Home Kitaifa Jicho la 3: Yanga ilistahili kipigo vs Stand United, msijidanganye kuhusu…

Jicho la 3: Yanga ilistahili kipigo vs Stand United, msijidanganye kuhusu…

1084
0
SHARE

img_3887

Na Baraka Mbolembole

Ubora wa Yanga SC hauwezi kufifia kirahisi kama baadhi ya watu wanavyofikiria. Sina shaka kuhusu hilo licha ya kupoteza mchezo wa kwanza kati ya mitano katika ligi kuu Tanzania Bara msimu huu.

Wana wachezaji bora wenye uzoefu ndani ya uwanja na kichapo cha 1-0 walichokipata kutoka kwa Stand United katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga siku ya jana Jumapili kimekuja wakati muhimu sana. Kabla ya kupoteza mchezo huo wa Shinyanga, kikosi cha Hans Van der Pluijm kilikuwa na rekodi ya kupoteza mara moja tu katika game 34 za VPL.

Ikumbukwe mara ya mwisho Yanga kupoteza mchezo wa VPL ilikuwa ni Januari 30 mwaka huu walipolazwa 2-0 na Coastal Union katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Kupoteza mechi mbili kati ya 35 si mbaya. Ila ubaya utakuwapo ikiwa timu hiyo itafungwa katika mchezo dhidi ya mahasimu wao Simba SC mwishoni mwa wiki hii.

STAND 1-0 YANGA

Kwa namna walivyocheza kwa kiwango cha chini katika sehemu ya kiungo, huku mlinzi wa kushoto, Hajji Mwinyi akishindwa kabisa kupeleka mipira sahihi mbele hakika Yanga walistahili kupoteza mechi baada ya Stand kupata goli dakika ya 58.’

Kubwa na muhimu ambalo linapaswa kufanywa na Yanga kama timu ni kujijenga upya na kusahau kila kitu walichofanya msimu uliopita, jambo ambalo ni wazi kabisa wanaweza kulifanya. Msingi mkubwa walionao ni kuwekeza mawazo mapya ya kufanikiwa katika kikosi, ambacho kina mkusanyiko wa vijana na wachezaji wenye uzoefu.

Hans ‘anamiliki’ wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu na hilo waliweza kulionesha wakati walipocheza game 30 na kupoteza mara moja msimu uliopita.

Kiwango cha mchezaji mmoja mmoja na nguvu ni kitu ambacho kiliwafanya wakatawala msimu uliopita na kujenga timu imara zaidi ndicho kitu kilichopo katika mipango ya kocha huyo Mholland ndiyo maana aliwaongeza wachezaji wapya katika kila nafasi.

Beno Kakolanya alikuwa mmoja wa magolikipa bora watatu msimu uliopita akiwa na kikosi cha Tanzania Prisons. Hans alimsajili mchezaji huyo ili kuja kuongeza hamasa kwa magolikipa, Ally Mustapha na Deogratius Munishi.

Mlinzi wa kulia, Hassan Kessy alisajiliwa akitokea Simba kwa lengo la kuongeza nguvu katika fullback namba mbili. Mlinzi wa kati, Vicent Andrew alitua hapo akitokea Mtibwa Sugar, kiungo wa pembeni, Juma Mahadhi na mshambulizi, Obrey Chirwa pia wamesajiliwa ili kuongeza pengo la ubora lililopo baina yao na timu nyingine shindani katika ubingwa.

Kuna mambo machache tu ambayo yakifanyika mabingwa hao mara mbili mfululizo wa VPL wanaweza kushinda taji lao la tatu msimu huu. Kitu muhimu kabisa ambacho Yanga wanapaswa kukifanya, isijaribu kurudia makosa kama wayofanya katika mchezo dhidi ya Stand United kuruhusu goli ambalo lingeweza kuzuilika.

Kiungo wa pembeni wa Stand United, Athanas Pastory ‘alivamia’ kwa kasi lango la Yanga na aliweza kupita katikati ya walinzi, Haji na Andrew kisha na kumfunga kiurahisi golikipa, Ally Mustapha. Ni goli la juhudi binafsi na unapaswa kumsifia mfungaji huyo alitumia vizuri ‘mwanya’ uliachwa wazi na walinzi hao wa Yanga.

Hans anakabiliwa na tatizo jipya katika timu yake-beki wa kushoto na kama anataka kuendelea kuona timu yake ikicheza bila kuruhusu magoli mara kwa mara anapaswa kumtumia ‘kiraka’ Mbuyu Twite katika nafasi hiyo wakati huu kiwango cha Haji kikiwa cha wasiwasi na mbadala wake, Oscar Joshua akiwa katika majeraha ya mara kwa mara.

JUMA ABDUL, KAMUSOKO, NGOMA 

Wachezaji hao watatu walikuwa ‘nguzo’ muhimu ya kikosi kilichotwaa mataji ya VPL na FA Cup msimu uliopita. Juma alizalisha magoli mengi na kufunga katika michezo muhimu akitokea katika beki namba mbili.

Kamusoko licha ya ku-asissts magoli mengi aliweza kufunga zaidi ya mara tano huku Ngoma akifunga magoli 17 katika msimu wake wa kwanza VPL na kusababisha mikwaju kadhaa ya penalti ambayo iliwabeba katika nyakati ngumu.

Mafanikio yao msimu uliopita yatakuwa ni ‘mzigo mkubwa’ msimu huu. Kushindwa kufikia walau asilimia 60 za viwango vyao vya msimu uliopita kwa wachezaji hao watatu itakuwa ni pigo kubwa hasa ikitokea wachezaji wapya kushindwa kufikia viwango vyao walivyokuwa navyo msimu uliopita.

Kila timu inataka kuwafunga wao, na si kuwafunga tu, bali wanataka kuhakikisha hawashindi taji la tatu mfululizo. Kuondoka kwa mchezaji makini kama Salum Telela hakuwezi kuwa pengo kwenye kikosi cha Hans, kwa sababu tayari kocha huyo alishamwona mbadala wake.

Said Juma Makapu, anapaswa kupandisha kiwango chake, huku usajili wa nyota wapya ukipaswa kuongeza nguvu haswa kama kweli wanataka taji la 3 mfululizo. Yanga wana kikosi tishio lakini hakitawapa matokeo ikiwa wachezaji wenyewe watashindwa kutambua kwamba ‘kila timu ina wakamia na inataka kuwafunga wao.’

Stand walicheza kwa nguvu na kujituma kwa muda wote huku wakihakikisha Juma Abdul hapandi na kutengeneza krosi zake, walihakikisha Kamusoko hapigi pasi zake za kupenyeza huku Ibrahim Job akimzima, Ngoma bila kumchezea faulo za kuonekana.

Hakuna timu isiyopoteza mechi na Yanga wamepoteza mechi yao ya kwanza katika michezo 19 ya mwisho katika VPL wakati muhimu sana. Ni muhimu kwa maana wataanza kujiuliza upya kuhusu ubora wao na kuongeza mbinu za kuwafanya kuimarisha matokeo yao bora yaliyopita.

Yanga walistahili kupoteza game ya kwanza msimu huu kwa sababu Stand walijituma na kucheza kwa nguvu zaidi yao katika muda wote wa mchezo. Ila usijidanganye na kuamini kwamba ubora wao umefika tamati. Watarejea kwa nguvu zaidi katika game ijayo na watarudi katika ‘tawi lao la ubora.’

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here