Home Kitaifa Jicho la 3: Yanga SC inamuhitaji Said Makapu mpya, si Mbuyu, namsubiri...

Jicho la 3: Yanga SC inamuhitaji Said Makapu mpya, si Mbuyu, namsubiri Justine Zulu

775
0
SHARE

justine-zulu

Na Baraka Mbolembole

SAID Juma Makapu alianza vizuri majukumu yake kama mchezaji wa Yanga SC msimu wa 2014/15.

Japokuwa alikuwa kijana mdogo kiumri, huku akitokea upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania-namaanisha Zanzibar mchezaji huyo wa nafasi ya kiungo wa kati alikuwa mgumu kupitika.

Anajua kukaba, anajua kucheza faulo-jambo muhimu kwa mchezaji wa nafasi ya kiungo, anajua kupiga pasi zenye mwelekeo, pia alikuwa na mbio nzuri ndani ya uwanja.

Nilitegemea mambo mengi mazuri kutoka kwa kijana huyu ambaye tayari alishapata nafasi ya kuitwa katika timu ya Taifa ya Tanzania. Msimu wake wa pili Yanga (2015/16) haukuwa mzuri, na sababu kubwa ya kushindwa kupandisha kiwango chake zaidi ni majeraha ya mara kwa mara.

Wengi tulidhani Hans van der Pluijm angependekeza kuachwa au kutolewa kwa mkopo kwa mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Zanzibar wakati wa usajili wa dirisha kubwa katikati ya mwaka huu, lakini mkufunzi huyo raia wa Holland aliendelea kulinda imani yake kwa mchezaji huyo aliyemsajili akiwa kinda miaka miwili iliyopita.

Katika michezo michache aliyofanikiwa kucheza msimu uliopita, Makapu alionesha imani kubwa kwa benchi la ufundi na mashabiki wa Yanga waliamini akiyashinda majeraha, basi watakuwa na mmoja ya wachezaji bora wa nafasi ya kiungo Tanzania.

Makapu si ‘mchangamfu’ uwanjani kama ilivyokuwa kwa Athumani Idd ‘Chuji’ na wala si mpigaji wa pasi za umbali mrefu zinazofika kwa walengwa kama, Frank Domayo ‘Chumvi,’ lakini yeye ni jasiri na mwenye nguvu zinazomsaidia kupora mpira kutoka kwa mpinzani wake, anajua kufunga njia za wapinzani wake kupitisha pasi za hatari. Uwezo wake ndiyo ulimfanya Hans kuendelea kumshikilia kijana huyo.

Kuelekea raundi ya pili ya ligi kuu Tanzania Bara msimu huu, na huku akiwa katika msimu wake wa tatu klabuni Yanga, bila shaka naweza kusema, Makapu ameshindwa kufikia matarajio yake kama mchezaji wa Yanga, ameshindwa kufikia matarajio ya bechi la ufundi, na ameshindwa kuwafanya mashabiki wa timu yake kuamini kama yeye ni kiungo bora namba 6 waliyemtarajia baada ya Chuji na Domayo.

YANGA INAHITAJI MAKAPU MPYA

Justine Zulu ni chaguo la kwanza la kocha mpya wa kikosi cha Yanga, Mzambia, George Lwandamina.

Kwa sasa siwezi kusema kuhusu ubora wa Lwandamina kiufundishaji kwa maana sijamfuatilia kwa ukaribu huko alipokuwa akifundisha (Zesco United) na sijui kuhusu ubora wa kiungo huyo anayetaraji kumsaini kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kikosi cha Yanga.

Kwa mtazamo wangu Yanga inahitaji namba 6 hasa na si Mbuyu Twite ambaye wakati mwingine amekuwa akitumika katika nafasi hiyo chini ya Hans. Mbuyu ni mchezaji muhimu sana ambaye nitaendelea kumuhusudu, amejitolea kila alichoweza kuisaidia Yanga kunyanyuka baada ya kuvurunda msimu wa 2011/12.

Mbuyu ni mlinzi bora wa kati na kiraka mwenye kipaji cha hali ya juu. Anaweza kucheza fullback namba 2 au 3, namba 4, 5 na 6 lakini Yanga ilimuhitaji zaidi Makapu katika nafasi ya kiungo namba 6 na si Mbuyu.

Yanga chini ya Hans imekuwa ikifunga magoli mengi kutokana na kujaza viungo wachezesha timu mwenye uwezo.

Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Saimon Msuva hakika hawa ni wachezaji ambao walirahisisha mbinu za Hans na kuisaidia timu kupata magoli ya kutosha, lakini katika uzuiaji mambo kiasi si mazuri kwa sababu Yanga imekuwa ikiruhusu magoli katika michezo yake mingi na ukitazama kwa jicho la tatu utagundua tatizo hilo linaanzia katika nafasi ya kiungo wa ulinzi.

Ili afanikiwe zaidi ya ilivyokuwa kwa Hans, kocha Lwandamina anapaswa kuimarisha ngome yake na hilo linawezekana kama atafanikiwa kumpata namba 6 mwenye uwezo wa kuchukua mipira kutoka kwa safu ya ulinzi na kuanzisha mashambulizi.

Yanga inapaswa kumsaini namba 6 mwenye uwezo wa kupunguza nafasi ya wapinzani kutengeneza magoli katika lango lao. Kama, Makapu asingesumbuliwa na majeraha alikuwa mtu sahihi lakini hawapaswi kumtegemea tena kijana huyo na badala yake ni kuingiza chaguo lingine bora ili kuifanya timu kuwa ngumu kufungika ukizingatia miezi mitatu ijayo watakuwa katika michuano ya Caf Champions League 2017.

Yanga inamuhitaji, Makapu mpya na chaguo la Mzambia, Zulu anaweza kuimarisha timu katika uzuiaji, uanzishaji wa mashambulizi na usaidizi katika upatilanaji wa magoli. Yanga SC inamuhitaji Said Juma Makapu mpya, si Mbuyu, namsubiri Justine Zulu…

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here