Home Kitaifa Yanga SC v Simba SC: ‘Wekundu wa Msimbazi’ watapigwa kwa mara ya...

Yanga SC v Simba SC: ‘Wekundu wa Msimbazi’ watapigwa kwa mara ya 3 mfululizo VPL

1409
0
SHARE

simba-vs-yanga

Na Baraka Mbolembole

KUHUSU kikosi cha Yanga SC kuelekea game ya Jumamosi hii vs Simba SC wala sina shaka nacho, nadhani huu ni wakati wa Simba SC kuendelea kuishi katika mashaka ya ‘Dar es Salaam-Pacha’.

Miaka 8 mfululizo pasipo kupoteza game ya mahasimu hao kwa kandanda nchini upande wa Simba ‘imekwishapita’ na ndani ya uwanja wapo katika nyakati ngumu dhidi ya mahasimu wao ambao wameshinda VPL mara tatu ndani ya misimu minne ya mwisho, huku wakipoteza mara moja tu pambano la ‘Watani hao wa Jadi.’

Ndani ya uwanja, Yanga wana timu ‘kabambe’ kuliko Simba inayopewa sifa nyingi katika vyombo vya habari. Katika uchambuzi wa kwenye makaratasi Simba wanaweza kuonekana ni wazuri lakini wanavyocheza hawaonekani kuwa kucheza kitimu zaidi.

Ndiyo, wana wachezaji wenye majina, lakini dhidi ya timu inayocheza kitimu kama Yanga watapata shida. Kuna mengi yamebadilika katika timu ya Yanga tangu Mei 7, 2012 walipofungwa 5-0 na mahasimu wao hao, na hilo pia lipo katika timu ya Simba.

Yanga wamepandisha kiwango zaidi wakati Simba wamekuwa wakiteremka. Msimu wa 2012/13 game mbili walizokutana, Yanga walipata ushindi mara moja na kulazimisha sare. Na ushindi pekee wa Simba tangu 2012 ni ule wa 1-0, Machi mwaka uliopita huku Yanga wakishinda tena mara mbili msimu uliopita.

Kwa sasa Yanga wapo katika daraja la juu na siri kubwa ya mafanikio yao ni kucheza kitimu licha ya kwamba wana wachezaji wenye uwezo binafsi.

Ibrahim Ajib, Laudit Mavugo ‘hawatengenezeani’ nafasi za kufunga, hili ni tofauti kabisa na Amis Tambwe na patna wake Donald Ngoma ambao wamekuwa wakicheza kwa ushirikiano mkubwa na kila mmoja ni mtengenezaji wa magoli ya mwenzake.

Viungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto na Jonas Mkude, sawa si wachezaji wabaya ila upigaji wao wa pasi ni tofauti kabisa na wale wa Yanga.

Pasi nyingi za wachezaji wa kati mwa uwanja upande wa Simba si makini na mipira yao mingi hupotea. Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima wamekuwa na viwango bora katika upigaji wa pasi na jambo hilo litaendelea kuibeba timu timu yao.

Beki ya Simba haina kasi na uwepo wa Saimon Msuva, Deus Kaseke, Juma Mahadhi na Geofrey Mwashuiya ni tatizo kwao.

Viungo hao wa pembeni wa Yanga watanufaika na kasi yao. Majuto pekee kwa Yanga itakuwa ni kushindwa kufunga katika nafasi watakazotengeneza kwa sababu safu ya ulinzi ya Simba haina uwezo wa kucheza mipira ya juu na Yanga wako vizuri katika mipira hiyo.

Yanga inazidi kuwa imara ndani ya uwanja na hilo limekuwa likiwaogopesha hadi wapinzani wao. Watashinda mechi ya 3 mfululizo ya Dar-Pacha, sina shaka na hilo. Wanazuia vizuri, wanashambulia vizuri na wana wafungaji wawili bora wenye usongo na umakini wa kutumia nafasi zinazopatikana.

Huu ni wakati wa Yanga kuendelea kuwaweka katika mashaka ya ‘Watani wa Jadi’ mahasimu wao ambao walishindwa kuwafunga katika ligi kwa misimu nane mfululizo miaka ya nyuma (2000-2008).

Kupoteza mara moja tu katika misimu minne iliyopita dhidi ya Simba ni hatua, pia dalili za kuashiria wamebadilisha mambo mengi mabaya na kuyageuza kuwa mazuri katika ‘Dar es Salaam-Pacha.’

Yanga v Simba, mwisho wa kuandikia mate ni kesho Jumamosi katika uwanja wa Taifa, ushindi nawapa Yanga SC.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here