza atakuwa na kipaji kinachoambatana na ufungaji, Pastory atamng’arisha kwa maana ameondoka katika timu ya kawaida akiwa amefunga magoli mawili na ku-asists magoli nane. Amefanya hivyo akiwa Stand.

Katika michezo miwili ya mzunguko wa pili hakuna straika wa Simba aliyefunga,wamefunga magoli matatu (yaliyofungwa na Muzamiru magoli mawili na Mohamed Ibrahim-goli  moja) Bado Liuzio hajacheza, ila kuna ‘chembechembe’  za kuonekana kiungo-mshambulizi mwenye kipaji kikubwa akichomoza.

“Anatakiwa apambane, yupo  kwenye timu kubwa yenye malengo makubwa, wachezaji wengi wenye vipaji, hamasa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki na wanachama ambao wote wanahitaji matokeo katika kila mchezo,” anasema Kanu ambaye pia anawasimamia wachezaji kama Rajab Zahir na Omar Issa wanaochezea Mbeya City,  Jacob Masawe wa Stand United, Hassan Dilunga, Mussa Said,  Hamis Thabit wanaokipiga JKT Ruvu na wengineo.

“Nimekuwa naye tangia nikiwa Toto mwaka 2013 hivyo kiuchezaji na kitabia nina weza kujua, namshauri apambane zaidi ili kocha amuamini ampe nafasi. Upande wangu namuamini anao uwezo zaidi ya kile alicho kionyesha katika mchezo dhidi ya JKT Ruvu. Naamini atafanya vizuri zaidi akitulia na timu yake mpya.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here