Home Ligi EPL CONTE, KWA SASA FABREGAS NI SUMU

CONTE, KWA SASA FABREGAS NI SUMU

726
0
SHARE

Fabregas

Antonio Conte ni moja kati ya makocha bora na wenye akii nzuri ya mpira pamoja na falsafa ambazo zimekuwa zikimpa matokeo pamoja na mafanikio kwa kipindi kirefu sana. Kama makocha wengine naye ana misimamo yake kutokana na kile anachokiamini pamoja na aina ya wachezaji anaowahitaji ndani ya kikosi. Ameishi Juventus kwa mafanikio huku pia akiwa hakufanya vibaya na timu ya Taifa ya Italia. Kocha ambaye anaamini zaidi katika ulinzi kuliko nguvu ya ushambuliaji kama MSN.

Kwake yeye atampenda zaidi Ngolo Kante kuliko Kevin De Bryune ni kawaida sana. Ni kama ambavyo Pep hawezi kumpokea Matic mbele ya Thiago Alcantara au alivyomkataa Javi Martinez mbele ya mtoto huyu. Falsafa hizi ndizo zilizofanya kuwe na matatizo kati ya makocha wengi dhidi ya wachezaji bora. Hii haiepukiki na wala haizuiliki. Hii ndio sababu leo mchezaji Cesc Fabregas anahaha kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Chelsea.

Fabregas huyu ambaye aliongoza kwa kupiga pasi za magoli wakati Chelsea ikitwaa ubingwa akiwa anatokea eneo la katikati mwa uwanja na wala sio nyuma ya mshambuliaji au katika nafasi ya winga. Hili limebaki kuwa swali kubwa na zito ambalo pengine limebakisha maswali mengi kuliko majibu ambayo kila mpenzi wa soka anaamini kivyake na kichwani mwake binafsi.

Kama ilivyokuwa kwa Baba Rahman, Fabregas naye hayupo kwenye mipango ya Conte. Conte anaamini katika wachezaji ambao wote wanaweza kuwa na uwezo wa kukaba vyema. Lakini kwa eneo la katikati amezoea kuwa na wachezaji wenye akili ya ukabaji zaidi, isipokuwa pale ambapo anaamua kutumia mfumo wa kuwa na mchezaji mbunifu wa chini (deep lying playmaker) kama ilivyokuwa kwa Andre Pirlo.

Huyu anakuwa mchezaji ambaye anacheza mbele ya mabeki wa kati na anakuwa anahusika na kuamua timu nzima icheze vipi.Sio kila mchezaji anaweza kufanya hili, na Cesc hajawahi kufanya hili tofauti na Pirlo ambaye alibadilishwa muda mrefu tangu akiwa kijana AC Milan na bado kote aliwekewa wachezaji wanaoweza kukaba vyema kwa niaba yake. Kumjaribu Fabregas eneo hili ilikuwa ni kujitia kitanzi kwa kocha na hatarishi.

Hivyo Conte akaamua kumwondoa ili nafasi imwendee Kante na Matic. Akaongeza ulinzi na kupunguza ubunifu. Conte alikuwa sahihi sana kutokana na ukweli kuwa asingepata anachotaka kutoka kwa Fabregas, huku pia akikosa ambacho angekipata kutoka kwake huyo huyo. Jambo pekee alilotegemea Conte ni kuwa Oscar na Willian wangempa ubunifu walau nusu ya Fabregas huku wakiongeza pia pressing (kukabia katika eneo la adui) kitu ambacho wanaweza kukifanya kwa ufasaha zaidi kuliko Fabregas ambaye hajajaliwa Mobility (yaani uwezo wa kuzunguka kwa kukimbia eneo kubwa la uwanja).

Bahati mbaya kwa Conte na nzuri kwa Fabregas ni kuwa jiwe alilokataa mwashi limekuwa jiwe kuu la pembeni. Willian hajacheza kwa kiwango chake cha misimu miwili iliyopita na Oscar sio yule aliyeifunga Juventus ya Conte goli la maajabu wakati akiwa ni kuku mwenye Kamba mguuni pale Stamford Bridge. Hii maana yake ubunifu wa timu uwanjani umebaki kwenye miguu ya Hazard ambaye anajaribu kutafuta fomu yake iliyoptea msimu uliopita. Hii inasababisha kukosekana kwa uwiano sahihi na inapelekea Chelsea kuzidiwa katikati mwa uwanja na mkungu unakuwa mzito sana kubewa na mgomba unaoitwa Kante na Matic.

Kuna namna mbili tu ambazo Conte anaweza kuwa salama bila Fabregas kwa sasa. Jambo la kwanza ni kukubali kurahisisha aina ya uchezaji na kuwafanya Willian na Fabregas kucheza kama wakati uliopita kwa maana ya kutanua uwanja sana na kumpa uhuru Oscar wa kutembea anavyotaka. Aina ya pili ni kumwondoa Oscar ili Batshuayi aingie na kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji ambalo litasaidia kuwaweka huru mawinga wake.

Lakini tofauti na hili na kama wachezaji hawatobadilika kuendana na mfumo wake na falsafa anazozihitaji, Conte ataendelea kuadhibiwa na kila ambacho Fabregas atakuwa anakileta uwanjani. Hata kule Man City hakuna anayepiga kelele kwa sababu maamuzi magumu ya Pep Guardiola kuamua kumwacha Yaya Toure nje, yameleta matokeo chanya zaidi. Kwa sasa Fabregas ni sumu kwake, na maziwa ni ama yeye kubadilika na kumrejesha kikosini, kubadili mifumo au kuwafanya anaowaamini wacheze vyema. Tofauti na hili atakufa taratibu.

Nicasius Nicholaus Agwanda (Coutinho Suso)

Follow Instagram @agwandanic

Mwananchi @ J3 & J2. Ukurasa unaitwa Gozi la Ng’ombe

 

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here