Home Kitaifa Jicho la 3: ‘Ni uasi kupinga mabadiliko, lakini mabadiliko yasilazimishwe…

Jicho la 3: ‘Ni uasi kupinga mabadiliko, lakini mabadiliko yasilazimishwe…

664
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

“Tunasema tunataka kufanya mapinduzi. Na siku hizi neno mapinduzi linapendwa sana katika Afrika. Mengine si mapinduzi, mengine ni maasi tu, nayo yanaitwa mapinduzi! Lakini nasema tunataka kufanya mapinduzi.

Lakini kwa nini tunataka kufanya mapinduzi? Inafaa kurudi nyuma kidogo, kutazama kwa nini lazima Yanga ifanye mapinduzi kutoka mfumo wa sasa na kumkodishia nembo ya klabu Mwenyekiti wao Yusuph Manji na si kuingia moja kwa moja katika mfumo wa kampuni.

Ukichunguza kwa umakini hili la Manji kutaka kukodishiwa Yanga kwa miaka kumi unaweza kusema ni kama Mwenyekiti huyo ‘alikurupuka,’ hasa baada ya kuona upande wa pili, namaanisha Simba SC kwa kauli moja ya wanachama walipokubali kuondokana na mfumo wa sasa wa klabu kutegemea wanachama na kuingia katika mfumo wa soko la hisa.

Siku mbili zilizopita nilikuwa nikifuatilia mahojiano kati ya watangazi wa kituo cha radio Clouds FM-Kipindi cha Sports Extra. Nilimuelewa sana Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga aliposema kwamba wana Yanga wanapaswa kufunga midomo yao na kuacha kutumia vyombo vya habari kupingana na mpango wa klabu kukodishwa kwa Manji na badala yake aliwasisitiza na kuwaomba waende katika mkutano wa dharura ulioitishwa na Mwenyekiti siku ya Jumapili hii ili kujadiliana kwa hoja na mwisho wa siku wafikie mwafaka wa pamoja.

Hata mimi japokuwa si mwanachama wala shabiki wa timu hiyo nilitikisa kichwa changu na kukubaliana na maneno ya Sanga. Majadiliano ndiyo msingi wa kusemezamana, na itapendeza sana kama ‘kikundi kidogo cha wazee wa klabu’ wanaongozwa na Mzee Akilimali wakienda wakienda kujenga mbele ya wanachama wenzao na hoja wanazotoa katika vyombo vya habari.

Yanga Sports Club inahitaji mapinduzi, kutoka miaka 80 ya utegemezi wa michango ya wanachama hadi kuwa klabu inayojiendesha kisasa. Baadhi ya watu wa Yanga wanasahau kwamba, miezi michache iliyopita walimchagua Manji kwa kura zote katika uchaguzi mkuu wa klabu.

Hii ilimaanisha kwamba walimkubali na kujenga imani kubwa kwake. Unyonge wa kwanza ulio mkubwa zaidi kwa binadamu ni ‘unyonge wa moyo.’ Mara kadhaa niliandika kwamba, wanachama wa Yanga wanahofu ya maisha bila Manji ndio maana kila alichokuwa akiamua Mwenyekiti wao hawakuwa wakihoji.

Pia, baadhi ya wanachama haohao wa klabu ya Yanga wamesahau kwamba walikuwa tayari kumpa uongozi wa miaka nane Manji miaka miwili iliyopita. Jitihada anazojaribu kufanya Manji na wanachama walio wengi ni jitihada kubwa sana, lakini kama wanachama wa klabu wataelewa nini hasa anachojaribu kufanya kiongozi wao.

Si kuelewa kwa juu-juu tu, lakini kuelewa kwa kwelikweli, na kwa dhati nini anachojaribu kufanya. Manji anataka kufanya mapinduzi, lakini nachokiona ni tatizo ni uharaka wa mapinduzi anayoyataka ukizingatia wazo la mfumo wa mapinduzi hayo ni yeye pekee aliyekuwa nalo.

Mzee Akilimali na wenzake wanaweza kuchukuliwa na kuonekana kama ‘waasi’ lakini sivyo. “Yanga haiwezi kukodishwa kama masufuria ya shughulini…” ni kauli ya kukera sana kwa wanachama wengi wa Yanga lakini itakuwa na maana sana kama Mzee huyo na wenzake wataipeleka na kuitengenezea hoja katika mikutano ya wanachama.

Ni kweli, Yanga ina histori kubwa sana tangu ilipoanzishwa mwaka 1935. Ni kweli Yanga haiwezi kukodishwa kama masufuria, lakini Mzee Akilimali na wenzake wanapaswa waelewe pia Yanga haiwezi kuendelea kutengeneza historia mpya ikiwa katika mfumo wa sasa.

Manji hapaswi kusalitiwa wakati huu muhimu japokuwa usaliti upo kwetu masikini siku zote. Manji pia hapaswi kutengeneza sababu za kusalitiwa. Kitu pekee kinachopaswa ni umoja, mshikamano wa mawazo, mshikamano wa hali na mali ili Yanga itengeneze historia mpya na si kuridhika na historia zilizopita ambazo daima zitabaki.

Wanachama wote walishakubali kuvunja katiba, ndio maana wakamruhusu na kumpa mamlaka ya uongozi Manji kinyume na katiba. YANGA YETU LIMITED nadhani ni tatizo ambalo Manji anapaswa kuliepuka. Yanga SC inapaswa kubaki hivyo daima ndio maana hata Manchester United, Manchester City, Chelsea, Liverpool zimebaki hivyo licha ya kununuliwa na wawekezaji binafsi.

Manji akodishiwe Yanga lakini hapaswi kubali kila kitu ili kufanikisha mapinduzi anayoyataka. Hapaswi kubadili jina la klabu, wala asikubali kushindwa kutokana tu na kutaka kubadili nembo ya klabu.

Yanga si mali yake bali atakodishiwa kwa muda tu na atairejesha kwa wenyewe. Yanga waende katika mikutano na kushindana kwa hoja za kufanikisha mapinduzi na si maslahi binafsi.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here